My Web

Emmanuel

CONTACT

Sunday, September 1, 2013

Sababu tano (5) za wewe kutokata tamaa




Ni rahisi mtu kukata tamaa pale mambo yanapomuendea vibaya au anapopata ugumu ambao hakuutegemea hapo awali alipokuwa akipanga mipango yake. Kukata huko tamaa ndipo panapompelekea mtu kutoweza kufikia makusudio yake. Jambo lolote lililofanyika na kufanikiwa kasoro mbalimbali zilitatuliwa. 

Ni vyema ukaelewa changamoto zitakuwepo katika kila kitu unachotaka kufanya, kwa kufahamu hivyo utaweza kufanya mambo yako mpaka yatimie bila kukatishwa na vikwazo au sababu nyinginezo ikiwemo ''kukata tamaa'' hata pale unapopata shida.
Wazo la kukata tamaa ni adui wa wewe kutofanikisha ulichokianza, hivyo nimeona niandike sababu tano(5) za wewe kutokata tamaa zikusaidie kushikamana na malengo yako.

 1. Kukata tamaa hukufanya ufikie kikomo cha mafanikio.

-Moja ya sababu ya watu wengi kushindwa kufanikiwa katika mambo yao ni kukata tamaa mapema kabla hajafika mbali kuendelea kufanya alichokianza. Kukata tamaa ni kudhihirisha hutaki tena kufanikiwa kwa maana ya hutofanya chochote kuhusiana na hicho ulichoamua kuacha. Kuwa mstahimilivu na ushikamane na malengo yako mpaka mwisho.

2. Kukata tamaa ni kuamua umepoteza muda wako wa thamani.

-Unaweza kuwa umetumia nguvu na muda wako mwingi kufanya kitu fulani ambapo thamani yake ni kubwa ya kuweza kukugarimu iwapo utaachana na malengo yako kwa kukata tamaa. Mfano mzuri ni ‘’usiku wenye giza na mchana wenye mwanga’’ linapoingia giza leo jioni kesho yake hakuwezi pambazuka mpaka upite wakati wa giza nene usiku wa manane ndio mwangaza utokee wakati wa asubuhi. Kwa mfano huo halisi ni kwamba unapokata tamaa wakati huko nyuma umejitahidi kwa kadri uwezavyo ni sawa na kuishia njiani ukiwa umeshafika karibu kabisa na mahali ulipotaka kufika.

3. Kukata tamaa ni dhana mbaya ya kujiona umeshindwa.

-Huna sababu ya kukata tamaa ikiwa wengine wameweza. Ikiwa unataka kufanikiwa muda mzuri wa kujipa matumaini kuwa unaweza ni pale unapojihisi unataka kukata tamaa. Usikubali hisia zako zinazokusukuma ukate tamaa zikutawale. Lady Jay Dee, Asha Rose Migiro au Ali Remtulla wasingeweza kuwa na mafanikio makubwa ya kazi zao kama wangekata tamaa na mambo wanayofanya. Unaposhindwa kitu jaribu tena na tena bila kukata tamaa  na hii ndio siri ya kutumiza malengo yako.

4. Kukata tamaa ni kikwazo kidogo kinachokuzuia kufanya mambo makubwa.

-Mambo yote mazuri tunayoona leo yamehangaikiwa kwa kutengenezwa na kuwa kama yalivyo. Amani na uhuru tulio nao leo wazee wetu na watu mbalimbali walipigania mpaka kufikia sasa. Huwezi jua uwezo wako ni mkubwa kwa kiasi gani mpaka uthubutu kutenda makubwa licha ya kuwa utakumbana na vikwazo. Kutokata tamaa kwako ndiko kutakokuwezesha kufanya mambo makubwa na kukufanya uwe mtu bora uliyekomaa.

5. Kukata tamaa ni kizuizi cha kufikiri njia mbadala ya kuendelea kuyaendea malengo yako.

-Matatizo mengi yanaufumbuzi ikiwa tutafikiri vizuri, kukata tamaa ni sawa na kusema hakuna njia nyingine yeyote ya kutatua shida yako. Kizuizi hiki cha kukata tamaa kinaweza kukufanya ushindwe kufikia malengo yako kwasababu tu yakupungukiwa na mawazo sahihi yakukuwezesha utafute njia mbadala na kuendelea kuyaendea na malengo yako.

No comments:

Post a Comment

New