Pep Guardiola, mwenye umri wa miaka 41, awali ilidhaniwa angelijiunga na Chelsea, au Manchester City, zote za Uingereza.
                           Guardiola ametia saini mkataba wa miaka mitatu na Bayern Munich, hadi mwaka 2016. 
                        
                           Atachukua madaraka ya Jupp Heynckes, ambaye ameamua kustaafu.
                        
                           Siku zake akiwa mchezaji, Guardiola, aliwahi 
kuvichezea vilabu vya Barcelona, Brescia, Roma, Al.-Ahli, Dorados na pia
 timu ya taifa ya Uhispania.
                        
                           Alikabidhiwa pia tuzo nyingi akiwa mchezaji.
                        
                           Katika kazi ya meneja, amewahi kuchukua 
ubingwa wa ligi kuu ya Uhispania, La Liga, mara tatu, ushindi wa 
Supercopa de Espana mara tatu, mara mbili kutwaa ubingwa wa Copa Del 
Rey, ubingwa mara mbili wa klabu bingwa barani Ulaya, mara mbili Kombe 
la Uefa na vile vile mara mbili ubingwa wa Kombe la Dunia la FIFA kwa 
upande wa vilabu.
                        
                           Guardiola, ambaye alizaliwa tarehe 18 
Januari, mwaka 1971, Santpedor, Uhispania, tangu kuondoka uwanja wa Nou 
Camp mwezi Mei mwaka 2012, amepumzika msimu mzima, baada ya kukiwezesha 
klabu kupata jumla ya vikombe 14, ikiwa ni pamoja na ushindi wa klabu 
bingwa barani Ulaya mara mbili. 
                        
                           "Tumefurahi sana tumefanikiwa kumshawishi 
mtaalamu wa soka Pep Guardiola kuja Bayern Munich, ambaye vilabu vingi 
vikuu vilimtamani na kuwasiliana naye," alieleza mkurugenzi mkuu wa 
Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
                        
                           "Yeye ni kati ya makocha waliofanikiwa sana 
duniani, na tuna hakika kwamba sio tu ataiwezesha klabu ya Bayern 
kung’ara, lakini hata soka ya Ujerumani kwa jumla."
                        
                           Bayern kwa hivi sasa inaongoza katika ligi 
kuu ya Ujerumani ya Bundesliga, na itapambana na Arsenal ya Uingereza 
mwezi ujao, ikiwa ni miongoni mwa timu 16 zilizosalia katika michuano ya
 klabu bingwa barani Ulaya. 
                        
                           Heynckes, mwenye umri wa miaka 67, kabla ya 
siku kuu ya Krismasi alikuwa ameifahamisha klabu hiyo inayocheza katika 
ligi kuu ya Bundesliga kwamba hana nia ya kutia saini mkataba mpya baada
 ya msimu huu. 
                        
                           Mkataba wake utakwisha tarehe 30 mwezi wa Juni, na Guardiola atachukua mahala pake siku itakayofuata. 
                        


No comments:
Post a Comment