Askari wa Kikosi cha zimamoto na Uokoaji wakizima moto uliokuwa unawaka
katika mitambo ya kuzalisha umeme ya songas, Ubungo jijini Dar es Salaam
jana. (Picha na Francis Dande)
DAR ES SALAAM, Tanzania
Mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas iliyopo Ubungo jijini dar es
Salaam, usiku wa kuamkia leo imeungua moto kabla ya kudhibitiwa na
Kikosi cha Uokoaji na Zimamoto kwa kushirikiana na kikosi cha Kampuni ya
Knight Support.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme
nchini (Tanesco), Mhandisi Felichesim Mramba, alisema hitilafu hiyo
imetokea katika kituo cha 33kv na kusababisha gridi ya taifa inayotumika
jijini Dar es Salaam kuzimika, hivyo baadhi ya maeneo umeme ukawa
umekatika.
“Tulipata taarifa saa 10 kuwa kuna hitilafu hapa na tukajaribu
kuwasiliana na Idara ya Zimamoto kwa simu wakawa hawapatikani mpaka
tulipowafuata ofisini kwao. Nashukuru baada ya taarifa walifika kwa
wakati na wakafanikiwa kuudhibiti moto,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na hitilafu hiyo maeneo mbalimbali ya jiji
yaliyokuwa yakipata umeme kupitia kituo hicho yataathirika na kuyataja
kuwa ni Kigogo, Mburahati, Magomeni, Tandale na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Meneneo mengine ni Changanyikeni, Kimara, Tabata na Riverside na kwamba
juhudi zinafanyika kuangalia uwezekano wa maeneo hayo kuunganishwa
katika njia nyingine kwa muda.
Aliongeza kuwa bado hawajajua thamani halisi ya hasara iliyopatikana na
muda utakaotumika kufanya marekebisho huku akiainisha kuwa ukarabati wa
vifaa hivyo unaweza kuchukua wiki moja mpaka mbili kutegemea na aina ya
uharibifu.
Baadhi ya mashuhuda waliliambia gazeti hili kuwa moshi uliokuwa ukitoka
katika mitambo hiyo ulikuwa mzito na uliwasababishia kushindwa kupumua
vizuri.
“Niliwaona kina mama na watoto waliokuwa wanakwenda katika kituo cha
mabasi Ubungo wakipata taabu kupumua hadi tukawa tunawasaidia kuwapeleka
mbali na eneo la tukio,” alisema Gervas Lutabalize, ofisa wa Chama cha
kutetea abiria.
Kamanda wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji jijini Dar e s Salaam, ACP
Jesward Ikonko, alisema walipata taarifa ya tukio saa 11:58 alfajiri na
kufika katika tukio saa 12:5 ambapo waliwakuta wafanyakazi wa kikosi cha
Knight Support wakiwa wameshaanza kazi ya kuzima moto.
No comments:
Post a Comment