Tunaendelea na sehemu ya tatu ya mada yetu tuliyoianza wiki mbili zilizopita juu ya namna ya kubadili fikra chakavu kuhusu mapenzi.
Kwa kawaida, mtu ambaye ni mjanja wa mapenzi anabaki kuwa namba moja katika kuhakikisha hapitwi na wakati. Ikiwa hujali hisia za mwenzi wako, wewe utaonekana walewale. Badilika leo na uzichange karata zako vizuri, mwenzi wako anakuhitaji, anataka ukweli wako, kujali kwako, huruma yako na anapenda sifa zake njema zitamkwe na kinywa chako.
Mwanasaikolojia Born Lewis wa Marekani katika makala yake “Your Sentimental and True Love” anasema:
“Inakuhitaji uwe mwelewa zaidi wa hisia za mwenzako ili uweze kudumu. Mfano; Msome na ujue kwamba anahitaji kusifiwa halafu umsifie. Akienda kupewa sifa na mtu wa pembeni atajua humkubali. Hilo ni kosa kubwa katika mapenzi.”
Lewis anafafanua: “Ni kosa kubwa kwenda kumpongeza mfanyakazi mwenzako kwa muonekano wake, wakati hujafanya hivyo kwa mpenzi wako nyumbani. Ukitaka kujua kwamba inauma, fikiria mwenzio amekuona ulivyovaa na hakukwambia kitu lakini unapata taarifa kuwa amemsifia jirani yenu. Itakuuma, itakupunguza imani yako kwa mwenzi wako.”
Sherry na Mosses ni wapenzi lakini hata siku moja Sherry hajawahi kuonesha kwamba anamkubali Mosses ingawa penzi lao linazidi kuvuta miaka. Ilivyo ni kwamba mara nyingi ni Mosses ndiye huonesha hisia zake kwa Sherry na hata marafiki zao hufikia kusema kwamba jamaa ndiye anayesababisha uhusiano wao uendelee kuwepo, vinginevyo wangekuwa wamekwishapigana mwereka.
Sherry anapoambiwa amependeza anajibu ‘asante’ halafu imetoka. Akiambiwa yeye ni mwanamke mzuri jibu ni ‘thank you’. Hathubutu kumwambia Mosses kuwa amependeza au ni mwanaume anayemvutia kuliko wote, ila akiwa kazini kwake, pongezi huzimwaga huko. “James umependeza!” Sherry anamwambia mfanyakazi mwenzake.
Wakati mwingine Sherry anakosa hekima, anamueleza Mosses: “Unajua sisi pale kazini kwetu kuna vijana wazuri. Unajua Jamal ana sura nzuri sana? Halafu Sam anajua kupigilia mavazi ukimuona hadi raha.”
Inawezekana Sherry anazungumza kweli lakini kichwani kwake kuna kelele za ndani (internal noise) zinazomsababishia umapepe, hivyo kukosa busara ya kuchagua maneno mbele ya mpenzi wake.
Ukitaka kujua mkuki kwa nguruwe, siku moja Sherry alikutana na Zawadi ambaye ni mfanyakazi mwenzake Mosses. Zawadi akaamua kuwa mkweli: “Mosses nimemuacha ofisini ila kanifurahisha, amenisifia huyo. Anasema nimependeza sana leo.” Ilikuwa ni kama Zawadi kamroga Mosses kwani Sherry alikasirika mno siku hiyo.
Walipokutana nyumbani, Sherry alitaka maelezo ni kwa nini alimsifia Zawadi kwamba amependeza badala ya sifa hizo kuzielekeza kwake. Mosses akaona mpenzi wake anampanda kichwani, akamjibu: “Mbona wewe huwa unawasifia wanaume wa kazini kwako mimi sisemi, tena mbele yangu.” Sherry ikamgonga kichwani, akapata pointi!
Sherry hakujua kwamba sifa alizokuwa anazimwaga kwa wanaume wa kazini kwake ilikuwa sawa na kuchezea hisia za Mosses. Haikumgonga kichwani kwamba anamuumiza mwenzake. Alipokutana na Zawadi ikawa maumivu kwake. Kila mtu anatakiwa kujali, kusifu kwa sababu hivyo ni vionjo muhimu kwenye mapenzi.
Kama hukubali kwa jinsi mwenzi wako alivyo ni bora kuachana naye kuliko kupotezeana muda. Tambua kuwa usipomsifu wewe anapokwenda atasifiwa halafu ukisikia itakuuma. Wewe humuelezi kama ni mzuri, anapokwenda wapo watakaomuona watamwambia anavutia, je, hapo huoni kama utakuwa umepoteza kura kwa mwenzi wako?
No comments:
Post a Comment