Wiki hii tunaendelea na sehemu nyingine ya mada yetu ya dhana zinazowaharibia wanawake kimapenzi ikiwa ni mwendelezo wa pale tulipoishia wiki iliyopita.
Ukiacha mateso ya Janette baada ya kutoswa na Mully aliporudi mara ya pili, Jambo la kuzingatia ni jinsi alivyomtenda boyfriend wake aliyekuwa anamhudumia na kwenda kuangukia kwa mwanaume ambaye ni mume wa mtu. Hakutafakari mwenye faida kwake ni nani, leo anahangaika.
Aina ya wanawake kama Janette ndiyo wanaosababisha wanaume watambe mitaani wakitoa maneno ya kebehi kwamba wanawake wote mwalimu wao ni kipofu. Hakutambua jema wala hakujua kwenye maisha haya anahitaji nini.
Mtu anayejihusisha kimapenzi na mume au mke wa mtu, maana yake hajui kesho yake ni nini.
Mully ni mmoja wa waathirika, wapo wanaume wengi waliotendwa na wapenzi wao ambao waliwalea na kutumia fedha nyingi kuwasomesha. Mambo yao yalipokaa sawa na kupata kazi, wakasahau walipotoka na kuanzisha uhusiano na wengine. Kipya kinyemi, mume aliyemsomesha akatupwa mbali.
Janette na wengine wenye tabia za namna hiyo ni mwendelezo wa dhana zinazowaharibia wanawake kimapenzi. Wanatakiwa wajirekebishe ili mambo yakae sawa. Wasiwaponze wengine wenye tabia safi, wenye akili hai za kulea familia yenye mafanikio tele.
Ipo dhana nyingine kuwa mwanamke akipendwa sana, hujenga kiburi na matokeo yake humdharau mwanaume anayeonesha mahaba ya ndani kabisa. Kwamba anaweza kumgeuza mwanaume punda kwa sababu tu anajua anampenda.
Hachukulii upendo ni tunu, yeye anaubeba kama fimbo ya kuchapia.
Nimeshakutana na watu kadhaa, wananieleza matatizo yao na jinsi walivyoshauriwa na watu mbalimbali. Mathalan, mtu mke wake anamsumbua, anamueleza mshauri kila kitu kinachozunguka mgogoro ndani ya familia yake. Mwisho katika kushauriwa anaambiwa: “Tatizo, umemuonesha mkeo unampenda sana.”
Je, kumuonesha mtu kuwa unampenda ndiyo igeuke adhabu kwako? Ni wazi kuwa mapenzi ya siku hizi, yanatawaliwa na nguvu kubwa ya shetani ndiyo maana tafsiri yake inakosewa. Ukweli wa mapenzi ni kuwa wawili wanaoamua kupendana ni lazima upendo wao uwe wa ndani ya nyoyo zao na waudhihirishe kwa vitendo.
Ni mateso kujilazimisha kuficha mapenzi, eti unahofia ukimuonesha atajua na atakufanyia vitimbi. Kufanya hivyo ni mateso, bora kutopenda kabisa. Inatupasa kupendana bila kuwa na shaka yoyote ndani. Kila mtu ausikilize moyo wake namna unavyomuongoza na atende pasipo kuhofia kuitwa Bushoke.
Wakati nashauri kwa watu kuruhusu nyoyo zao ziwaongoze katika kudhihirisha mapenzi yao bila kuogopa jinsi watakavyochukuliwa na jamii, ni vema nikatoa angalizo kwa wale wanaooneshwa mapenzi, kuheshimu hisia za wenzao. Maisha ya sasa, kupata mtu anayekupenda, anayekujali na kukuheshimu kwa dhati, ni bahati.
Ukigundua ni bahati, basi ni vizuri kuitunza kwelikweli, vinginevyo unaweza kuichezea, ukaipoteza, matokeo yake ni kujuta baadaye. Usimfanye mwenzi wako ashindwe kukuonesha penzi la dhati. Mpe uhuru na amani juu yako. Mpokee vizuri, zungumza naye kwa lugha tamu ili ajisikie kuwa nawe.Ni vipi mwenzio kwa mapenzi aamue kukununulia zawadi aliyoona inafaa, wewe kwa sababu unamdharau kutokana na jinsi anavyokupenda kupitiliza, unaitazama kwa nyodo kisha unapotezea. Husemi hata asante. Inawezekana inakuvutia lakini hutaki tu kumuonesha kwa sababu unamuona katuni, kisa anakupenda kupitiliza.
Mwenzio ametulia, anaona akutoe ‘auti’, mwende sehemu mkapate chakula cha jioni. Hisia zako za dharau juu yake, iliyotokana na mtazamo kuwa anakupenda mpaka kero, unaamua kukataa bila sababu: “Sitaki tu kwenda, acha nipumzike nyumbani.”
No comments:
Post a Comment