My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, July 17, 2018

CHAKULA MUHIMU CHA MJAMZITO

BAADHI ya vyakula ambavyo mama anapaswa kula awapo mjamzito na vile anavyotakiwa kuviepuka katika kipindi hicho tutavijadili leo.

Mjamzitto anashauriwa kula vyakula vyenye vitamini kwa wingi kila siku. Ili kumjenga mtoto, mama anapaswa kula vyakula vyenye folic acid na vitamini B12 ili kujenga seli nyekundu za damu, vitamini C ili kuzalisha collagen, vitamini D kwa ajili ya kujenga mfupa, na zinki kwa ajili ya maendeleo na kukuza ubongo.
Kila mjamzito anapohudhuria kliniki amekuwa akishauriwa kupatiwa vidonge vya aina ya folic acid. Kwa bahati mbaya, baadhi yao huwa hawavimezi, jambo linalowakosesha watoto walio tumboni virutubisho muhimu kwa ajili ya afya ya ubongo.


PROTINI

Mjamzito anapaswa kula vyakula vyenye utajiri wa protini kama vile samaki, vinaongeza nguvu ya ubongo wa mtoto aliye tumboni.
Utafiti kutoka Harvard Medical School, ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani unaeleza kuwa ulaji wa samaki kwa wingi wakati wa ujauzito, hasa katika miezi sita ya mwanzo, huchangia kuujenga ubongo wa mtoto tumboni.
“Vyakula vyenye protini kwa wingi hujenga seli muhimu kuufanya ubongo wa mtoto tumboni kufanya kazi haraka,” anasema Profesa Lisa Eliot wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Rosalind Franklin, kilichopo Chicago, Marekani.
Profesa Eliot, anashauri kuwa kama mama hapendi samaki, azungumze na daktari wake ili amshauri vyakula mbadala au vidonge vya mafuta ya samaki.
Hata hivyo, wajawazito wanashauriwa wachukue tahadhari kwani baadhi ya samaki wana madini ya zebaki ambayo yanaweza kumletea madhara.
Kazi nyingine ya protini ni kujenga seli na homoni kwa ajili ya ukuaji wa mtoto tumboni.
Baadhi ya vyakula vingine ambavyo havina gharama makubwa, ni supu ya maharage au mboga za majani, siagi pamoja na karanga.
Vyakula vingine vyenye protini kwa wingi ni maziwa, nyama na mayai. Napendekeza pia ulaji wa matunda kwa wingi kwa mjamzito.
Matunda yana virutubisho kwa ajili ya afya ya ubongo wa mtoto tumboni na kulinda tishu za eneo hilo zisiharibiwe. Baadhi ya matunda ambayo mama anaweza kula ni machungwa, papai, parachichi, ndizi mbivu na hata nyanya, huku akizingatia kuosha kwa maji safi kabla ya kula.


MADINI YA CHUMA

Mjamzito unashuriwa kula vyakula vyenye chuma kwa wingi. Ulaji wa vyakula vyenye madini ya chuma wakati wa ujauzito, husaidia katika usambazaji wa endelevu oksijeni kwa mtoto na kukabili tatizo la upungufu wa damu.
Hata hivyo, wanawake wengi hupata ujauzito wakiwa tayari na upungufu wa madini hayo na nawashauri kuwa mjamzito achunguze wingi wa madini hayo aendapo kliniki ili aweze kuchukua hatua stahiki.
Karibu asilimia 85 ya upungufu wa damu au anaemia wakati wa ujauzito
husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini.
Upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini haya au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini ya chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kikubwa wakati wa hedhi, kabla ya kushika mimba.
Baadhi ya vyakula vyenye utajiri wa madini ya chuma ni nyama, samaki, kunde, dagaa, kabichi na jamii yote ya nafaka.


TAHADHARI

Jihadhari na pombe. Matumizi yoyote ya pombe yana athari kwenye afya ya ubongo wa mtoto tumboni kwani husababisha matatizo ya uwezo wa mtoto kujifunza na kutunza kumbukumbu.
Usiongezeke uzito kupita kiasi. Pamoja na kwamba mjamzito anakula zaidi anapaswa kudhibiti uzito wake kwani uzito mkubwa unamuweka kwenye hatari ya kujifungua kabla ya wakati yaani kupata mtoto njiti.

No comments:

Post a Comment

New