Na Luqman Maloto
Ushamba wa mapenzi alionao dogo ‘mgonjwa’ wa warembo, Naseeb Abdul ‘Diamond’ (pichani), umekwenda hatua mbaya zaidi, alichokifanya Uingereza hivi karibuni, kimeshusha thamani yake kutoka geji hafifu hadi sifuri.
Akiwa Uingereza, Diamond alibwabwaja maneno ‘mbofumbofu’ ambayo siyo tu kwamba yalimfanya azomewe jukwaani, bali pia yaliwadhalilisha warembo wenye majina makubwa Bongo, Wema Sepetu na Jokate Mwegelo.
Inadaiwa kuwa Diamond akiwa katikati ya shoo kwenye ukumbi mmoja jijini London, alisimamisha muziki halafu akawaambia mashabiki waliohudhuria, wamchagulie mpenzi wa maisha yake, kati ya Wema na Jokate.
Madai yanaanikwa kwamba kitendo hicho, kiliwakera mashabiki ambao walilipuka na kumzomea, huku wengi wakimponda kwa kumwita limbukeni wa mapenzi, anayetumia umaarufu wake vibaya kuwachezea warembo.
Mashabiki mbalimbali wametoa maoni kwamba kauli ya Diamond kuwa hamjui mpenzi wake kati ya Wema na Jokate, inatosha kuchangamsha ubongo wa warembo hao ili wajivue gamba mapema na endapo wataendelea naye, basi nao wataonekana ni sifuri.
Dongo hilo la mashabiki, linanogesha kama siyo kusherehesha msemo kuwa mia halali kitanda kimoja na nunge, siku zote ziro huchangia shuka na sifuri kwa sababu ndiyo wanaofanana kuanzia thamani mpaka umbile.
Kwa upande mwingine, kauli ya Diamond imeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao mbalimbali, huku kipande cha video, kinachomuonesha ‘dogo huyo mpenda sifa’ akibwabwaja jukwaani kikisambazwa kwa fujo kupitia intaneti na kuchangiwa maoni ya kufuru.
Kuweka pamoja maelfu ya maoni yaliyotumwa, wachangiaji wamemwita Diamond ni mchafuzi wa watoto wa kike, hana mapenzi ya kweli, gusa unate, mkuki popote na mengineyo ambayo hayana tafsiri nzuri kwa ‘dogo huyo’ aliyekulia Tandale, Dar.
Promota mmoja wa Uingereza (jina tunalo), aliliambia gazeti hili kuwa alipanga kumpa shoo tatu Diamond katika majiji ya Leads, Swansea na Leiceste lakini aliahirisha baada ya kuona amewachafua mashabiki na hakubaliki tena.
NI TUSI KUBWA KWA WEMA
Oktoba 2, 2011, Diamond kwa utashi wake, bila kulazimishwa, alijishaua kumvisha pete ya uchumba, Wema ambaye ni staa wa filamu mwenye taji la Miss Tanzania 2006-07.
Diamond, alimvalisha pete Wema na kuahidi kufunga naye ndoa katika tukio kubwa la shoo ya siku yake ya kuzaliwa, iliyochukua nafasi ndani ya New Maisha Club, Masaki, Dar es Salaam.
Wakati Diamond anautangazia ulimwengu kuwa Wema ndiye mke wake mtarajiwa, Jokate ambaye ni Miss Tanzania namba mbili 2006-07, alikuwepo.
Kwa mujibu wa watoa maoni, tusi kwa Wema ni kuwa kumbe alivishwa pete kanyaboya isiyo na mapenzi ya moyoni, kama ni mpira, basi alipangwa kikosi cha kwanza kwa ajili ya kumshikia nafasi mchezaji mwenye namba yake.
UKWELI NI UPI?
Jokate anaendelea kusisitiza kwamba hajawahi kukwea kitandani na Diamond, isipokuwa yupo karibu na ‘bwa mdogo’ huyo mpenda wa’mama kwa ajili ya kazi tu.
Wema anadai anao ushahidi kuwa Jokate kaanguka dhambini, wakati huo huo Diamond naye anajichetua ili aonekane kidume cha mbegu kwa kuomba mashabiki wamchagulie anayefaa.
HESHIMA YA JOKATE
Kabla ya tukio hilo, Jokate ni mrembo maarufu ambaye heshima yake kwenye jamii ilikuwa juu kutokana na jinsi alivyoendesha mtindo wa maisha yake.
Tathmini inaonesha kuwa tangu alivyoanza kuhusishwa kutoka kimapenzi na Diamond, heshima yake imepungua, huku watu wengi wanaompenda wakisema kwamba mrembo huyo ameingia ‘chaka’.
Kitendo cha Diamond kumuweka mezani na Wema, kisha kumchezesha bahati nasibu kama atashinda au la, kimezidi kuporomosha heshima ya Jokate.
Mrembo huyo ambaye amekuwa akifanya kazi nyingi za harakati, ameshauriwa kuwa hadhi yake ni kubwa, hivyo haipendezi kugombania sadakalawe na Wema ili kumpata Diamond.
KUTOKA RISASI
Wema na Jokate, kama kuna makosa ambayo mmefanya ni wakati wenu kujisahihisha. Mungu amewajaalia vipaji na nyota za umaarufu, haivutii mkatumiwa bila heshima mithili ya vitanda vya nyumba za kulala wageni.
Maisha yenu ni mazuri endapo mtaamua kushika yenye faida. Kwa Diamond, vema akajikosoa, umri wake ni mdogo, kwa hiyo anatakiwa kuzingatia kwamba anaweza kuzunguka mabucha nyama ni ileile. Akidanganywa na ujana, fainali uzeeni.
No comments:
Post a Comment