Mitambo ya Dowans
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Fredrick Werema na Jaji 
Kiongozi, Fakihi Jundu, wamemmwagia sifa kedekede Jaji Emilian Mushi 
kutokana na hukumu ya kesi kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, 
dhidi ya Shirika la Umeme (Tanesco).
Katika hotuba zao za kumuaga Jaji Mushi 
aliyestaafu hivi karibuni, Jaji Werema na Jaji Jundu walirejea hukumu za
 kesi kadhaa alizozitoa Jaji Mushi kama kielelezo cha umakini, ujasiri, 
uadilifu na weledi wake, ikiwamo hukumu hiyo ya Dowans.
Msimamo huo wa Jaji Werema na Jundu umekuja wakati
 Tanesco ikihaha kukata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyosajiri tuzo ya 
Dowans, iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro 
ya Kibiashara (ICC).
AG Werema
Katika hotuba yake ya kumuaga Jaji Mushi, Werema 
alisema kuwa Jaji Mushi katika utendaji wa shughuli zake alikuwa 
akitenda bila kufungamana na upande wowote, pasipo hofu wala upendeleo, 
nia mbaya au kuathiriwa na hali yoyote. Akizungumzia kesi ya Dowans, 
Werema alisema kuwa Jaji Mushi amethibitisha kuwa ni mtafiti, mtu wa 
kutafakari na mchambuzi wa sheria, huku akiifananisha na chuo cha sheria
 za usuluhishi wa migogoro ya kibiashara.
“Wale wanaotamani kuwa wataalamu katika 
usuluhishi, anawashauri kusoma hukumu yake katika shauri la Madai namba 
8/2011 linalohusiana na usuluhishi baina ya Dowans Holdings SA (Costa 
Rica) na Dowans Tanzania Ltd ya Tanzania dhidi ya Tanesco.”, alisema 
Jaji Werema.
Jaji Jundu
Kwa upande wake Jaji Kiongozi, Jundu, akizungumzia
 hukumu ya Dowans alisema kuwa ni mfano wa jinsi Jaji Mushi alivyokuwa 
akisisitiza hukumu zinazozingatia ushahidi na ukweli, na kwamba alikuwa 
mwangalifu, mwadililifu, mweledi, mtenda haki bila upendeleo.
Alisema kuwa katika hukumu hiyo Jaji Mushi 
alizingatia sana ukweli na ushahidi, pamoja na sheria zinazohusiana na 
masuala ya usuluhisi..
Kwa upande wake Jaji Mushi pia aliitaja kesi ya 
Dowans kuwa ni miongoni mwa kesi ambazo hatazisahau katika maisha yake 
ya ujaji kutokana na changamoto mbalimbali alizokabiliwa.
Alisema miongoni mwa changamoto aliyoipata katika 
kesi hiyo ni jinsi ya kuwianisha uamuzi wa ICC na kulinganisha na sheria
 zinazotumika hapa nchini, pamoja na msukumo wa kisiasa katika shauri 
hilo.
Novemba 15, 2010 ICC, chini ya Mwenyekiti Gerald 
Aksen akisaidiwa na wasuluhishi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, 
iliiamuru Tanesco iilipe Dowans fidia ya Sh94 bilioni kwa kuvunja 
mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment