Ubalozi wa Tanzania nchini China umetoa taarifa na kusema kuwa kuanzia leo Jumamosi Machi 28, Serikali ya China imesitisha VISA zote za kuingia nchini China na Hati za Ukazi (residence permit), na kwamba Watanzania wenye VISA na wanafunzi wenye hati za ukazi wasitishe mipango ya kurejea China hadi itakapotangazwa.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa kupitia ukurasa wa twitter wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo imeeleza kuwa hatua hiyo imekuja ikiwa ni kuendelea kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya ugonjwa Corona.
Baada ya taarifa hiyo Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema kuwa hatua hiyo ni ya muda mfupi ili kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Corona huku akiwataka Wafanyabiashara waliokuwa wanapanga kwenda nchini humo kuahirisha safari zao.