Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CHADEMA na UKAWA, Bw. Edward Lowassa ameendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bw. Lowassa jana aliendelea na kampeni zake katika majimbo matatu ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni Ukonga, Kigamboni na Mbagala
Jimbo la Ukonga
Akiwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tungine, Jimbo la Ukonga,Bw. Lowassa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CCM wataisoma namba kwani Watanzania wanahitaji mabadiliko.
Alisema anataka kutimiza ndoto yake ya kuondoa umaskini wa Watanzania kwani ana utashi na ataweza kuuondoa kwa nguvu zote ili kuijenga Tanzania mpya wanayoitaka wananchi.
"Nimeamua kugombea urais ili niweze kuwatumikia Watanzania; hivyo naomba mniamini niijenge Tanzania mpya ili kila mtu awezekuishi kwa amani na kujituma kwenye kazi," alisema.
Aliongeza kuwa, akiwa rais atafanya maamuzi magumu ili kuwaonesha Watanzania maana ya mabadiliko na maendeleo yanayohitajika ambapo anayekula mlo mmoja atakula mitatu, mwenye kanga tano awe na kumi lengo ni kuijenga Tanzania yenye maendeleo.
Bw. Lowassa aliahidi kuondoa ushuru kwenye zana za kilimo ili kila mkulima aweze kunufaika na kuuza mazao yake mahali popote iwe ndani au nje ya nchi ili aweze kujipatia kipato cha uhakika.
"Serikali yangu itatoa elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu,nawashangaa viongozi wa CCM wanaposema hawawezi kutoa elimu burewakati wao wanatembelea mashangingi ya gharama kubwa.
"Nilikwenda Pugu kwa daladala ili kutembelea wananchi; wakaanza kuongea kwani hizi daladala za kazi gani, mbona wao wanapandisha twiga kwenye ndege na hawasemi?" alihoji Bw. Lowassa.
Alisema atahakikisha matatizo ya wananchi kama alivyoyataja mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara, ambapo atayatatua ambayo ni pamoja na tatizo la ukosefu wa umeme, umaskini, huduma mbovu za afya, ukosefu wa maji pamoja na hali ngumu ya maisha.
Jimbo la Kigamboni
Bw. Lowassa akiwa kwenye Jimbo la Kigamboni, alisema akiwa rais wananchi watatumia Kivuko cha Kigamboni bure na kujenga upya mji huo ili uwe mfano wa kuigwa.
Jimbo la Mbagala
Akiwa Jimbo la Mbagala katika Uwanja wa Zakheem, alisema ataunda Serikali maalumu ambayo itashughulikia matatizo ya wakazi wa jiji hilo na kuleta maendeleo ya haraka ambayo hayajawahi kutokea.
Juma Duni Haji
Naye mgombea mwenza, Bw. Juma Duni Haji, alisema mwaka huu,CCM lazima waachie Serikali watake wasitake kwani miaka 50 waliyokaa madarakani imekuwa ya dhuluma na kuwanyanyasa wananchi.
Alisema baada ya kuona wanashindwa, wameanza kuleta vurugu kwakuwaambia Watanzania kutakuwepo na vurugu baada ya uchaguzi.
James Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, alisema pamoja na CCM kumpaka matope Bw. Lowassa, wataendelea kusonga mbele hadi waingie Ikulu, hivyo Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake,waanze maandalizi ya kukabidhi Ikulu.
Mbowe amvaa Bulembo, Lubuva
Akihutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Abdallah Bulembo kuwa UKAWA wataachiwa vitu vyote isipokuwa Ikulu ni ya kichochezi.
Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, anatetea kauli hiyo akisema ni maneno ya kisiasa na kumtaka atoe tamko juu ya hilo kwani nchi inaweza kuwaka moto.
"Mtu ambaye atashinda lazima apewe haki yake, Jaji Lubuva asifanye utani na kauli za akina Bulembo, nchi inaweza kuwaka moto, wananchi wapo tayari kwa mabadiliko hivyo wapewe haki yao,"alisema.
Aliongeza kuwa, NEC ilipaswa kukemea kauli za aina hiyo pamoja na kutoa tamko rasmi akitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa UKAWA, kukubaliana na maamuzi ya viongozi wakuu wa umoja huo juu ya kusimamisha mgombea mmoja katika kila jimbo na kata.
"Tuko katikati ya mabadiliko hatutaki mchezo, kiongozi wa NLD, CUF, CHADEMA au NCCR-Mageuzi katika ngazi za kata na wilaya ambaye atadharau maamuzi yetu tutamfukuza," alisema.
Frederick Sumaye
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, alisema hali anayoiona, hakuna sababu ya CCM kubaki madarakani ambapo wanachofanya sasa ni kuwabembeleza na kuwarubuni Watanzania ili wawape kura.
"CCM lazima iondoke madarakani, kote tulikozunguka watu wanataka mabadiliko wakisema Oktoba 25, mwaka huu, wachukue chao kila eneo wakidai CCM ina kiburi," alisema.
Alisema CCM imefilisika na kuishiwa sera ndiyo maana mgombea urais wao, Dkt. Magufuli anajinadi yeye badala ya chama akitumia nembo za CHADEMA; hivyo alimtaka aache kuwadanganya Watanzania.
Dkt. Makongoro Mahanga
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira ambaye alitoka CCM na kuhamia upinzani, Dkt. Makongoro Mahanga, alisema Bw. Lowassa ndiye mwarobaini wa tatizo la ajira.
Alisema inashangaza kuona Dkt. Magufuli kudai ataanzisha mahakama ya mafisadi wakati idadi kubwa ya wagombea ubunge wa CCM wamepata nafasi hizo baada ya kutoa rushwa.