...dondoo hizi zitakusaidia sana
SAHAU yote kuhusu mwaka uliopita, anza kila kitu upya. Hata fikra zako zinatakiwa kuwa mpya. Ondoa uchafu wote katika ubongo wako hasa ule ambao unakukatisha tamaa ya kila kitu.
Jiambie mwenyewe kwamba unaweza kufanya kila kitu. Rafiki zangu, hapa katika Let’s Talk About Love, tunasisitiza upendo, kuachana ni neno ambalo si mahali pake kabisa.
Hata hivyo, kugombana ni sehemu ya maisha ya binadamu. Yawezekana kabisa ulikuwa na mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote na sasa mmeachana. Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine ilikuwa hasira tu.
Siku zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi yake halisi ya kufanya maamuzi. Hapo ndipo kwenye lengo la mada yetu ya leo. Kwamba kwa msingi huo umegundua kwamba kumbe mpenzi wako uliyeachana naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya, ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala yake mnaweza kukaaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza. Yes! Hilo ndilo ninalotaka kulizungumzia.
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi hilo? Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani? Kama majibu ni ndiyo, mada hii inakuhusu sana. Twende kazi...
JE, NI SAHIHI?
Baadhi ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha. Kwamba hakuna mwanaume wala mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa naye tofauti na huyo anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo, kikubwa cha kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha, hivyo kukupa urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda jambo litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye ndoa.
UTAFAIDIKA NA NINI?
Utafiti usio rasmi nilioufanya, unaonesha kwamba zipo faida za kurudiana na mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni awe moyoni mwako.
Hebu msikie Julius Kihesupe wa Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam, ambaye alipata kuzungumza nami hivi karibuni akitoa maoni yake kuhusu suala hili: “Si vibaya kurudiana, maana kwanza mnakomaza uhusiano.
“Kumrudia mtu wako wa zamani maana yake ni kwamba umekubaliana na udhaifu wake wote. Unajua anachopenda na anachochukia, hapo lazima mtadumu. Bila kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu, tukiwa na miaka miwili kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila mmoja alikaa kivyake kwa miezi kama sita hivi, nikakutana naye Dar, nikiwa nimeachana naye Mbeya, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi minne mbele yake tukafunga ndoa.”
CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuchunguza ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema hivyo kwa sababu yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua anapopatikana ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika himaya yako.
ANA HISTORIA GANI?
Lazima ujue kuhusu historia yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya ‘ushushushu’ wako kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’ sana, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na tamaa za kimwili na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano, itakubidi uhairishe zoezi lako.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu kwanza, anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako.
Kubwa zaidi ni kwamba, utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya. Natamani kuendelea kuzungumza nanyi rafiki zangu, lakini nafasi yangu kwa leo imeishia hapa. Vuteni subira, wiki ijayo tutaendelea.
No comments:
Post a Comment