My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, September 21, 2012

Watanzania mabingwa wa kiswahili

Kwa mpenzi yeyote wa Kiswahili ni sharti azingatie stadi nne za lugha hiyo. Yaani kuzungumza, kusoma kuandika na kuelewa lugha ya Kiswahili. Hata hivyo baadhi ya wakenya wamekuwa wakilamika kuwa vitabu vingi vya Watanazani vimekuwa vikitahiniwa nchini Kenya hususan katika vidato vya tatu na vinne.
Ukweli ni kuwa Watanzania wamewabwaga wakenya na ipo mifano ya kutajika kuhusiana na hilo katika vitabu hususan vya fasihi. Swali ni je Wakenya wamepewa fursa ya kuandika au la? Ni nani anastahili kuwaambia waandike vitabu vya Kiswahili, na je wachapishaji vitabu wako radhi kuzichapisha kazi za Wakenya?
Kuanzia miaka ya themanini hadi sasa, idadi ya vitabu vya Watanzania vilivyotahiniwa katika kunga za riwaya, tamthilia na ushairi ni kubwa kushinda vya Wakenya. Riwaya ya Kusadikika ya Shaaban Robbert(Mtanzania) ilitahiniwa mwanzoni mwa miaka ya tisini hadi mwaka 1994. Wakati huo hadi mwaka 1997 tamthilia ya Mashetani ya Ebarahim N. Hussein(Mtanzania) ilitahiniwa. Mwaka wa 1994 hadi mwaka 1998 riwaya ya Kisima cha Giningi ya Mohamed Said Abdullah(Mtanzania) ilitahiniwa. Katika miaka hiyo kuanzia mwaka 1998 tamthilia ya Amezidi ya Said Ahmed Mohamed (Mpemba) ikaanza kutahiniwa kuchukua mahali ya tamthilia ya Buriani ya A. S Yahya na David Mulwa(Wakenya). Wakati huo Mkenya Khaemba Ongeti alijipenyeza na tamthilia yake ya Visiki.
Hayakuishia hapo, baada ya tamthilia za Visiki na Amezidi kuondolewa katika ratiba ya shule za upili nchii Kenya ikaingia riwaya nyigine ya Mohamed Said Ahmed (Mpemba) ya Kitumbua kimeingia mchanga. Na hiyo ilipoondoka ikaja riwaya ya Utengano ambayo inatahiniwa hadi sasa.
Ukweli unaojitokeza hapa ni kuwa taasisi ya elimu nchini haiviteui vitabu hivyo kwa sababu ni vya Watanzania. Ni kutokana namna vilivyosukwa kimaudhui na kifani. Isitoshe waandishi wa vitabu hivyo wameandika wameandika vitabu vingi tu. Kwa mfano Said Ahmed Mohemed ameandika zaidi ya vitabu 40 vya Kiswahili. Mohamed Said Abdullah ameandika vitabu vingi tu kama vile Kisima cha Giningi, Duniani kuna watu, Mizimu ya watu wa kale na Kadhalika.
Hata hivyo ni vyema kutambua kuwa baadhi ya Wakenya wamejitokeza na kuandika kazi nzuri za fasihi ya Kiswahili kama vile Siku Njema ya Ken Walibora, Mstahiki Meya ya Timothy Arege na Kifo Kisimani ya Kithaka Wamberia. Kwa ufupi wapenzi wa Kiswahili katika kanda ya Afrika Mashariki wakijumuisha mataifa ya Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Somalia na Uganda waandike vitabu zaidi vya Kiswahili. Twasubiri siku watanzania watavitahini vitabu vya Kiswahili vya wakenya, Vivyo hivyo si dhambi kitabu cha Kiswahili kilichoandikwa na Mrundi ama Mnyarwanda kikitahiniwa Uganda na vinginevyo.

Saturday, September 8, 2012

Obama apigiwa debe na Bill Clinton



Rais mstaafu Bill Clinton na Barack Obama

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton amemtetea vikali mgombea urais wa chama cha Democrats nchini Marekani Barack Obama.
Katika hotuba iliyochukua muda wa dakika 50 katika kongamano la chama hicho linalofanyika mjini Charlotte, North Carolina, Clinton alikosoa sera za uchumi za chama pinzani cha Republican.
Bill alisisitiza kuwa sera ya uchumi ya Barack Obama imeweza kuimarisha uchumi wa nchi hiyo ambao ulikuwa umedorora. Bwana Clinton alimaliza hotuba yake kwa kumteua rais Obama kuwa mgombea rasmi wa urais wa chama.
Rais Obama atamenyana na mgombea wa chama cha Republican Mitt Romney katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Novemba.
Hotuba ya Clinton ni dalili ya kuimarika kwa uhusiano kati yake na Obama na pia kama juhudi za kupiga jeki mvuto wa obama miongoni mwa wazungu wanaofanya kazi.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa wapiga kura wa chama hicho wamekuwa waangalifu sana kuhusu sera za Obama lakini Clinton ana rekodi nzuri ya kuwashawishi watu kumuunga mkono Obama.
Clinton aliambia wafuasi wa chama '' Amueni nchi mnayotaka kuishi. Ikiwa mnataka viongozi wasio wajali basi pigieni kura chama cha Republican. Mkitaka nchi yenye nafasi nyingi na ambayo majukumu yanagawanywa, basi sote tuko pamoja. Lazima mumpigie kura Barack Obama na makamu wake Joe Biden."
Bwana Clinton alikosoa vikali chama cha republican kwa kuzuia juhudi za uchepuzi wa uchumi na badala yake kujihusisha na mijadala kuhusu sera.
Kura za maoni zinaonyesha Barack Obama akiongoza kwa asilimia 47 huku mpinzani wake Mit Romney akimfuata kwa asilimia arobaini na sita.

Michelle Obama amuombea mumewe kura



Mkewe rais Obama , Michelle akihutubia kongamano la Democrats 

Mkewe Rais wa Marekani, Barack Obama, Michelle, amehutubia kongamano la chama tawala cha Democratic ambapo alitetea haki ya mumewe kupewa nafasi kutawala taifa hilo kwa muhula wa pili.
Akiongea Kaskazini mwa Jimbo la Carolina, alimtaja mumewe kama mtu anayeelewa matatizo yanayowakumba wamarekani.
Alitetea hatua ya mumewe ya kuanzisha mpango maalumu wa bima ya afya ulioleta utata mwingi sana hasa miongoni mwa wanachama wa chama cha upinzani cha Republican walioupinga.
Alisema kuwa mumewe alinuia kutoa nafasi sawa ya matibabu kwa wote. Hata hivyo alikiri kuwa mageuzi aliyoahidi mumewe miaka minne iliyopita yalikuwa magumu kuyatekeleza lakini akasisitiza kuwa yatafaulu baadaye.
Rais Obama atahutubia kongamano hilo baadaye juma hili, ambapo atakubali rasmi kuwa mgombea wa Urais wa chama cha Democratic.

Apple yaipiku Samsung mahakamani

Jopo la mahakama moja ya Marekani limeamua kuwa kampuni kubwa ya teknolojia ya Korea Kusini, Samsung, iliiga baadhi ya ufundi mpya wa kampuni ya Marekani ya Apple kuunda simu zake wenyewe za kisasa za smartphone na kumputa ndogo - tablet.
Simu za Apple na Samsung
Baada ya kesi iliyoendelea kwa mwaka mzima, ambayo ilichunguza mashtaka kama 700 ya aina ya ufundi ulioigwa, mahakama ya California yaliiamrisha Samsung iilipe Apple fidia ya dola zaidi ya bilioni moja.
Samsung imelalamika kuwa Apple inajaribu kuhodhi soko zima la smartphone, na imesema itakata rufaa.
Zaidi ya nusu ya simu za smartphone zinazouzwa duniani ni ama za Apple au Samsung, na kampuni hizo mbili zinashtakiana katika mahakama ya nchi mbali mbali duniani.

Ombi la Rais Obama kwa wamarekani



Rais wa Marekani Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama, amewaomba wamarekani kumpa fursa nyingine kuiongoza nchi hiyo.
Ombi lake amelitoa katika kilele cha kongamano la chama cha Democratic mjini North Carolina.
Akijiwasilisha kama mgombea wa urais mwenye kuleta matumaini kwa wamarekani, Rais Obama alisema kuwa uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba, utatoa fursa kwa wapiga kura kuchagua kati ya maono mawili tofauti kuhusu hatma ya Marekani.
Aliwataka Wamarekani kuwa wavumilivu akisema kuwa matatizo yanayokabili Marekani yamekuwa yakiongezeka kwa miaka mingi na kuwa itachukua muda kuweza kuyatatua.
Lakini aliongeza kuwa ikiwa watamchagua tena, ataweza kubuni nafasi mpya za kazi, kupunguza madeni na kuimarisha uchumi wa Marekani.
Rais Obama alisema anajiona kama kiongozi aliyekuwa amewekwa kwa mizani kujaribiwa uongozi wake na kuwa amefaulu. Alisema mpinzani wake wa Republican, Mitt Romney, hayuko tayari kwa mashauriano ya kidiplomasia.
Alitofautisha malengo yake na yale ya chama pinzani na kurejelea kauli mbiu yake ya mwaka 2008 , kuwataka watu kuwa na matumaini.
"sikuwahi kusema kuwa safari hii itakuwa rahisi na sitatoa ahadi hiyo hii leo'' Obama aliambia kongamano la wajumbe wa Democrat.
Mitt Romney wa chama cha Republican atapambana na Rais Obama kuwania urais huku kura za maoni zikionyesha wawili hao wakikaribiana.

Hofu ya vita kuhusu mpaka wa Sudan na S. Kusini



Mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu mzozo wa Sudan mbili
Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Susan Rice, amesema mzozo kuhusu mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini huenda ukasababisha vita kuzuka tena kati ya nchi hizo mbili.
Bi Rice ametoa matamshi yake katika mkutano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu mzozo wa mpaka kati ya nchi hizo nchini Marekani.
Sudan Kusini imekubali mpango wa amani uliopendekezwa na Muungano wa nchi za Afrika ingawa Sudan imeukataa.
Nchi hizo mbili nusura zipigane mapema mwaka huu sababu kuu ikiwa mzozo wa mpaka na ugawanaji wa mapato ya mafuta .
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka jana na kumaliza miaka mingi ya mapigano kati yake na Sudan.
Akiongea mjini New York, Bi Rice alisema kuwa hatua ya serikali ya Khartoum kukataa kusaini mpango wa amani inaweka nchi hizo katika hatari ya kurejelea vita.
Alisisitiza kuwa hatua ya kujikokota ya Khartoum inazua wasiwasi kuhusu kujitolea kwake kutatua mzozo huo.
Licha ya Sudan Kusini kukubali mpango wa amani, Bi Rice amekariri kuwa Marekani ina wasiwasi kwamba nchi hizo hazichukulii kwa uzito swala hilo kama ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa dharura.
Muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa mataifa wa kuafikia makubaliano mwezi Agosti tarehe mbili, haukuweza kufikiwa na nchi hizo mbili.
Hata hivyo, pande hizo mbili zinashinikizwa kutia saini mpango huo wa amani ifikapo tarehe 22 mwezi Septemba.
Mwezi jana serikali za Khartoum na Juba zilifanya mkutano wa wiki tatu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Kwenye mazungumzo hayo, mwafaka ulifikiwa wa kugawana mapato ya mauzo ya mafuta ingawa bado mazungumzo zaidi yanahitajika kuhusu usalama.
Mazungumzo hayo yataendelea mwishoni mwa mwezi Agosti.
Majeshi ya Sudan yamepigana mara kadhaa na yale ya Sudan kusini tangu Sudan kusini kujipatia uhuru mwaka jana.
Huenda baraza la usalama la umoja wa mataifa likaziwekea vikwazo nchi hizo iwapo zitashindwa kukubaliana kusitisha mzozo huo katika eneo la mpakani.

Kanisa la Anglikana lataka kuwa na rais

Askofu Mkuu wa kanisa la Anglikana, Rowan Williams, amefichua kuwa kanisa hilo linaandaa mpango wa kumteua rais wa kanisa, ambaye atabeba sehemu ya jukumu la kuongoza kanisa duniani.
Askofu Rowan Williams
Alisema mtu atayechukua nafasi hiyo ataweza kusafiri kwa urahisi, na hivo kumuacha Askofu Mkuu kushughulika zaidi na kuongoza kanisa.
Doctor Williams, ambaye anastaafu mwezi wa Disemba baada ya uongozi wa miaka 10, alikiri kuwa hakuweza kufanya mengi kuzuwia mgawanyiko kanisani juu ya swala la uhusiano wa jinsia moja.

John Tendwa


Makundi mbalimbali ya jamii yamesema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, hana ubavu wa kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwamba kauli aliyoitoa juzi ilikuwa ya jazba na ya kisiasa. Wamesema kauli hiyo haina mashiko kwa sababu makosa ya jinai hayafanywi na taasisi bali watu binafsi. Walisema suala hilo ni gumu kwa kuwa anapaswa kuangalia sera za chama na kwamba hadi sasa hakuna chama ambacho kina sera za mauaji ama uvunjifu wa amani.

DK. BANA: TENDWA ANATAKA KUWASHA MOTO 

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema si rahisi Tendwa kufuta Chadema, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuzua moto mkubwa, ambao ni vigumu kuuzima. Alisema kauli ya Tendwa ni ya kijazba na pia ni ya kisiasa, kwani ofisi yake haina uwezo wa kukifuta chama chochote cha siasa, kwa kuwa suala hilo ni la kisheria. “Sijawahi kuona msajili anafuta chama chochote japo baadhi ya vyama vimekuwa vikikiuka sheria. Kwa hiyo, si rahisi msajili kufuta Chadema. Anataka kuzua moto, ambao huwezi kuuzima,” alisema Dk. Bana.

Alisema kwa mujibu wa sheria, chama kinatakiwa kifutwe iwapo kitakiuka sheria na kwamba, hatua hiyo itachukuliwa hadi hapo vyombo vya sheria vitakapothibitisha ukiukwaji wa sheria uliofanyika. Hata hivyo, alivitaka vyama vya siasa kujenga maadili mema, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka halali iliyopo.

Tuesday, September 4, 2012

Historia ya Charles Taylor

 
Charles
Charles Taylor amekutwa na hatia

Mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imempata na hatia aliyekua Rais wa Liberia, Charles Taylor, kwa kosa la kushiriki na kusaidia uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji, ubakaji na ugaidi.
Mahakama ya huko The Hague imesema kua Bw Taylor anawajibika kwa kuunga mkono waasi wa kundi lililojulikana kama RUF yaani Revolutionary United Front katika nchi jirani ya Sierra Leone wakati wa vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe katika miaka 1990.
Bw Taylor ndiye kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kukabiliwa na hukumu mbele ya Mahakama ya Kimataifa tangu kesi maarufu za Nuremburg baada ya vita vikuu vya pili vya Dunia. Atahukumiwa mwezi ujao.
Maelezo yafuatayo yalikusanywa na kuandikwa na mwandishi wa BBC aliye nchini Liberia na mara kadhaa alikutana na Charles Taylor.
Charles Taylor alikua Rais wa Liberia kuanzia mwaka 1997 hadi alipojiuzulu mnamo mwaka 2003 kufuatia shinikizo kali za kimataifa. Alianza shughuli za siasa wakati wa ziara yake nchini Liberia kama kiongozi wa msafara wa mashirika ya Waliberia yaliyo barani Amerika mapema katika muongo wa 1980, mapinduzi ya kijeshi yalipofanyika naye kupewa kazi katika serikali ya Samuel Doe.
Baada ya kuteuliwa kama Naibu waziri katika Wizara ya biashara ya serikali ya Rais Doe, Taylor aliikimbilia Marekani kufuatia madai kwamba amepoteza takriban dola za kimarekani milioni moja.
Alifungwa huko Marekani lakini akatoroka jela katika mazingira ambayo hadi leo bado ni ya kutatanisha. Hatimaye aliunda kundi lake la waasi, lililojulikana kama National Patriotic Front of Liberia, ambalo liliiondoa serikali ya Samuel Doe madarakani.
Taylor
Alikuwa kiongozi wa waasi
Taylor ana kipaji cha kua mtu mchangamfu ambaye aliweza kumbadili adui na kumpenda kiasi cha kumfanya kua mfuasi sugu. Kwa mfano alipoingia mji wa Monrovia mnamo mwaka 1995 makumi kwa mamia ya watu waliompinga walijitokeza kumpokea na kumuimbia nyimbo za kumsifu kama shujaa.
Licha ya kuwateua watu wengi kama washauri wake lakini hiyo ilikua danganya toto'' kwa sababu hakufuata ushauri wao hata siku moja. Mmoja wa washauri wake wa karibu aliwahi kuniambia kua yaliyomfika Taylor yangeweza kuepukika kama angewasikiliza washauri hao.
Taylor alipenda sana kujifananisha na watawala wa enzi ya karne ya kumi na tisa kwa jinsi alivyowazawadia fukara akifahamu kua fadhila zake zitamjengea sifa na kumfaa siku moja.
Akiwa mpenda madaha alifahami vyema nguvu ya vyombo vya habari na jinsi ya kuvitumilia. Kupitia miaka ya 1990 alishiriki mahijiano mengi ya kipindi cha BBC cha Focus on Africa.
Katika kipindi cha kwanza, akiwa ni kiongozi wa kundi la waasi asiyefahamika, alitangaza mpango wake wa kuivamia Liberia.
Miaka michache baadaye, alipodokezewa na mtangazaji kwamba watu wengi wanamuonelea kua muuwaji, alilipuka na kusema ''Hata Yesu Kristu alituhumiwa kua ni muuwaji enzi zake.
Katika mahojiano mengi tuliyofanya naye daima alijitahidi kudhibiti mahojiano ili kutoa sura inayompendeza yeye. Mfano uilipomrushia suali lililomchukiza alijitahidi kulibadili liweze kusikika kwa manufaa yake.
Kama mpiganaji mahiri alijivunia uwezo wake wa kiume na uwezo wa kuzaa watoto wengi. Hakuficha siri yake ya kupenda wanawake, akidokeza wakati mmoja kua kama kiongozi wa Kiafrika ana haki ya hadi wake wanne.

Naomi
Mwanamitindo Naomi Campbell alihusishwa katika kesi ya Taylor

Wakosoaji wake walipokashifu tabia yake ya uzinzi, alijibu kwa kuwakemea wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na kujibu ''Bora mimi nawapenda wanawake.''
Mnamo mwaka 1996 alidokezea kua angetaka kujaliwa na watoto wengine watano na wote watakua wanaume. Hata hivyo hakujaliwa na ndoto yake hio watoto wake wawili waliofuata walikua wa kike.
Labda kama ishara ya kujiliwaza majaliwa hayo, aliwahi kuniambia kua kama mzazi anayewapenda wanawe, mume yeyote atakayewaoa wanangu, itabidi akubali watoto wake warithi jina la Taylor liendelee kudumu katika familia yao.

Wadai kuachishwa kazi kwa ajili ya imani zao

Watu wanne nchini Uingereza wanaodai kuwa waliachishwa kazi baada ya kubaguliwa kwa misingi ya dini yao, wanapeleka kesi yao katika mahakama ya haki za binadamu ya ulaya baadaye leo.
Kesi ya wanne hao ambayo waliwahi kuiwasilisha kwa jopo maalum kuhusu maswala ya ajira ilishindwa.

Mwandishi wa BBC Robert Pigott anasema kuwa uamuzi utakaotolewa kuhusu kesi hiyo katika mahakama hiyo , utakuwa muhimu sana hasa ikizingatiwa swala la mabadiliko ya mawazo kuhusu dinni ya kikristo kwa jamii.
Waliofikisha kesi hiyo mahakamani ni pamoja na mfanyakazi wa shirika la ndege la uingereza, Nadia Eweida, muuguzi Shirley Chaplin, mshauri nasaha na mtaalamu wa maswala ya mapenzi, Gary McFarlane na msajili wa watu Lilian Ladele.
Bi Eweida, mkristo wa madhehebu ya Pentecostal kutoka London,aliachishwa kazi mwaka 2006 baada ya kukataa amri ya kuvua mkufu wake uliokuwa na msalaba.

Kanisa nchini Uingereza
Muuguzi Chaplin pia aliachishwa kazi katika hospitali ya Royal Devon kwa sababu sawa na hiyo.
Bwana McFarlane, mshauri nasaha kutoka Bristol alifutwa kazi na kampuni ya Relate baada ya kusema kuwa aliona ugumu kutoa ushauri kwa wapenzi wa jinsia moja.
Naye Bi Ladele aliadhibiwa baada ya kukataa kuwafungisha ndoa wapenzi wa jinsia moja kaskazini mwa London.
Mapema mwaka huu, kilio cha wanne hao kiliungwa mkono na tume ya usawa na haki za binadamu nchini Uingereza, ambayo ilisema kuwa majaji walitafsiri kwa udhaifu sheria za usawa kwa madai ya udini.
Tume hiyo ilisema kuwa hatua hiyo iliwafanya waajiri kuweka sheria tata jinsi wakristo wanavyoweza kuishi kutokana na imani zao.
Katika kisa kilichomkumba muuguzi Chaplin, mwajiri wake alimwambia kuwa mkufu wa msalaba aliokuwa ameuvaa ulikiuka miongozo ya afya na usalama. Hata hivyo alishindwa kesi yake mwaka 2010

Walimu waanza mgomo wa kitaifa Kenya


Mabango ya walimu Kenya wakitaka kuongezwa mishahara
Maelfu ya walimu nchini Kenya wameanza mgomo wao rasmi wakidai kuwa serikali imekuwa ikipuuza kilio chao kuongezwa mishahara kwa miaka mingi.
Walimu hao ni wa shule za misingi na zile za upili na leo wamesusia kazi wakitaka nyongeza ya mishahara huku shule nyingi nchini humo zikiathirika.
Walimu hao wamekiuka agizo la mahakama lililoharamisha mgomo huo. Shule nyingi katika miji mikubwa mfano Mombasa, Nairobi na Nakuru zilisalia kufungwa.
Walimu hao wanadai nyongeza ya kati ya asilimia miamoja na miatatu.
Walimu wa shule za upili pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu wamesema watajiunga na mgomo huo baadaye wiki hii.
Mgomo huu unajiri wakati shule zikifungua kwa muhula wa tatu kitu ambacho walimu hao wanasema sio hoja kwani wamekuwa wakigoma kila muhula wa tatu unapofungua kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakidai hiyo nyongeza.
Wanasema kuwa serikali haina usawa katika mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwani ni hivi maajuzi tu wauguzi na wafanyakazi wengine wa umma walipoongezwa mishara baada ya kugoma. Wanadai kuwa walimu wamepuuzwa.
Mgomo huu umeonekana kufanikiwa kwani shule nyingi zimesalia kuwa bila walimu wanafunzi wengi wakibaki nyumbani.
Walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe kwa serikali kuwa wao hawawezi kula panya kwa mishahara midogo ambayo wanapata. Na vile vile walisema kuwa wamechoka na ahadi za uongo za serikali.
Mgomo huo uliitishwa na mashirika ya wafanyakazi yanayowakilisha takriban walimu laki mbili na nusu.
Wameahidi kuendelea na mgomo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Wachimba Migodi 122 waachiliwa Afrika Kusini

 
Wachimba migodi walioachiliwa

Wachimba migodi mia moja ishirini na wawili wa kampuni ya Lonmin yenye kuchimba madini ya Platinum wameachiliwa huru na Mahakama ya Kharankuwa iliyoko kaskazini mwa Pretoria.
Mara tu baada ya kuachiliwa wachimba migodi hao walikaribishwa nje ya mahakama na wenzao ambao walionekana kuimba nyimbo za kushangilia na kuwaelekeza katika eneo kulikotokea mauaji
Hatua ya kuachiliwa kwa wachimba migodi inakuja baada ya viongozi wa mashtaka kufutilia mbali mashtaka dhidi ya wachimba migodi 270 kufutia shinikizo za umma.
Wachimba migodi wa kwanza hao walikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya wenzao 34 waliouawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi.
Wakili wa wachimba migodi hao Bi Mapuli Kesi, alifurahia uamuzi huo wa mahakama na kunukuliwa akisema, "mimi ninayo furaha kubwa na ni ushindi mkubwa kwa kundi letu. Tumefanya kazi kubwa kufikia hapa tulipo."
Mwandishi wetu wa Afrika Kusini, Omar Mutasa, aliyekuweko mahakamani wakati kundi la kwanza la wachimba migodi lilipoachiliwa huru, alisema wachimba madini hao walilalamikia kile walitaja kuwa mateso mikononi mwa maafisa wa polisi.
Mmoja wao ambaye hakutaka kusema jina lake aliambia BBC, "polisi walikuwa wakali sana wakisema tusiwatazame na wakati mwingine walikuwa wakitutoa nguo na kutupiga marungu."
Hapo jana polisi waliwapiga riasasi na kuwajeruhi wachimba migodi wanne katika tukio tofauti .
Inadaiwa kuwa polisi walitumia risasi za mipira kuwatawanya waandamanaji katika Mgodi mwingine wa Gold Miners wanaogoma wakidai nyongeza ya mishahara ndipo wanne hao walipojeruhiwa.
Kisa hiki kinafuatia kuuwawa kwa wachimba migodi wengine 34 wakati walipopigwa risasi na polisi wiki mbili zilizopita.
Mazungumzo yanayolenga kusitisha mgomo wa wachimba migodi hao wa mgodi wa madini ya Platinum wa Marikana, vile vile yalitarajiwa kuanza hapo jana.
Polisi wanadai kuwa walilazimika kuwafyatulia risasi wachimba migodi hao kama hatua ya kujilinda kwani na wao walikuwa wamejihami kwa mapanga wakati wakikabiliana nao.
Mgomo wao ulioitishwa kulalamikia nyongeza ya mishahara pamoja na kutaka chama chao kipya cha wafanyakazi kutambuliwa, ungali unaendelea huku mgodi ukisalia kufungwa kwa wiki tatu sasa.
Hata hivyo kampuni inayomiliki mgodi huo, Lonmin, ambayo ndio ya tatu kwa ukubwa wa uzalishaji wa madini hayo, imesema kuwa mgomo huo ni haramu.
Lakini imetupilia mbali matakwa yake kuwa ikiwa wafanyakazi hao hawatarejea kazini , watafutwa kazi.
Baada ya ufyatuliaji risasi, viongozi wa mashtaka wa serikali, walitumia kanuni ya enzi ya ubaguzi wa rangi ya kosa la ujumla kuweza kuwafungulia mashtaka wachimba migodi 270 waliokamatwa wakati wa vurugu baada ya mgomo wao kuwalazimisha polisi kuwafyatulia risasi.
Kanuni hiyo ilitumika na walowezi wa kizungu wakati wa enzi ya ubaguzi wa rangi kuwanyanyasa wapinzani wao waafrika weusi.

New