Katika taarifa kwa vyombo vya habari saa chache zilizopita, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amesema kuwa amesikitishwa kwa namna rais Nkurunziza ameiponda katiba ya nchi na kupuuza mkataba waliosaini mjini Arusha miaka kumi na tano iliyopita.
Amesema kuwa rais huyo ametumia mbinu ghushi kung'ang'ania madarakani katika uchaguzi ambao sio huru wala wa haki.
Kerry amesisitiza kuwa ni lazima pande zote husika nchini humo zirudi katika majadiliano ya dhati na kuhusisha pia mashirika ya kijamii.
Amesema kuwa hii ndio njia ya pekee ya kurejesha imani sio tu ya raia wa Burundi bali jamii ya kimataifa pia, na kuzuia ghasia zaidi nchini humo zilizosababisha watu kuikimbia nchi.
Hapo jana tume huru ya uchaguzi nchini Burundi ilitangaza kuwa rais Nkurunziza amepata asilimia karibu sabini ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumanne wiki hii.
Kura katika majimbo zinatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Viongozi wakuu wa upande wa upinzani nchini Burundi walisusia uchaguzi huo,lakini majina yao yalisalia katika karatasi za kupigia kura.
Kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa alimaliza katika nafasi ya pili akizoa asilimia kumi na tisa ya kura zilizopigwa.