Rais wa Marekani, Barack Obama anatua nchini kwa ziara ya siku mbili ikiwa ni hatua yake ya mwisho ya ziara yake barani Afrika.
Dar es Salaam.
Yametimia! Baada ya siku kadhaa za kusubiri kwa hamu, vitabu vya
historia ya Tanzania vinaongezewa kumbukumbu wakati Rais wa Marekani,
Barack Obama atakapowasili nchini leo mchana kwa ziara ya siku mbili.
Ndege ya Air Force One itakayombeba Obama na msafara wake itakanyaga
ardhi ya Tanzania saa 8.40 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere ambako atapokelewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya
Kikwete.
Obama ambaye anafuatana na mkewe
Michelle na binti zake, Malia na Sasha, anatua Tanzania ikiwa ni sehemu
yake ya mwisho ya ziara yake barani Afrika.
Anawasili Tanzania akitokea Afrika Kusini ambako alikwenda Ijumaa baada ya ziara yake ya Senegal.
Historia imetimia
Imepita miaka 50, tangu Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere alipotembelea Marekani, Julai 13, 1963 na
kukutana rais wa nchi hiyo wakati huo, John F Kennedy na ziara hiyo
inaaminika kuanzisha urafiki wa viongozi hao ambao umedumu hadi sasa.
Ujio wa Rais Obama una maana na faida
kubwa kwa Tanzania katika maeneo ukiangalia kihistoria, kisiasa,
kidiplomasia na kiuchumi pia.
Ziara ya Obama ni heshima kubwa kwa
Tanzania na itaingia katika vitabu vya kihistoria kwani ana rekodi ya
kuwa mtu mweusi wa kwanza kuchaguliwa kuongoza taifa la Marekani.
Kuchaguliwa kwake (Obama), ambaye baba yake mzazi alikuwa na asili ya
Kenya kuliashiria nuru mpya kwa siasa za Marekani kwani watu weusi wa
taifa hilo kwa miaka mingi walikuwa wakipigania haki za kufaidika na
fursa za kiuchumi na kisiasa katika taifa la Marekani.
Tanzania, kwa miaka mingi ilikuwa inaunga mkono harakati za watu weusi na ndiyo
iliikuwa karibu na viongozi wa harakati za kupigania haki za watu weusi.
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa karibu na
Martin Luther King na mkewe Correta , ambao waliongoza harakati za mtu
mweusi kujikomboa.Pia, viongozi wengine wa harakati hizo za mtu mweusi
kutambuliwa kule Marekani, Jesse Jackson, Andrew Young na Malcolm X
waliitembelea Tanzania mara nyingi. Obama alipochaguliwa kushika
nafasi hiyo mwaka 2008 alifurahiwa na wapenda amani kote duniani na hasa
Waafrika kwani walimhesabu kuwa ni sehemu yao.
Kuja kwake leo ni heshima kubwa kwani
Tanzania inakuwa nchi ya nne Afrika kutembelewa na Obama baada ya Ghana
mwaka 2009 na ziara yake ya hivi karibuni ya nchi za Senegal na Afrika
Kusini.
Ukizingatia kuwa Obama ana miaka
mitatu na nusu kabla ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi wake
huenda ziara hii ndiyo ikawa ya mwisho kwake barani Afrika akiwa na
wadhifa wa rais.
No comments:
Post a Comment