My Web

Emmanuel

CONTACT

Saturday, January 28, 2012

Umempoteza na unataka kumrudisha mikononi mwako? - 3

...dondoo hizi zitakusaidia sana
KAMA ni kweli unataka kufanikiwa, ishi kwa upendo na wenzako. Uwe na furaha muda wote, shirikiana na wenzako na penda zaidi majadiliano kuliko uamuzi wa peke yako ambao mara nyingi husababisha matatizo.
Rafiki zangu, nimeanza na utangulizi huo kwa sababu naamini kuna baadhi ya watu wenye tabia hizo. Upendo ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha. Ukiwapenda wenzako, hata milango ya riziki hufunguka.
Nazungumza na wale ambao wameachana na wenzi wao kwa sababu mbalimbali, lakini baada ya kujichunguza kwa muda, wamegundua kwamba bado wana nafasi katika mioyo yao. Wanataka kuwarudisha.
Mengi nilishaeleza katika matoleo mawili yaliyopita. Leo nahitimisha mada hii. Hebu twende tukaone vipengele vilivyosalia.



OUTING

Kutokana na ukaribu wenu, kumwalika katika mtoko wa chakula cha mchana au usiku, haitakuwa vigumu kwake. Hiyo itakuwa njia nyingine ya kumfanya awe karibu yako zaidi.
Mkiwa katika mtoko huna haja ya kuzungumza chochote kuhusu uhusiano wenu, labda kama yeye ataanzisha mjadala huo. Ongelea mambo mengine ambayo ni maarufu zaidi labda katika duru za siasa, sanaa n.k lakini si mambo yanayohusu mapenzi kabisa.
Kama kichwani mwake alikuwa amekufanya kama rafiki yake wa kawaida, mtazamo utaanza kubadilika taratibu na kuanza kutamani kurudi tena mikononi mwako. Jaribu kufikiria, kama umetoka naye, akiamini labda unataka kumuomba msamaha na kurudiana naye, wewe unaanza stori za soka! 
Bila shaka atajiona kama mpumbavu kichwani, si ajabu akaamua kujifunga mwenyewe kwa kuomba urudi tena kwake.





JADILI PENZI LENU


Hatua hii ndiyo muhimu zaidi hapa; sasa unatakiwa kuanza kuzungumzia juu ya uhusiano wenu. Mwambie jinsi ulivyokuwa ukifurahishwa na mapenzi yenu. Msifie alivyokuwa anajua majukumu yake na kukuonesha mapenzi ya dhati.
Si vibaya kama utamweleza pia sababu ambazo unahisi zilisababisha wewe na yeye kuachana. Kwa kauli hizo utampa nafasi ya kuchambua/kumjua mwenye makosa na mahali pa kurekebisha.



KIRI MAKOSA YAKO
I

kiwa kuna mahali unaamini ulikwenda kinyume na yamkini ndiyo sababu kuu iliyosababisha muachane, kiri makosa yako mbele yake. Mweleze kwamba wewe ndiyo chanzo cha matatizo na huenda kama si kukosea, msingeachana.
Kujutia hasa kama uso wako utawakilisha vyema kilicho moyoni mwako, kutamfanya akuone muungwana ambaye unatambua ulipojikwaa na sasa unataka kurekebisha makosa yako. Hapo utakuwa na nafasi kubwa ya kumnasa kwa mara nyingine.



MWELEZE YAKO YA MOYONI


Sasa huna sababu ya kuendelea kujitesa, toa dukuduku lako. Mwambie moja kwa moja kilichopo moyoni mwako. Kwamba unahitaji nafasi nyingine kwake, maana umeshajua makosa yako.
Hii ni nafasi ambayo si rahisi kabisa kuchomoka. Itumie vilivyo. Sauti yako pekee itoshe kumaanisha kile kilichopo moyoni mwako. Lazima atakuelewa.
Kama utakuwa umefuata kwa makini vipengele vyote hapo juu, lazima urudi tena mikononi mwake. Kuna nini tena? Ameshakuwa wako huyo, ila kuwa makini usimpoteze tena.

AKIKATAA JE?
Pamoja na kufuata vipengele vyote hivyo, inawezekana akakataa. Kukataa kwake lazima kuna sababu nyingi. Mwingine anaweza kukuambia moja kwa moja sababu za kukataa kurudiana na wewe wakati mwingine anaweza asiseme chochote.
Huenda akakumbia kwamba tayari ana mtu wake, au hafikirii kurudi mikononi mwako; usihuzunike.
Ni bora sana huyu anayekuambia ukweli, kuliko kurudi halafu ukutane na mateso yale yale.Inawezekana labda hana mapenzi na wewe. Kama ndivyo, kuna sababu gani ya kujikomba? Kubaliana na ukweli, halafu subiri mwingine!
Sikia, subiri mwingine na siyo utafute, maana mwenzi wa kweli huja mwenyewe, hatafutwi! Naamini somo limeeleweka vyema.

JK AKUTANA NA KUFANYA MAONGEZI NA WAZIRI MKUU WA UINGEREZA DAVID CAMERON MJINI DAVOS

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika maongezi na Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron walipokutana mjini Davos pembeni mwa Kongamano la Uchumi la Dunia jana Januari 26, 2012. Picha na Ikulu

Wednesday, January 25, 2012

WEMA: DIAMOND ANA NUKSI

Wema Isaac Sepetu.

Naseeb Abdul ‘Diamond’.

Na Shakoor Jongo
STAA mwenye nyota ya kukubalika Bongo, Wema Isaac Sepetu amecharuka, safari hii anatengeneza kichwa cha habari akimtuhumu aliyekuwa mchumba wake, Naseeb Abdul ‘Diamond’ kuwa ana nuksi, Risasi Mchanganyiko pekee lina data mkononi.
Wema aliye Miss Tanzania mwaka 2006 na msanii anayetingisha kwenye soko la filamu za Kibongo kwa sasa, alisema hayo mara baada ya kutoka kwa habari katika gazeti moja linalotoka mara mbili kwa wiki, ikidai bado anamng’ang’ania Diamond.
Katika habari hiyo, Diamond anamtuhumu Wema kuendelea kumganda na kwamba alimfuata nyumbani kwake Sinza Mori, jirani na Baa ya Meeda alipohamia hivi karibuni, kwa lengo la kujaribu kutafuta suluhu.

WEMA ATEMA CHECHE
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu, juzi Jumatatu, Wema alisema hana mpango tena na Diamond kama alivyodai kwenye gazeti hilo.
“Sifikirii kuwa naye, halafu mimi ndiye niliyemtema...kwa nini nimhangaikie? Anataka kutafuta umaarufu kupitia jina langu. Kwa nini asifanye mambo yake?
“Sijazoea kujibizana kwenye magazeti, kama anataka kusema, aendelee lakini mimi sipo tayari kwa malumbano. Halafu namshangaa sana, kwa nini anamwingiza mama yangu kwenye haya mambo yasiyomhusu?” alifoka Wema.
Alisema, alichokiongea Diamond ni ‘utumbo’ tu na hakuna cha maana kilichomwingia akilini, zaidi ya kumuona kama mfa maji anayetapatapa.

DIAMOND ANA NUKSI
Akienda mbali zaidi, Wema alifunguka kuwa kwa kipindi alichokuwa na Diamond, dili zake nyingi zilikuwa haziendi poa lakini muda mfupi baada ya kuachana naye, kila kitu kinakwenda sawa.
Kwa kauli hiyo, Wema anaonekana kumaanisha kuwa Diamond ana nuksi, ndiyo maana baada ya kutemana naye anakula kuku kwa mrija.
Alisema: “Sikupata kitu nikiwa na Diamond zaidi ya nuksi... tangu nimeachana naye naona mambo yangu yananyooka. Naomba aniache nipange maisha yangu...
“Nipo happy kuliko nilivyokuwa naye, mambo yangu yanakwenda sawa zaidi kuliko mwanzo, sitaki kusikia habari zake. Sitaki kurudia mambo ya zamani ambayo kwangu mimi hayana maana.
“Sasa hivi naishi maisha mapya, nina mipango yangu na inakwenda vizuri, huyo Diamond ni nani kwangu? Sitaki kumsikia kabisa. Nina kazi nyingi za kufanya, siyo kulumbana naye na kufaidisha watu.”
Akaongeza: “Diamond ameshajua nina nyota nzuri, sasa asinitumie kujipandisha chati. Sitaki anishirikishe kwenye mambo yake na nimeshaamua kwamba sitaki kuwa naye, hata yeye anajua. Awe mkweli.”

AMUONYA DIAMOND
Wema alitoa onyo kali kwa Diamond, akimtaka aache kumfuatafuta kwa kuwa kwa sasa kila mtu ana maisha yake.
“Diamond anatakiwa kufahamu kwamba nimeshaachana naye. Basi aniache...Diamond aniache...aniache Diamond...sitaki tena kumsikia. Aniache please,” alisema.

Monday, January 23, 2012

Mwaka 2012, badilisha fikra chakavu kuhusu mapenzi-3

Na luqman maloto

Tunaendelea na sehemu ya tatu ya mada yetu tuliyoianza wiki mbili zilizopita juu ya namna ya kubadili fikra chakavu kuhusu mapenzi.

ANGALIA USIPITWE NA WAKATI
Kwa kawaida, mtu ambaye ni mjanja wa mapenzi anabaki kuwa namba moja katika kuhakikisha hapitwi na wakati. Ikiwa hujali hisia za mwenzi wako, wewe utaonekana walewale. Badilika leo na uzichange karata zako vizuri, mwenzi wako anakuhitaji, anataka ukweli wako, kujali kwako, huruma yako na anapenda sifa zake njema zitamkwe na kinywa chako.
Mwanasaikolojia Born Lewis wa Marekani katika makala yake “Your Sentimental and True Love” anasema:
“Inakuhitaji uwe mwelewa zaidi wa hisia za mwenzako ili uweze kudumu. Mfano; Msome na ujue kwamba anahitaji kusifiwa halafu umsifie. Akienda kupewa sifa na mtu wa pembeni atajua humkubali. Hilo ni kosa kubwa katika mapenzi.”
Lewis anafafanua: “Ni kosa kubwa kwenda kumpongeza mfanyakazi mwenzako kwa muonekano wake, wakati hujafanya hivyo kwa mpenzi wako nyumbani. Ukitaka kujua kwamba inauma, fikiria mwenzio amekuona ulivyovaa na hakukwambia kitu lakini unapata taarifa kuwa amemsifia jirani yenu. Itakuuma, itakupunguza imani yako kwa mwenzi wako.”
Sherry na Mosses ni wapenzi lakini hata siku moja Sherry hajawahi kuonesha kwamba anamkubali Mosses ingawa penzi lao linazidi kuvuta miaka. Ilivyo ni kwamba mara nyingi ni Mosses ndiye huonesha hisia zake kwa Sherry na hata marafiki zao hufikia kusema kwamba jamaa ndiye anayesababisha uhusiano wao uendelee kuwepo, vinginevyo wangekuwa wamekwishapigana mwereka.
Sherry anapoambiwa amependeza anajibu ‘asante’ halafu imetoka. Akiambiwa yeye ni mwanamke mzuri jibu ni ‘thank you’. Hathubutu kumwambia Mosses kuwa amependeza au ni mwanaume anayemvutia kuliko wote, ila akiwa kazini kwake, pongezi huzimwaga huko. “James umependeza!” Sherry anamwambia mfanyakazi mwenzake.
Wakati mwingine Sherry anakosa hekima, anamueleza Mosses: “Unajua sisi pale kazini kwetu kuna vijana wazuri. Unajua Jamal ana sura nzuri sana? Halafu Sam anajua kupigilia mavazi ukimuona hadi raha.”
Inawezekana Sherry anazungumza kweli lakini kichwani kwake kuna kelele za ndani (internal noise) zinazomsababishia umapepe, hivyo kukosa busara ya kuchagua maneno mbele ya mpenzi wake.
Ukitaka kujua mkuki kwa nguruwe, siku moja Sherry alikutana na Zawadi ambaye ni mfanyakazi mwenzake Mosses. Zawadi akaamua kuwa mkweli: “Mosses nimemuacha ofisini ila kanifurahisha, amenisifia huyo. Anasema nimependeza sana leo.” Ilikuwa ni kama Zawadi kamroga Mosses kwani Sherry alikasirika mno siku hiyo.
Walipokutana nyumbani, Sherry alitaka maelezo ni kwa nini alimsifia Zawadi kwamba amependeza badala ya sifa hizo kuzielekeza kwake. Mosses akaona mpenzi wake anampanda kichwani, akamjibu: “Mbona wewe huwa unawasifia wanaume wa kazini kwako mimi sisemi, tena mbele yangu.” Sherry ikamgonga kichwani, akapata pointi!
Sherry hakujua kwamba sifa alizokuwa anazimwaga kwa wanaume wa kazini kwake ilikuwa sawa na kuchezea hisia za Mosses. Haikumgonga kichwani kwamba anamuumiza mwenzake. Alipokutana na Zawadi ikawa maumivu kwake. Kila mtu anatakiwa kujali, kusifu kwa sababu hivyo ni vionjo muhimu kwenye mapenzi.
Kama hukubali kwa jinsi mwenzi wako alivyo ni bora kuachana naye kuliko kupotezeana muda. Tambua kuwa usipomsifu wewe anapokwenda atasifiwa halafu ukisikia itakuuma. Wewe humuelezi kama ni mzuri, anapokwenda wapo watakaomuona watamwambia anavutia, je, hapo huoni kama utakuwa umepoteza kura kwa mwenzi wako?

Mwaka 2012, badilisha fikra chakavu kuhusu mapenzi-2

Na Luqman Maloto
Wiki iliyopita tulianza kuijadili mada hii ya kubadilisha fikra chakavu kuhusu mapenzi na kuishia kwenye mfano wa wapenzi wawili, Justin na Jamie. Justin anamlalamikia mpenzi wake kuwa kuna mambo ambayo huwa hamtekelezei na huwa hamuonei wivu kabisa. Wiki hii tunaendelea na mfano huo ambapo Justin anazidi kumlalamikia mpenzi wake huyo.
Justin anasema...

“Nikiwaona marafiki zangu jinsi wao na wapenzi wao wanavyoishi, nashangaa kwangu mbona haiwi hivyo? Naweza kuwa mbali naye hata kwa siku mbili lakini wala hashtuki, haniulizi.
“Tukikutana haoneshi shauku ya kuwa na mimi mpaka nahisi thamani yangu kwake ni ndogo. Hajawahi hata kunikumbatia na hasemi kama alikuwa amenimisi. Nyumbani kwangu naishi peke yangu lakini hutamsikia akisema anataka kuja mpaka nimuombe, tena kwa kumbembeleza, wakati mwingine anasema yupo bize.
“Tukiwa katika ulingo wa mapenzi haoneshi msisimko. Nijuavyo mimi wanawake wengine hutoa hamasa kwa kuangusha kilio fulani cha mahaba na kusifia jinsi kazi inavyofanyika, Jamie yeye habari hiyo hana. Hata nyonga yake anaibania. Ukimuuliza kama anatosheka anadai anafika bila wasiwasi. Hapa ndipo anaponifanya nijiulize maswali mengi.

“Mara mbili nimejikuta nikitoka na rafiki zake wawili. Wa kwanza alionesha ananijali kuliko hata Jamie mwenyewe. Nilipotoka naye nilijiona mwanaume kamili hasa. Ananiuliza maswali ya mahaba, ananikumbatia kwa bashasha kila tunapokutana. Tukiwa kwenye shughuli ananionesha jinsi anavyoridhika na mimi.
“Mwingine hivyohivyo, tunapomaliza mchezo ananimwagia sifa kemkemu, ananiambia hajapata mwanaume aliyemsafirisha kule ambako nimempeleka. Katikati ya mahaba ananililia kwa sauti fulani ya kutoka puani. Kusema ukweli, hao marafiki wamenikosha kiasi ambacho naona thamani yao ni kubwa kuliko Jamie.
“Vile vilio vya kimahaba, sauti za kubembeleza na pongezi baada ya kazi ni kitu kikubwa kwangu. Hata kama ni sifa za uongo lakini mimi zinanipeleka pale ninapotaka. Sijisikii kwenda faragha na mtu ambaye mimi najitahidi kumfurahisha na kumridhisha lakini yeye ananitolea macho utadhani hana hisia. Najisikia kumchoka!”
Kauli ya Justin kama nilivyomnukuu kwenye makala haya, inaweza kuwa fundisho kwako kwa sababu wengi wamejikuta wakipoteza mvuto wao, kisa ni vitu vidogo.
Hii ndiyo sababu ya kumtaka kila mmoja kuzingatia yale ambayo mwenzi wake atakuwa anapenda na kutekeleza kwa kiwango bora ili kumridhisha. Sanaa ya mapenzi kama ambavyo nimekuwa nikipigania kuisambaza siku zote, inamtaka mtu kuishi ndani ya mwenzake. Kuugua kwa maumivu, kuhuzunika katika majonzi na kufurahia palipo na sherehe.

Ni kituko mwenzi wako anaumia wewe unacheka. Yupo kwenye maumivu makali, wakati huo kwa upande wako ni chereko kwa kwenda mbele. Aina hii ya maisha haiwezi kuwa sawa na haikubaliki. Unapaswa kumjali mpenzi wako hata kama haikugusi lakini machoni muoneshe kuwa upo pamoja naye, vinginevyo ni mateso kwako.
Zingatia: Inawezekana mwenzi wako hakwambii lakini ukweli usimame kwenye kipimo chake kwamba anahitaji manjonjo yako ili afurahie penzi. Kama humtekelezei, tambua anaumia kwa sababu unabana.

Mwaka 2012, badilisha fikra chakavu kuhusu mapenzi

Ni mwaka mpya wa 2012, inakubidi na wewe uwe na fikra mpya. Uondokane na vitu ambavyo vinaweza kukuondolea mvuto au kukuingiza kwenye migogoro. Jiepushe na kila kilichokugombanisha na mwenzi wako.

Ni vizuri uwe na hisia hizo ili somo hili likuingie sawia. Mapenzi hayahitaji ugumu. Huwezi kusifiwa kwa kushindwa kumnyenyekea mwenzi wako. Jeuri dhidi ya mwenzako, maana yake una alama ‘F’ kwenye mapenzi.

Kila mtu anapenda kuonewa wivu ili awe na uthibitisho kuhusu mvuto wake. Anahitaji kujua kama anapendwa na kwamba yupo anayemjali, kwa hiyo asipokuwa karibu yake, atamsumbua kwa maswali,
“Upo wapi? Unafanya nini? Na nani?”

Asije kukudanganya mtu kuwa hapendi kuonewa wivu. Mara kwa mara huwa nalazimika kutoa neno hili kwa sababu kumekuwa na tabia ya watu kuongopeana kuwa hawapendi usumbufu. Wengine wanajaza hekima dhaifu za mapokeo ya kizamani: “Mimi mpenzi wangu Mzungu, hanibani wala nini!”
Je, ni kweli kuwa Wazungu hawaoni wivu? Huko nyuma nimewahi kuuliza swali hili: Ni kwa nini Chris Brown alimpa kipigo Robyn Rihanna Fenty? Uhusiano wa kimapenzi una nguzo zake, na moja kuu ni jinsi wewe unavyomjali mwenzi wako na kumfanya ajione mwenye thamani.

Hujui kuwa mpenzi ni mali yenye thamani? Kama unatambua hilo ni vizuri kuilinda kwa gharama yoyote. Abiria anahimizwa achunge mzigo wake, iweje wewe usidhamirie kumhifadhi mwandani wako? Akili itulie kichwani kwako, wapo wanaolia kwa kuzidiwa kete na marafiki zao.
Hawajui kuwa walicheza ‘faulo’ ndiyo maana wakajikuta wanawekwa pembeni. Hutaki kumuonesha unamjali kwa kipimo kinachostahili, matokeo yake rafiki yako anachukua nafasi. Hujui kumuuliza kulikoni anapokuwa mnyonge, mwenzako anatimiza hilo.

Mapenzi ni sanaa ambayo inamtaka mtu aishi ndani ya mwenzi wake. Uwe rahisi kujua yaliyomo kwenye fikra zake. Katika ‘malavidavi’ epuka u-sistaduu, u-brazameni wala ugumu. Unahitaji kuwa rahisi kwa mwenzi wako na umfanye ajione hajakamilika bila uwepo wako.

Unaweza kufanya kitu ambacho wewe utakiona ni kidogo lakini kwa mwenzako ukawa umemmaliza kabisa. Fikiria unaamka asubuhi mapema unamuamsha kuwahi kazini. Anakuta umemuandalia kila kitu, mnakwenda kuoga pamoja, mnapata kifungua kinywa mezani halafu mnatengana kwa muda kwa sababu mnawajibika ofisi tofauti.

Si kwa kuangalia jinsia. Fikiria pia wewe ni mwanaume ambaye unafanya kitu kumfurahisha mwenzi wako. Unaamka mapema na kunyoosha nguo za mkeo. Unamuamsha na kukuta kila kitu tayari, anajiona mwepesi. Anakukumbatia na kukushukuru kwa sababu anakuona ni mtu wa kipekee. Wengi wamelemazwa na mfumo dume!
Kufanya hivyo, haina maana ni ‘ubushoke’ kama inavyoweza kutafsiriwa, isipokuwa ni njia ya kumpa sababu ya kukupenda. Atakuona ni mwanaume bora uliyekamilika, na usipokuwa naye ataona kuna upungufu mkubwa. Usisome kama mapitio ya vitu rahisi, ila unatakiwa kutunza kichwani na kuhamishia katika vitendo kile ambacho unakipata hapa.


Asilimia kubwa ya watu waliosalitiwa kimapenzi na marafiki zao, ilisababishwa na watu kutoheshimu hisia za wenzi wao. Kiasili, kuna mambo ambayo mtu anakuwa anahitaji kutoka moyoni afanyiwe na mwenzi wake lakini anakuwa hapati, hivyo kusababisha aone pengine jirani anaweza kumtekelezea.

CHUKUA MFANO HUU
Justin na Jamie wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa miaka mitatu sasa. Tatizo kubwa linalowakabili ni kwamba mara kwa mara huwa wanagombana na kusalitiana. Hata hivyo, wao hawajui.
Justin anasema: “Nampenda sana Jamie lakini kuna mambo huwa hanitekelezei, na zaidi huwa nashangaa hata hanionei wivu.

GLOBAL Je, umempoteza na unataka kumrudisha mikononi mwako?

...dondoo hizi zitakusaidia sana
SAHAU yote kuhusu mwaka uliopita, anza kila kitu upya. Hata fikra zako zinatakiwa kuwa mpya. Ondoa uchafu wote katika ubongo wako hasa ule ambao unakukatisha tamaa ya kila kitu.
Jiambie mwenyewe kwamba unaweza kufanya kila kitu. Rafiki zangu, hapa katika Let’s Talk About Love, tunasisitiza upendo, kuachana ni neno ambalo si mahali pake kabisa.
Hata hivyo, kugombana ni sehemu ya maisha ya binadamu. Yawezekana kabisa ulikuwa na mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote na sasa mmeachana. Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine ilikuwa hasira tu.
Siku zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi yake halisi ya kufanya maamuzi. Hapo ndipo kwenye lengo la mada yetu ya leo. Kwamba kwa msingi huo umegundua kwamba kumbe mpenzi wako uliyeachana naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya, ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala yake mnaweza kukaaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza. Yes! Hilo ndilo ninalotaka kulizungumzia.
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi hilo? Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani? Kama majibu ni ndiyo, mada hii inakuhusu sana. Twende kazi...

JE, NI SAHIHI?
Baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha. Kwamba hakuna mwanaume wala mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa naye tofauti na huyo anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha, hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye ndoa.

UTAFAIDIKA NA NINI?
Utafiti usio rasmi nilioufanya, unaonesha kwamba zipo faida za kurudiana na mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni awe moyoni mwako.
Hebu msikie Julius Kihesupe wa Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam, ambaye alipata kuzungumza nami hivi karibuni akitoa maoni yake kuhusu suala hili: “Si vibaya kurudiana, maana kwanza mnakomaza uhusiano.
“Kumrudia mtu wako wa zamani maana yake ni kwamba umekubaliana na udhaifu wake wote. Unajua anachopenda na anachochukia, hapo lazima mtadumu. Bila kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu, tukiwa na miaka miwili kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila mmoja alikaa kivyake kwa miezi kama sita hivi, nikakutana naye Dar, nikiwa nimeachana naye Mbeya, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi minne mbele yake tukafunga ndoa.”

CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuchunguza ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema hivyo kwa sababu yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua anapopatikana ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika himaya yako.

ANA HISTORIA GANI?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya ‘ushushushu’ wako kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’ sana, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uhairishe zoezi lako.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu kwanza, anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako.
Kubwa zaidi ni kwamba, utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya. Natamani kuendelea kuzungumza nanyi rafiki zangu, lakini nafasi yangu kwa leo imeishia hapa. Vuteni subira, wiki ijayo tutaendelea.

Anakupenda lakini anakutesa, mapenzi yapo wapi?

MU hali gani wapenzi wa kona hii? Nina imani hamjambo, kwa upande wangu namshukuru Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema.
Kama ilivyo ada, tunaendelea na mada mpya baada ya kuona jinsi gani unaweza kuishi ndani ya mapenzi katika mwaka 2012 bila kuumizwa. Leo nataka kujibu swali la watu wengi ambao maelezo yao yanapingana kabla ya kuomba ushauri.
Mtu anasema kuwa ana mpenzi wake ambaye wanapendana sana lakini sasa hivi hamuelewi baada ya kuona upendo umepungua.
Ukiangalia kichwa cha habari hapo juu, kina jibu la moja kwa moja lakini ni vigumu mtu kuelewa kwa vile bado hajifahamu katika mapenzi amesimama upande gani.
Unasema wewe na mpenzi wako mnapendana sana, lakini sasa hivi mpenzi wako humuelewi, ukimpigia simu hapokei kama zamani au akipokea, anakuwa na majibu ya mkato tofauti na mwanzo wa mapenzi yenu.
Hili swali naweza kusema limekuwa fasheni katika mapenzi ya sasa, hasa kwa wapenzi waliokuwa pamoja na baadaye kutengana kwa ajili ya kazi au masomo, kwa hawa lazima baada ya muda tatizo hili hutokea.

Kuna nini?
Wengi sehemu hii huwashinda kwa vile huwa na mapenzi ya mdomoni na machoni. Wapenzi wengi huwa na heshima na uaminifu kama wanawaona wapenzi wao kila siku, mtu huogopa kufanya usaliti kwa kuwa mpenzi wake yupo, lakini huyohuyo huwa hana uaminifu anapokuwa peke yake sehemu ya mbali.
Huwa mwepesi kuanzisha uhusiano mpya kwa kuamini ni wa kupita.
Kwa vile wengi hawana mioyo migumu ya uvumilivu, hujikuta wakizama moja kwa moja na kuwasahau waliowaacha nyumbani. Hapo ndipo ule utata unaosumbua huanza. Utasikia nipo bize au simu kutopokelewa kabisa na kwa wengine huwapa wapenzi wao wapya wapokee.
Kwa vile uliye mbali na mpenzi wako hujui mwenzako kazama kwenye penzi jipya, hapo ndipo huanza kuumia moyoni ukiamini kabisa mpenzi wako anakupenda lakini hujui tatizo.
Kama ungekuwa mfuatiliaji mzuri wa makala zangu, ungejua mtu mwenye mapenzi ya kweli yupo vipi. Mwenye mapenzi ya kweli ni tulizo la mawazo ya mpenzi wake, ni mpole na mwenye huruma na mara zote hujiepusha kuwa sehemu ya maumivu yako.
Hivyo, ukiona mpenzi wako haeleweki, unatakiwa kuanza kuizoea hali ile ili kujiandaa kwa penzi jipya, kwa vile ule mche wa mapenzi ulioupanda ndani ya moyo wa mwenzako umesinyaa.
Usipende kujitesa kwa kujitakia, kama umeona kabisa kuna mabadiliko ndani ya penzi ni wakati wa kuchukua uamuzi mgumu ili kunusuru mateso yasiyo na sababu.
Jiepushe kuishi mapenzi ya mazoea kwa kuamini unapendwa wakati unateswa, hakuna upendo wa mateso hata siku moja. Mapenzi ni furaha na wala si karaha. Acha kuusemea moyo wa mwenzako kuwa anakupenda wakati ndiye chanzo cha ugonjwa wako wa moyo.
Kabla ya kuchukua uamuzi mgumu wa kuvunja penzi, msomee mpenzi wako mashtaka na kumueleza ukweli kuwa umechoka kuumia, akikosa utetezi unaoeleweka, una nafasi ya kuvunja penzi.
Kama atakuwa tayari kukiri makosa na kujirudi, unaweza kumpa nafasi nyingine lakini akirudia makosa, achana naye, fungua ukurasa mpya.

GLOBAL Sindano 11 zitakazotibu tabia yako ya wivu

WIVU ni chachandu, vilevile ni kionjo cha mapenzi. Wakati mwingine ni sumu ya uhusiano, hali kadhalika hutokea kuwa kikwazo cha penzi endelevu. Ni vizuri kulitambua hilo ili ujue jinsi ya kuishi kwa kuendana na mazingira yanayofaa.
Mtu mwenye mafanikio kwenye mapenzi ni yule anayeamini katika saikolojia ya kujitambua. Hapa nikupe msisitizo kuwa ni lazima ujitambue ili uweze kuwa bora kwenye mapenzi. Kama hujitambui, maana yake hutajua ulitendalo.
Ikiwa utashindwa kujua ulitendalo, wewe utageuka kuwa kero kwa mwenzi wako. Ukifikia hatua hiyo, unadhani ni nani anaweza kukuelewa? Ni vema ujijue, ujifahamu kasoro na uimara wako katika uhusiano wako. Kama unamfurahisha au kumchukiza, yote yanafaa kugota ndani ya kichwa chako.
Je, una wivu? Hilo unapaswa kulitambua kwa sababu lipo ndani yako. Bahati mbaya ni kwamba watu wanakuwa na wivu wa kupitiliza lakini wakiambiwa wanakuwa wakali. Wanadai wanasingiziwa. Ni vizuri ukatambua upungufu ulionao kabla ya kuelezwa na mtu wa pili.
Wivu wako umekugharimu mara ngapi? Makala haya yanatosha kuwa tiba yako ya kudumu. Pengine hujawahi kukaa, ukatafakari na kugundua kuwa wivu wako unakupeleka njia isiyo sahihi kimapenzi, hapa chini kuna mambo 11 ambayo ni muongozo madhubuti.
11. JIFUNZE KWA WATU WENGINE
Mara nyingine ni rahisi kugundua kuwa unafanya makosa baada ya kuwaona wengine na kujifunza kutoka kwao. Hivyo basi, jaribu kuwaangalia watu wengine walio kwenye uhusiano. Fuatilia mtindo wao wa maisha, mafanikio yao kisha ujitazame wewe.
Bila shaka hapo ulipo, utakuwa umeshawahi kujionea wanaume na wanawake wenye wivu, jinsi wanavyotenda mambo yao, wanavyoudhi na kuchukiza kwenye uhusiano. Kama ndivyo, basi hilo ni somo kwako kwa kuepuka yale yaliyowafanya wachukize.
Inawezekana ukawa umeona kupitia kwa macho yako au umesimuliwa. Muhimu kutambua ni kwamba hulka za wivu, hususan unapozionesha mbele za watu wa pembeni ni mbaya. Kwa mantiki hiyo, kama utaweza kutambua na kuelewa alama za wivu, sina shaka kuwa utakuwa unaweza kujua jinsi ya kuishi katika mazingira salama.

10. MPE NAFASI
Kumbana mwenzi wako haina maana ndiyo utamfanya adumishe uaminifu kati yenu. Jifanye kama mtu usiyejali, muache atoke na marafiki zake. Inaweza kuwa tatizo endapo ataona unamnyima uhuru anaoutaka. Anahitaji nafasi ya kufurahi na marafiki zake, unambana kwa nini?
Akilini kwako lazima ukubali kwamba mwenzi wako ni mtu mzima na anajitambua, kwa hiyo uhuru utakaompa, utawezesha yeye kujiamini zaidi na kuheshimu uaminifu wako kwake. Kisaikolojia, mwenzi wako akigundua unamuamini, naye huzidisha upendo.
Vizuri pia kutambua kuwa wivu hukua zaidi pale mmoja anapokuwa na hisia kwamba mwenzi wake anasaliti. Kama upo kwenye uhusiano wenye afya, huhitaji kusumbuliwa na mawazo mabaya. Endapo utashindwa kuondoa wingu la shaka ndani yako, kaa ukijua kuwa unajiharibia.

9. ONGEZA UAMINIFU
Mojawapo ya dawa nzuri ya kukabiliana na wivu ni kuongeza kiwango cha uaminifu. Muamini mwenzi wako na utaona jinsi mambo yatakavyokwenda. Tunza akilini kwamba kutengeneza uhusiano imara na wenye mafanikio, huhitaji kiwango kikubwa cha uaminifu.
Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.

GLOBAL SUMA LEE, AT, MASHAUZI CLASSIC , MASHUJAA, EXTRA BONGO WAKAMUA DAR LIVE USIKU WA KUAMKIA LEO

Ally Tall ‘AT’ akiwa amekaa chini baada ya raha kumkolea wakati wa makamuzi.

...Akikamua na mmoja wa wanenguaji wake.

Msanii anayetamba na ‘Hakunaga’, Ismaili Thabit ‘Suma Lee’, akiwajibika.

...Suma Lee akiserebuka na mkali wa miondoko ya kwaito.

Mkurugenzi wa kundi la Mashauzi Classic Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’, akiwajibika.

...Akijinafasi jukwaani.

Extra Bongo chini ya Ally Choki (wa pili kushoto), wakiwajibika.

Wanenguaji wa Extra Bongo wakifanya kazi jukwaani.

Nyota wa bendi ya Mashujaa, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’ akikamua na wanenguaji wake.

Wasanii wa kundi la Sliders wakionyesha uwezo wao.

Baadhi ya watoto walioingia ukumbini wakicheza na sungura-mtu.

Wakali Dancers wakipagawawisha.

Ali Choki (kulia), akiteta jambo na Chaz Baba.

Ofisa Utawala wa Global Publishers Ltd, Soud Kivea (wa pili kulia), akikabidhi jezi na mpira vyenye thamani ya sh. 380,000 kutoka Dar Live kwa meneja wa timu ya Vita FC ya Mbagala Zakhem, Ernest Nyanda (wa kwanza kushoto), akishuhudiwa na baadhi ya viongozi wa timu hiyo na viongozi wa Dar Live.

Mmoja wa watoto waliofika ukumbini hapo akiwa kwenye pozi baada ya kuchora usoni kwake.

Watoto wakicheza na Bodaboda zilizomo ukumbini hapo.

…..Wakichorwa mapambo usoni.

…..Wakilishwa keki na kipande cha nyama wakati wa kutoka ukumbini humu ikiwa ishara ya upendo wa uongozi wa ukumbi huo.

Baadhi ya mashabiki wakishuhudia shoo zilizokuwa ukumbi hapo.

Umati uliyofurika ukumbini hapo.

WASANII wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Ismaili Thabit ‘Suma Lee’, Ally Tall ‘AT’, Mashauzi Classic, Extra Bongo ‘Next Level, na Bendi ya Mashujaa usiku wa kuamkia leo walipata nafasi ya kufanya makamuzi ndani ya ukumbi wa kisasa wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam.
Wasanii hao waliwapagawisha mashabiki wa pande hizo na wakausifia Dar Live wakisema kuwepo kwake kulikuwa mwanzo wa wao kufanya shoo za kimataifa huko Mbagala.
Miongoni mwa wasanii hao waliotumbuiza hapo kwa mara ya kwanza tangu ufunguliwe Januari Mosi mwaka huu, waliahidi kupiga shoo zaidi pindi wanapoalikwa.
Shoo hiyo pia ilisindikizwa na kundi la wanenguaji la Sliders kutoka Kinondoni jijini Dar na Wakali Dancers la Temeke ambao pia walifanya makamuzi ya kufa mtu na kusifia mandhari ya ukumbi huo.

MMAREKANI AKWAMISHA MSUMARI KWENYE UBONGO WAKE BILA KUJUA

Msumari ukiwa katika ubongo wa Autullo kama ulivyoonyeshwa na mashine ya X-ray.

Dante Autullo anaelezea jinsi msumari ulivyopenya kwenye ubongo wake.

Mchumba wa Autullo aitwaye Gail Glaenzer akifurahia mafanikio ya tiba ya mpenzi wake. PICHA ZOTE NA SHIRIKA LA AP

MWANAMME mmoja wa Marekani, Dante Autullo, aliandikwa sana na vyombo vya habari hivi karibuni nchini humo baada ya kujidunga msumari wa sentimita tisa kwa bunduki ya kuchomeka misumari ambapo chuma hicho kilikaa katika ubongo wake kwa karibu siku mbili na yeye akiwa hajagundua hali hiyo.

Autullo, anayeishi Orland Park, Illinois, ambaye baadaye alionyesha picha zake za X-ray katika mtandao wa Facebook, alikwenda hospitali yakiwa yamepita masaa 36 baada ya kujipiga na msumari huo.

Hata hivyo, hakugundua madhara ya hali hiyo kwani msumari huo ulikuwa umeacha mkwaruzo mdogo tu wakati ulipoingia kwenye ubongo wake – jambo ambao lilimfanya afikiri kwamba msumari ulikuwa umemkosa.

Autullo alilazimika kwenda kutibiwa baada ya kulalamika alikuwa anasikia kichefuchefu na kuumwa kichwa.

Madaktari walimshangaa kwa kuendelea kutembea na kuzungumza bila wasiwasi na baadaye walimwambia kwamba msumari huo ulikuwa umepita milimita kadhaa pembeni mwa sehemu muhimu ya ubongo wake.

Hata hivyo, jamaa huyo alipewa tiba iliyofanikiwa katika hospitali ya Christ Medical Center, hukohuko Illinois, ambako msumari huo ulitolewa na akawekewa kisahani cha madini ya ‘titanium’ kwenye fuvu lake ambako msumari huo ulipenya.

MASTAA WA FILAMU WATUZWA, WAJIMWAYA KWA MUZIKI MAISHA CLUB

Mnenguaji wa Offside Trick akifanya vitu vyake.
Mastaa waliotunukiwa tuzo wakiwa pamoja.

Wanenguaji wakinogesha hafla hiyo.
Mambo bambam!

Vijana wa Offside Trick wakikamua na mnenguaji wao.

Mashabiki wakicheza mduara.
AT akiwa mzigoni.
MASTAA wa filamu nchini ambao walitunukiwa tuzo za heshima na kampuni ya Pilipili Entertainment jana walijimwaya katika burudani kali iliyosindikizwa na muziki wa Offside Trick na mwanamuziki AT kutoka Zanzibar.

Hafla hiyo iliyofahamika kama Mini-ZIFF (Zanzibar International Film Festival) ilifanyika katika ukumbi wa New Maisha Club ambapo iliendelea hadi usiku wa kuamkia leo.

GLOBAL Sindano 11 zitakazotibu tabia yako ya wivu - 2

KATIKA kipengele “Ongeza Uaminifu” ambacho nilimaliza nacho wiki iliyopita, nilieleza kwamba mojawapo ya dawa nzuri ya kukabiliana na wivu ni kuongeza kiwango cha uaminifu.
Muamini mwenzi wako na utaona jinsi mambo yatakavyokwenda. Tunza akilini kwamba kutengeneza uhusiano imara na wenye mafanikio, huhitaji kiwango kikubwa cha uaminifu.
Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.
Kwa kawaida, anaweza kuwepo mtu ambaye atakufanya usimuamini mwenzi wako hata kidogo. Inawezekana akakujengea picha kutokana na maneno ya zamani au matukio yaliyopita. Je, unaona wivu kwa sababu umeambiwa mpenzi wako aliwahi kutoka na watu wawili tofauti kabla yako?
Wivu wa nini? Kwa nini maneno hayo yakuchanganye akili? Je, ulimkuta akiwa mbumbumbu wa mapenzi na hajawahi kutoka na yeyote? Kumbe utabaini kuwa historia ya mwenzi wako haina maana inayokubalika kwenye uhusiano endelevu.
Wanasema shetani wa jana, leo anaweza kuwa malaika. Vilevile malaika wa leo kesho anaweza kuwa shetani. Inawezekana hao ulioambiwa alitoka nao walimtenda ndiyo maana hakuwapa nafasi ya kudumu lakini wewe umepata fursa hiyo kwa sababu unakidhi mahitaji yake. Hata hivyo, hii haina maana kuwa kila wivu unaotokana na kuambiwa hauna maana. Yapo mengi yenye maana.

8. MWONESHE MWENZI WAKO
Ukiwa na mwenzi wako, muoneshe kwa mifano halisi jinsi unavyojisikia au unavyoweza kumtendea katika nyakati ambazo unamuonea wivu. Kufanya hivyo, ni rahisi kwako kutambua maumivu yako, vilevile na yeye atajua mahali ambako anakosa mengi matamu.
Mtu anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu. Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinaga ubaga kile unachomaanisha. Je, umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua kuwa anakohofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya kumuonea wivu.
Fikiria kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofu unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu wako? Fungua moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe nikupe.
Hata hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau, hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.

7. JIAMINI
Wivu mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha kwa sababu umepungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.

Wema, Kanumba wazua gumzo

Musa Mateja
PICHA mpya za pamoja walizopiga Wema Isaac Sepetu na Steven Charles Kanumba, zimezua gumzo jipya na watu wanahoji imekuwaje tena wakati ‘wanasemaga’ hawana ukaribu wowote?
Wema ‘alibipu’ na picha hizo kwenye mtandao wa BlackBerry Messenger (BBM) juzikati ili kuona kama watu watasemaje ambapo ndani ya dakika chache, alikuwa ameshambuliwa vibaya kwa maoni kibao.
Katika tukio hilo lililojiri Januari 17, mwaka huu, Wema alilazimika kuiondoa picha hiyo mara moja kwani watu walikuwa wakitaka kujua ukaribu huo ulitokana na mazingira gani.
“Umbeya mwingine bana! Watu wameshaanza kutumiana meseji kwamba baada ya kutibuana na Diamond (Naseeb Abdul), sasa Wema karudi kwa Kanumba,” ilisomeka sehemu ya maoni hayo.
Hata hivyo, Ijumaa Wikienda lilipozungumza uso kwa uso na Wema juu ya ishu hiyo, alisema kuwa alikutana na Kanumba kwenye mahojiano katika Runinga ya EATV, ndipo ‘wakafotoana’ picha hizo.
“Sipendi bifu na mwanaume niliyeachana naye, nikimwagana na mtu, haina maana kwamba hatuwezi ‘kushea’, picha tulipiga watu wengi na wala hazimaanishi nimerudiana na Kanumba,” alisema Wema aliyewahi kuwa mpenzi wa staa huyo wa muvi za Kibongo.

Siri nzito bifu la Johari, Nora

Nuru Nassor Masoud ‘Nora’.

Blandina William Chagula ‘Johari’.

Brighton Masalu na Erick Evarist
KUFUATIA tangazo lake la kurejea katika ulingo wa filamu Bongo, msanii Nuru Nassor Masoud ‘Nora’, ametonesha kidonda cha bifu lake la kitambo na muigizaji mwenzake, Blandina William Chagula ‘Johari’ akieleza kuwa nyuma yake kulikuwa na siri nzito.
Akizungumza ishu hiyo alipopewa nafasi na Ijumaa Wikienda mwishoni mwa wiki iliyopita, Nora alifunguka kuwa kisa cha yeye kutofautiana na Johari kilikuwa ni mwanaume.
Alipotakiwa kumwanika mwanaume huyo, Nora alishikilia msimamo wake kuwa hayupo tayari mtu huyo aandikwe gazetini. Akaongeza kuwa wakati akiwa na uhusiano na mwanaume huyo, akageuziwa kibao kwamba alikuwa ni mali ya Johari.
“Sikuwa na mpango na huyo mwanaume lakini Johari alidhani namchukua hivyo nikaundiwa kundi la kunifanyia kitu mbaya,” alisema Nora.
Johari alipotafutwa kwa njia ya simu ili kusema anachokijua juu ya bifu hilo, alisema yuko mbali na Jiji la Dar es Salaam hivyo atalizungumzia suala hilo kiundani atakaporejea.
Hivi karibuni, wawili hao walikutana kwenye msiba wa mwigizaji mkongwe, marehemu Fundi Said ‘Mzee Kipara’ ambapo walilizika rasmi bifu hilo kwa kuwa hakuna aliyefanikiwa kuolewa na mwanaume huyo katika vita hiyo.

LULU SKENDO NO 1 2012

Na Shakoor Jongo
ELIZABETH Michael ‘Lulu’ amesahau waraka alioandika Mwaka Mpya 2012 kuwa amejirekebisha na hataki tena skendo kwani kabla ya mwezi Januari kumalizika, tayari amekwaa skendo namba moja ya kujihusisha na vitendo vya kisagaji.
Picha ya Lulu anayefanya poa kwenye filamu za Kibongo imenaswa mtandaoni akilishana keki kwa staili ya ‘kudendeka’ na msanii anayeuza nyago kwenye video za wanamuziki wa Bongo Fleva, Halima Mohamed ‘Baby Candy’.
Picha hiyo ilionesha ilipigwa ndani Club Bilicanas, Dar es Salaam, Jumapili ya Januari 15, mwaka huu.
Tukio hilo limesababisha mjadala mzito kwa watu walioiona picha hiyo kwenye mtandao wa BBM kufuatia kuwepo kwa tuhuma zinazoenea kwamba baadhi ya mastaa wa filamu kwa sasa wamejikita zaidi kwenye ‘kamchezo hako’.
“Inawezekana ni mtindo wa kisasa kulishana keki kwa mdomo, lakini hawa wamezidisha hasa katika kipindi hiki ambacho wasanii wengi wanatuhumiwa kujihusisha na usagaji,” ilisomeka sehemu ya maoni ya picha hiyo.
Baada ya kuona mjadala unazidi kushika kasi, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Lulu ili kupata undani wa picha hiyo ambapo hakuonesha kushtushwa na chochote kwa kudai ni jambo la kawaida.
“Ni kweli ilikuwa Bilicanas, siku hiyo shosti wangu Baby Candy alikuwa na sherehe ya kuzaliwa, kwangu mimi hakuna ubaya wowote,” alifunguka Lulu nusunusu kwa kukataa maswali zaidi.

Friday, January 20, 2012

MSANII ANASWA KWA UKAHABA

Na Richard Bukos
MREMBO mwenye mvuto wa kimahaba, Evonia William, juzi Jumatano alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Dar es Salaam kwa kosa la kufanya biashara haramu ya ukahaba.
Awali, mrembo huyo aliwahi kutupa karata yake kwenye ulingo wa filamu za Kibongo kwa kushiriki sinema tatu (scene chache) lakini ‘akalamba galasha’.


KUTOKA MAHAKAMANI
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Richard Magodi alimsomea Evonia shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi, William Mutaki na kumwambia kuwa kosa alilokutwa nalo ni la kukaa eneo la wazi na kufanya ukahaba.
Mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa, Januari 17, mwaka huu, saa 2:00 usiku, mshitakiwa huyo alinaswa eneo la Buguruni karibu na Baa ya Kimboka akifanya kosa hilo.

AKANA SHITAKA
Evonia alikana shitaka hilo na kumwambia hakimu kuwa alikamatwa eneo hilo kwa kosa la kupigana na changudoa aliyekuwa akijiuza, lakini yeye hakuwa na lengo la kufanya biashara hiyo.
Baada ya mrembo huyo kukana shitaka, mheshimiwa hakimu alimwambia kuwa, dhamana ipo wazi, lakini alikosa mdhamini hivyo alipelekwa rumande.

AMWANGUSHIA LAWAMA BABA YAKE
Mshitakiwa huyo akiwa mahakamani hapo, alimlalamikia baba yake mzazi aliyemtaja kwa jina la William Molo, kuwa ndiye chanzo cha yeye kuteseka na kuzurura hovyo.
Alisema, baba yake pamoja na uwezo wake mkubwa kifedha, alikataa kumsomesha, ndiyo sababu anahangaika mitaani.


“Kama baba yangu angenisomesha, nisingekuwa hivi. Ningekuwa na maisha mazuri kama mabinti wengine. Nimembembeleza sana anisomeshe lakini hataki. Akitokea msamaria yeyote kunisomesha au hata kufanya kazi za ndani, nipo tayari kutulia,” alisema msichana huyo huku akiangua kilio.
Kesi hiyo itatajwa tena Januari 31, mwaka huu mahakamani hapo huku Evonia akiendelea kula msoto rumande.

New