My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, March 20, 2012

MKAPA, SLAA WACHAFUKA ARUMERU

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.

Na Mwandishi Wetu, Arumeru
WAKATI kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki zikishika kasi, tathmini ya jumla inaonesha kwamba viongozi wakubwa wa kitaifa nchini, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, wamechafuka.
Viongozi hao wenye heshima kubwa kitaifa, wamechafuliwa kutokana na makombora yanayoendelea kurushwa wakati huu wa kampeni, hivyo kuwafanya wananchi watumie muda mwingi kuwajadili Mkapa na Slaa badala ya wagombea husika.
Mwandishi wetu, pamoja na kufuatilia sera za wagombea amekuwa akipita mitaani kupata maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi huo na alichobaini kwa wiki nzima iliyopita ni mjadala mzito kuhusu madongo yaliyotupwa kwa Mkapa na Slaa.

MKAPA
Kauli yake kuwa Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vincent Nyerere si familia ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere, imemchafua hasa baada ya majibu ya mtoto mkubwa wa rais huyo wa kwanza wa Tanzania, Madaraka Nyerere.
Madaraka alitoa majibu kuwa Vincent ni ndugu yao, kauli ambayo imechukuliwa na wananchi wengi wa Arumeru Mashariki kwamba imemzodoa Mkapa, hivyo kupunguza heshima yake.
Kauli ya Vincent kuwa Mkapa alilazimisha Baba wa Taifa apelekwe Uingereza, kinyume cha ushauri wa daktari wake, Profesa David Mwakyusa, nayo imeibua mjadala mzito Arumeru Mashariki, huku wananchi wengi wakihoji kunani kifo cha Nyerere?
Vincent alidai kuwa kifo cha Nyerere ni tata akataka Mkapa aeleza siri aliyonayo.

SLAA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira ndiye anayetajwa kumchafua Slaa kutokana na dongo alilomrushia kuwa alifukuzwa ukasisi wa Kanisa Katoliki baada ya kufanya ufisadi kwenye fedha za mapokezi ya Papa John Paul II (hayati) alipokuja nchini Septemba Mosi 1990.
Wassira amedai kuwa mbali na Slaa kufanya ufisadi kwenye fedha za Kanisa Katoliki mpaka akafukuzwa pia ana kashfa ya kumfukuza mhasibu wa Chadema kwa sababu alikataa kumpa fedha, shilingi milioni 10, mchumba wake, Josephine Mushumbusi.
Japo inaelezwa kwamba Slaa anayo majibu kuhusu madongo hayo ya Wassira lakini mtaani kwa sasa amechafuka kutokana na jinsi wananchi wanavyomzungumzia.

KUHUSU UCHAGUZI
Uchaguzi Mdogo Arumeru Mashariki, unafanyika kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari aliyefariki dunia Januari 19, 2012.
Katika uchaguzi huo, mchuano mkali upo kati ya mgombea wa tiketi ya CCM, Sioi Sumari dhidi ya Joshua Nassari wa Chadema.

No comments:

Post a Comment

New