Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa akiongea na wanahabari (hawapo pichani).
Dar es Salaam, 12. Des. 2012 …
Mdhamini wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara, Kampuni ya simu ya Vodacom
Tanzania imezishauri klabu zinazokipiga ligi kuu kutumia nafasi ya
usajili wa dirisha ndogo kuimarisha vikosi ili kuongeza kasi ya
ushindani katika mzunguko wa lala salama wa ligi hiyo.Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kampuni hiyo, Vodacom imesema vuilabu vina nafasi ya kutumia fursa ya dirisha dogo la usajili kujihakikishia kufanya vema kuelekea ubingwa wa ligi kuu.
“Msimamo wa ligi sasa unaonyesha dhahiri kuwa hata timu iliyo katika nafasi ya tano ina nafasi ya kuchukua ubingwa ikitambua mapema mapungufu yaliyosababisha usifanye vizuri katika mzunguko wa kwanza kupitia dirisha dogo klabu inaweza kujisahihisha.” Amesema Kelvin Twissa, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania.
“Kabla ya usajili wa dirisha ndogo haujafanyika ni vyema klabu zikafanya tathmini ya aina ya wachezaji wanaohitaji na kufanya usajili wa kisayansi ambao utazijenga timu na kukabiliana na mikiki ya msimu ujao ambao ni mgumu zaidi,” amesema Twissa.
“Tumeshuhudia ushindani wa kiwango cha juu katika mzunguko wa kwanza hili linaweza kuufanya mzunguko wa pili ukawa mgumu zaidi kuusaka ubingwa na kujinusuru kushuka daraja hivyo ni vema kila timu ikajiandaa kimkakati kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi”Aliongeza Twissa
Mkuu huyo wa Masoko amesema kuwa kampuni yake inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuinua michezo na wao kama wadhamini wa ligi kuu ni vyema kushirikiana na timu ili kujenga uwezo na kiwango cha soka nchini.
“Timu zetu zimekuwa gumzo katika michuano ya Chalange kwa kufunga magoli mengi zaidi na kuonyesha kiwango cha hali ya juu. Ni Wachezaji hao hao wanaocheza katika Ligi kuu ya Vodacom pamoja na wale wa ligi kuu Zanzibar ndio wamezua gumzo katika michuano hiyo,” amesema Twissa, na kuongeza kuwa, “Ukitazama hilo kwa kina lazima utawapa makocha wetu wa Tanzania sifa kwani ndio wanao waandaa wachezaji katika ngazi ya vilabu na wanapokuja kucheza katika timu ya taifa wanakuwa na mafanikio makubwa,”
Twissa amehitimisha kwa kuzisihi timu za Simba na Azam kufanya maandalizi ya michuano ya kimataifa inayo wakabili na kuzitakia kila la kheri.
“Tunazitakia kila la kheri timu zitakazoiwakilisha nchi yetu katika michuano ya kimataifa. Tunaamini tutafika mbali kwani ligi yetu inaendelea kuwa bora zaidi,” amesema Twissa.
Klabu ya Simba itachuana na timu ya C.R Libolo ya Angola katika michuano na Klabu bingwa Afrika na Azam FC itachuana na Ali Nasir Juba ya Sudan Kusini katika kombe la Shirikisho.