Matunda na mbogamboga ni sehemu muhimu sana katika mlo bora wa chakula. Kutumia kiwango cha matunda na mbogamboga kinachofaa au kukidhi mahitaji ya mwili, kunaweza kusaidia kuzuia magonjwa makubwa yanayowasumbua binadamu walio wengi, kama vile magonjwa ya moyo na saratani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani vifo milioni 1.7, sawa na asilimia 2.8 ya vifo vyote duniani, huchangiwa na matumizi madogo ya matunda na mbogamboga. Aidha, WHO linabainisha kuwa ulaji mdogo wa matunda na mbogamboga, unakadiriwa kusababisha takriban asilimia 14 ya vifo vitokanavyo na saratani za tumbo, asilimia 11 ya vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo na asilimia tisa (9) ya vifo vitokanavyo na kiharusi duniani kote.
SWALI: Je, kuna tofauti gani kati ya Juisi Halisi ya Matunda na Juisi Bandia ya Viwandani?
JIBU: Juisi halisi ya matunda, ni juisi ambayo inatokana na kukamuliwa matunda. Mara nyingi juisi ya aina hii haiongezwi majiwala sukari, ingawa kuna aina ya matunda ambayo inakuwa bora ukiongeza maji kidogo kama vile pesheni, maembe, mananasi na kadhalika.
Juisi halisi za matunda zilizotengenezwa kiwandani huandikwa "100% juice." Juisi hizi mara nyingi huwa na bei ya juu zinapouzwa madukani.
Juisi bandia ni pamoja na vinywaji vyenye rangi mbalimbali vinavyouzwa madukani, ambavyo ni mchanganyiko wa maji, sukari, rangi na ladha bandia ya matunda. Vinywaji hivi hata kisheria haviruhusiwi kuitwa juisi.
Vinapokuwa ndani ya paketi au chupa kwenye lebo huongezewa neno "Drink" na hivyo kusomeka "Juice-Drink". Hii ina maana si juisi halisi ya matunda. Nyingine zimewekwa juisi kwa kiasi kidogo tu kwa hiyo ukisoma lebo utaona asilimia ya juisi iliyowekwa. Wataalam wa masuala ya afya kuwa vinywaji hivi bandia kwa kiasi kikubwa huchangia kuupa mwili nishati-lishe nyingi na havina virutubishi vingine, hivyo kuchangia kuongeza uzito wa mwili tu. Wakati mwingine, juisi bandia hii, huhusishwa na kuongezeka uwezekano wa kupata saratani za aina mbalimbali.
Si kweli kwamba vinywaji hivi vinapokuwa na rangi ya zambarau au nyekundu huongeza damu, bali vinywaji hivyo vimeongezewa rangi ambayo haina virutubishi vyovyote, bali ladha tu ya matunda husika.
SWALI: Je, nitumie kwa kiasi gani matunda na mbogamboga?
JIBU: Ni muhimu kula matunda na mbogamboga kwa wingi kila siku, hasa wakati wa mlo. Unashauriwa kula mbogamboga na matunda ya rangi mbalimbali kwa kuwa rangi zinapokuwa za aina mbalimbali, ubora wake huongezeka.
Inashauriwa kutumia angalau vipimo vitano vya mbogamboga na matunda kila siku. Mfano wa kipimo kimoja kinachotakiwa ni karoti zilizokatwakatwa na kupikwa kiasi cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250 mls), mboga za majani zilizopikwa kama mchicha au matembele kiasi cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250 mls), mboga zisizopikwa (kachumbari/saladi)- bakuli moja kubwa ujazo unaoweza kuchukua mlo wa mtu mmoja.
Chungwa moja zima, ndizi mbivu moja kubwa kiasi, tikiti-maji kipande kikubwa kimoja, parachichi moja dogo, mapera mawili na Juisi Halisi glasi moja (250 mls).
Kwa siku moja (asubuhi hadi usiku), mtu anashauriwa kula kama ifuatavyo; na hii iwe ni katika kila mlo siku nzima. Glasi moja ya juisi, mapera mawili, mchicha uliopikwa kiasi cha ujazo wa kikombe cha chai (250 mls), matembele yaliyopikwa kiasi cha ujazo wa kikombe kimoja cha chai (250 mls) na saladi bakuli moja.
Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa kushirikiana na WHO, katika ripoti yao ya hivi karibuni kabisa kuhusu ulaji bora wa matunda, wanashauri kula angalau gramu 400 za matunda na mbogamboga kila siku kwa ajili ya kuzuia magonjwa sugu kama ya moyo, saratani, kisukari na kitambi, ikiwa ni pamoja na kuzuia na kuondoa upungufu wa vitamini na madini muhimu mwilini, hasa kwenye nchi zinazoendelea.
SWALI: Je, nitakuwa na madhara gani ya kiafya kama nikiamua kutumia juisi tu badala ya matunda au mbogamboga?
JIBU: Juisi Halisi ya Matunda inaweza kuwa sehemu ya matunda, ingawa hata hivyo haiwezi kuwa mbadala wa matunda au mbogamboga. Katika vipimo vitano vya mbogamboga na matunda unavyotakiwa kutumia kwa siku, juisi inahesabika kama kipimo kimoja tu hata kama utakunywa nyingi kiasi gani.
Ina maana kwamba ni lazima pia kula matunda na mbogamboga kila siku kwa kwa kuwa matunda na mbogamboga vina makapi-mlo ambavyo havipatikani kwenye juisi. Matunda mengine huliwa na maganda yake ambayo huongeza ubora wake. Kwa hiyo, glasi moja ya Juisi Halisi kwa kwa siku inatosha, lakini mtu akipenda anaweza kunywa zaidi ya hapo.
No comments:
Post a Comment