My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, October 24, 2013

JENGA MSINGI IMARA WA BIASHARA YAKO KWA FAIDA ENDELEVU!-2

tulianza kujadili mada ya namna ya kujenga msingi imara katika biashara. Niliyaorodhesha maswali kumi magumu ya kujiuliza kabla hujaamua kuanzisha biashara yako. Naamini umejifunza mengi na sasa tunaendelea na sehemu ya pili ya mada yetu.
Endapo utachukua muda wa kutosha kufanya tathmini ya uwiano wa thamani, utakuwa umefanya jambo la muhimu sana katika safari yako ya mafanikio. Na kama huwezi kuwa na shauku ya kutaka kujua jambo hili kabla ya kuanza, utawezaje basi kuwa na shauku ya kujifunza zaidi kuhusu biashara yako pindi utakapokuwa umeanza?
Wajasiriamali wanaofanikiwa sana maishani ni wale wanaozichukulia biashara zao kama uwanja wa kujifunza zaidi jinsi ya kufanikiwa katika ujasiriamali. Hivi ndivyo ilivyo katika nyanja mbalimbali za maisha.
Mimi nimekuwa mpenzi sana wa mpira wa kikapu (basketball) na kwa miaka mingi sana nimekuwa mfuasi na shabiki wa mchezaji nyota wa kikapu aliyewahi kuwa bora kuliko wengine wote ulimwenguni – Michael Jordan. Ndugu huyu alikuwa akiichezea timu ya Chicago Bulls na aliiongoza kuchukua ubingwa wa ligi ya mpira wa kikapu ya Marekani (NBA) zaidi ya mara 5.
Siku za hivi karibuni, Jordan au Air Jordan kama alivyobatizwa na washabiki wake aliulizwa: “Je, kama hivi leo ungeshindanishwa na mchezaji mwingine yeyote katika historia ya wachezaji wote nyota ulimwenguni waliofariki na waliowahi kuwa katika mpambano wa watu wawili tu uwanjani (one-on-one), je unadhani kuna yeyote ambaye angeweza kukushinda?”
Michael baada ya kufikiria kwa kitambo, alisema: “Sidhani. Hakuna ambaye angeniweza, kuanzia enzi za kina Larry Bird, Jerry West, Gary Payton na miamba wengineo mpaka leo hii akina Lebron James na wengine wa sasa, hakuna ambaye angefua dafu. Isipokuwa kuna mmoja tu ambaye pengine angeniweza, kwa kuwa mchezaji huyu ananiibia michezo yangu (moves) karibu yote. Na huyu si mwingine, bali ni ndugu Kobe Bryant.”
Nilishangazwa sana na majibu haya ya mwamba huyo. Kisha nilipoanza kumchimba na kumfuatilia Kobe Bryant ambaye kwa sasa pengine ndiye mchezaji bora kuliko wote (japo najua hili ni jambo linalobishaniwa sana kwani wengi wanaamini kuwa Le Bron James ndiye mkali kuliko wote), nikagundua kuwa Kobe ni mwanafunzi mzuri wa mchezo wa vikapu! Kwa muda mrefu sasa amekuwa akiwafuatilia kwa karibu sana wachezaji wakubwa wote waliowahi kuitingisha dunia hii katika mpira wa vikapu kwa kuangalia video zao na kuzirudiarudia na kuiga mazuri mengi kadiri awezavyo.
Hii ni pamoja na mikanda mingi ya Michael Jordan. Kwa sababu hiyo basi, ndiyo maana Kobe ameweza kuwa mchezaji bora kuliko wote kwa sasa na anajulikana na kuheshimiwa hata na gwiji wa magwiji wa mpira wa kikapu!
Hivyo msomaji ndivyo unavyopaswa kuichukulia biashara yako. Ujione kama wewe ni mwanafunzi wa hiyo biashara yako kila siku. Unatakiwa uwe mwanafunzi hodari wa hiyo biashara yako na ujifunze kwa bidii siri nyingi kadiri uwezavyo. Ikiwezekana uanze michakato hii kabla hujafungua biashara yako.
Hii itakupa mwangaza na kukuokoa na kushindwa kwa kila aina kwa mamia ya biashara kila mwaka hapa nchini kwetu Tanzania. Hii haijalishi aina ya biashara unayoifanya, iwe ni ya chakula au burudani, mazao au madini, elimu au biashara za ufundi. Kanuni ni zilezile.
Wakati unayafanya yote haya ni muhimu sana kuwa na mtazamo chanya kuliko kuwa na mtazamo hasi. Ukialikwa kwenye harusi kama mpigapicha za video na muda wote ukaamua kuelekeza kamera yako kwenye kona ambayo mtu na mkewe wanagombana na kubishana kwa uchungu tangu mwanzo mpaka mwisho wa harusi unapoondoka, ukiulizwa ile harusi ilikuwaje, bila shaka utasema ilikuwa ni mbaya sana.
Lakini vilevile kama utaelekeza kamera yako sehemu ambayo kuna watu watano wameketi mezani wanacheka, wanataniana na kufurahi sana kuanzia mwanzo hadi mwisho, wakati unaondoka utasema kwamba ile sherehe ilikuwa kama paradiso.
Lakini ukitaka kupata ukweli wa kutosha na halisi zaidi, ni vizuri kama ukizungusha kamera yako sehemu mbalimbali na kuchukua matukio mengi kadiri iwezekanavyo! Hivyo ndivyo ilivyo kwetu sisi wajasiriamali.

No comments:

Post a Comment

New