Rais Museveni amemtembelea Rais Magufuli katika Ikulu ndogo ya Arusha leo jioni mara baada ya kuwasili hapa nchini akitokea nchini Uganda, ambapo hapo kesho atahudhuria mkutano mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baada ya wawili hawa kufanya mazungumzo ya faragha, Rais Magufuli amesema wamekubaliana kutekeleza mradi huo wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanga hadi Uganda kwa manufaa ya nchi zote mbili na nchi nyingine za Afrika Mashariki, litakuwa na urefu wa kilometa 1,120 na kwamba mradi huo utazalisha ajira za watu zaidi ya 15,000.
Rais Magufuli ameongeza kuwa pamoja na kujengwa kwa bomba la mafuta, pia wamezungumzia kuongeza biashara ndani ya nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki, kujenga viwanda na kuzalisha ajira zaidi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji mali.
Rais Magufuli amesema katika mkutano huu nchi wanachama watajadili maombi ya nchi ya Sudan Kusini kupata uanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa Sudan Kusini kuwa mwanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na uwezo wa kufanya biashara katika eneo lenye takribani watu milioni 150.
Kwa upande wake Rais Yoweri Museveni pamoja na kuunga mkono yaliyosemwa na Rais Magufuli amempongeza kwa kasi yake nzuri aliyoanza nayo katika uongozi na amesema ni matumaini yake kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa zitakuwa katika nafasi nzuri ya kwenda kwa kasi ya Rais Magufuli katika maendeleo.
No comments:
Post a Comment