Watu wanne nchini Uingereza wanaodai kuwa
waliachishwa kazi baada ya kubaguliwa kwa misingi ya dini yao,
wanapeleka kesi yao katika mahakama ya haki za binadamu ya ulaya baadaye
leo.
Kesi ya wanne hao ambayo waliwahi kuiwasilisha kwa jopo maalum kuhusu maswala ya ajira ilishindwa.Mwandishi wa BBC Robert Pigott anasema kuwa uamuzi utakaotolewa kuhusu kesi hiyo katika mahakama hiyo , utakuwa muhimu sana hasa ikizingatiwa swala la mabadiliko ya mawazo kuhusu dinni ya kikristo kwa jamii.
Waliofikisha kesi hiyo mahakamani ni pamoja na mfanyakazi wa shirika la ndege la uingereza, Nadia Eweida, muuguzi Shirley Chaplin, mshauri nasaha na mtaalamu wa maswala ya mapenzi, Gary McFarlane na msajili wa watu Lilian Ladele.
Bi Eweida, mkristo wa madhehebu ya Pentecostal kutoka London,aliachishwa kazi mwaka 2006 baada ya kukataa amri ya kuvua mkufu wake uliokuwa na msalaba.
Bwana McFarlane, mshauri nasaha kutoka Bristol alifutwa kazi na kampuni ya Relate baada ya kusema kuwa aliona ugumu kutoa ushauri kwa wapenzi wa jinsia moja.
Naye Bi Ladele aliadhibiwa baada ya kukataa kuwafungisha ndoa wapenzi wa jinsia moja kaskazini mwa London.
Mapema mwaka huu, kilio cha wanne hao kiliungwa mkono na tume ya usawa na haki za binadamu nchini Uingereza, ambayo ilisema kuwa majaji walitafsiri kwa udhaifu sheria za usawa kwa madai ya udini.
Tume hiyo ilisema kuwa hatua hiyo iliwafanya waajiri kuweka sheria tata jinsi wakristo wanavyoweza kuishi kutokana na imani zao.
Katika kisa kilichomkumba muuguzi Chaplin, mwajiri wake alimwambia kuwa mkufu wa msalaba aliokuwa ameuvaa ulikiuka miongozo ya afya na usalama. Hata hivyo alishindwa kesi yake mwaka 2010
No comments:
Post a Comment