Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
*Asema haikubaliki, matatizo si yao*Mgomo wa madaktari hauepukiki
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema sharti la madaktari la kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, wawe wameachia ngazi kwanza ndani ya saa 72 ndipo majadiliano kati yao na serikali kuhusu maslahi yao yafanyike, halikubaliki.
Amesema sharti hilo halikubaliki si kwake (Pinda) tu, bali hata kwa bosi wa mawaziri hao, Rais Jakaya Kikwete, na kwa mtu mwingine yeyote, kwa vile linawaingiza kwenye mgogoro mpya katika muktadha wa mazungumzo kati yao ya kutafuta utekelezaji wa madai ya madaktari, hivyo ni gumu kutekelezeka.
Pinda aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu tamko lililotolewa na madaktari kwa nyakati tofauti wiki hii na wiki iliyopita, wakitishia kugoma leo.
Alisema tangu mwanzo wa mgomo wao, dai la msingi la madaktari lilikuwa ni kutaka kupitiwa upya uamuzi wa kuhamisha madaktari bingwa 61, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupelekwa wizarani na baadaye kupelekwa kwenye vituo mbalimbali vya afya.
Pinda alisema kufuatia dai hilo, serikali ilianza kuchukua hatua kwa kutafuta njia ya kulipatia ufumbuzi, pamoja na madai mengine yaliyomo kwenye ripoti ya kamati ya wataalamu aliyoiunda kupitia madai yote ya madaktari; kama vile nyongeza ya posho mbalimbali, ambayo alisema yote yanazungumzika.
“Lakini lilipokuja hili (la sharti kwanza Dk. Mponda na Dk. Nkya waachie ngazi ndipo majadiliano yafanyike), nikasema mnatupeleka pagumu,” alisema Pinda.
Alisema baya zaidi madaktari walipoibua sharti hilo, walidiriki kutamka kwamba, liwe limetekelezwa mara moja ndani ya saa 72 ndipo majadiliano kati yao na serikali kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya kamati hiyo yafanyike.
“Jambo hili ni la Rais. Hivi ifike mahali tumpe Rais saa 72 kwa sababu eti umebeba maisha ya watu? Mimi hilo siliafiki hata Rais hawezi kuliafiki. Hata angekuwa mtu yeyote asingekubali. Siwezi kumwambia Rais atekeleze hilo,” alisema Pinda.
Alisema suala la Dk. Mponda na Dk. Nkya kuachia ngazi au la, yote yanawezekana na kwamba, mchakato wake unaendelea vizuri.
Hata hivyo, alisema ambacho madaktari walipaswa kukihoji ni kujua mchakato huo ulikofikia hadi sasa, lakini si kuibuka na sharti jipya la kufanyika majadiliano kati yao na serikali.
Alisema kabla ya kuibuka na sharti hilo, Machi mosi, mwaka huu, walipokea barua kutoka kwa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) iliyosainiwa na Rais wake, Dk. Namala Mkopi, wakiiomba serikali majadiliano kati yao na serikali yasijumuishe makundi ya watu wengine wanaoguswa na sekta ya afya.
Alitaja makundi yaliyohusika na suala hilo yaliyokuwa na jumla ya wajumbe 12, ni pamoja na Utumishi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali, Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), MAT na Wizara ya Kazi na Ajira.
Pinda alisema kutokana na maombi hayo, alimweleza Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, azungumze na Dk. Mkopi amweleze kwamba si vizuri kutengana, lakini hilo halikukubalika.
Alisema mbali na jambo hilo kutokukubalika, madaktari waliamua kususia kikao hicho wakipinga kujumuika na makundi hayo.
Alisema upande wa serikali uliamua kuendelea na mazungumzo na makundi mengine, lakini makatibu wakuu waliowakilisha wizara husika kwenye kikao hicho waliona kikao hicho kisiendelee kwa vile madaktari ambao ndio wadau wakubwa hawapo.
Alisema Machi 2, mwaka huu upande wa serikali uliamua kuendelea na majadiliano na madaktari na pande zote mbili kila moja ulipeleka timu yake katika majadiliano.
Hata hivyo, alisema wakati kikao kinaanza, ndipo madaktari wakaibuka na sharti la kutaka kabla majadiliano kufanyika, kwanza Dk. Mponda na Dk. Nkya waachie ngazi.
“Nikasema tunaingia kwenye mgogoro mpya, kwani ilitakiwa tuingie kwenye majadiliano kwanza. Mgomo wa kihistoria siujui wala sura yake,” alisema Pinda.
Alisema Machi 3, walipata habari kuwa madaktari walikuwa na mkutano wao na kupata pia kwamba kuwaondoa Dk. Mponda na Dk. Nkya ni sharti lao la lazima kutekelezwa.
Pinda alisema sheria haiwaruhusu madaktari kugoma kutokana unyeti wa sekta wanayoifanyia kazi.
Kutokana na hilo, aliwataka madaktari kutogoma leo kama walivyodhamiria kufanya, badala yake warudi mezani kukamilisha hatua iliyofikiwa ya majadiliano na kwamba, serikali imekwishaanza kuchukua hatua kuhusiana na madai yao yote wanayoyadai.
Alisema njia ya majadiliano ndio mwafaka na kusema: “Kama madaktari wana dhamira nyingine fine (sawa).”
Pinda alisema matatizo katika sekta ya afya ni ya muda mrefu, hivyo si sahihi ‘kumshikia bango’ Dk. Mponda kutaka aachie ngazi kwani hana muda mrefu tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo.
“Haya matatizo ni ya muda mrefu. Dk. Mponda maskini ana mwaka mmoja na kidogo. Baba wa watu wa mwaka mmoja ndio imekuwa issue kweli? Turudi tufanye mazungumzo,” alisema Pinda.
Alisema anashangazwa na kauli ya madaktari kutishia kugoma leo, huku wakiionya serikali kwamba itakiona cha mtema kuni.
“Si serikali, ni wagonjwa ndio watakiona cha mtema kuni. Nawasihi madaktari waone busara, waone hekima ya kuwahurumia wasiokuwa na hatia,” alisema Pinda.
Akijibu swali serikali itachukua hatua gani iwapo madaktari watatekeleza azma yao ya kugoma leo, Pinda alisema: “Ngoja tuone kwanza, itakapotokea tutaona nini la kufanya.”
WANAHARAKATI: JK CHUKUA HATUA
Wanaharakati nchini wamemtaka Rais Kikwete kugeuka nyuma na kuangalia ukubwa wa tatizo la madaktari linaloendelea ili kulitatua kwa lengo la kuepusha vifo vinavyoweza kutokea ikiwa mgomo wao utafanyika leo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na wanaharakati hao kutoka mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya serikali (NGOs) na kusisitiza kwamba Rais ana wajibu wa kumaliza msuguano uliopo kati ya madakatari na serikali.
Akisoma tamko la pamoja, Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, aliwataka wananchi wote wanaojali wenzao kuinuka na kuchukua hatua ili kuishinikiza serikali kuchukua hatua ili kumaliza mgogoro wa madaktari.
Alisema kama kweli Rais anajali afya za wananchi ni lazima achuke hatua bila kusita kwa kuwa madhara ya mgomo ni makubwa endapo yatatokea tena.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, katika mkutano huo wa wanaharakati alimtaka Pinda amwangukie Rais Kikwete na kumuomba amalize mgogoro huo.
“Waziri Mkuu kama anajua kulia basi atumie machozi yake vizuri na kumuangukia Rais Kikwete amsaidie kumtimua Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake Dk. Lucy Nkya ili kumaliza mgogoro wa madaktari,” alisema
Aidha, Dk. Bisimba alitaka kila mwananchi aamke na kuitaka serikali ichukue hatua za haraka kushughulikia madai ya madaktari kwa kuwa suala la afya linamhusu kila mmoja.
Baadhi ya wanaharakati hao wanatoka mashirika ya LHRC, TGNP, WLAC, FARAJA TUST FUND, TAMWA na HAKIARDHI.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani jana walivamia mkutano huo na kuwa sehemu ya washiriki ambapo walijitambulisha na kushiriki hadi mwisho wa mkutano huo na waandishi wa habari.
MADAKTARI: MGOMO PALEPALE
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema kuwa mgomo wao uko pale pale na kwamba leo madaktari wataweka vifaa vyao chini bila kufanya kazi.
Alisema kuhusiana na taarifa aliyoyatoa Pinda ya kueleza kitendo cha kuwaondoa viongozi hao wawili ni madai mapya jambo hilo sio la kweli.
Dk. Ulimboka alisema madai hayo sio mapya na hata taarifa yao ya kwanza waliyompelekea waliweka taarifa hiyo na ndio maana Pinda aliamua kumsimamisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa.
Alisema Pinda aliwajulisha katika mkutano wao ambao ulifanyika Februari 9 mwaka huu kuwa suala la kumuondoa Dk. Mponda na Dk. Nkya hataweza kwani aliyewaajiri ambaye ni Rais Jakaya Kikwete atatolea maamuzi juu ya jambo hilo.
Akizungumzia hoja ya Pinda kueleza kuwa Dk. Mponda ni mgeni na wizara hiyo kwa madai kuwa matatizo ya madaktari yapo siku nyingi alisema hawakubaliani na suala hilo kwani pamoja na ugeni wake ameonyesha udhaifu mkubwa.
"Suala la kuondolewa katika wizara haliangalii ugeni wa mtu kwanza ana udhaifu mwingi wizara yake imemshinda embu niambie eti waziri anashindwa kutofautisha daktari ambaye anasoma mwaka wa nne na yule ambaye yupo internship Doctor haelewi," alisema Dk. Ulimboka
Alisema ili madai yao yaweze kutekelezwa ni pamoja na kuondolewa kwa viongozi hao ili mazungumzo yaanze rasmi.
Hata hivyo, alisema kuwajibishwa kwa viongozi hao serikali haihitaji bajeti yoyote katika kutekeleza jambo hilo.
Alisema hakuna mabadiliko yoyote ambayo wameyafanya na kwamba msimamo wao uko pale pale kuanza mgomo leo.
Alisema hakuna mazungumzo yoyote waliyofanya na Ofisi ya Waziri Mkuu mpaka sasa na pia hawajapokea taarifa yoyote dhidi ya madai yao.
"Sisi hatujabadilisha maamuzi yoyote msimamo wetu uko pale pale wa kuweka vifaa chini na hakuna mazungumzo yaliyofanyika na ofisi ya waziri mkuu tangu tulivyotoa tamko letu mpaka sasa na ndio maana tunasema mgomo unaanza kesho (leo) na hivi tunavyozungumza madaktari wanajiandaa," alisema
Alisema tayari ameshawajulisha madaktari wengine wa mikoani kuhusiana na suala hilo na wameliafiki kufanya mgomo ili serikali iwapatie madai yao
No comments:
Post a Comment