My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, March 15, 2012

Tatizo la uchafu Dar es Salaam; Tujifunze kutoka Moshi na Iringa

Haika Kimaro
UCHAFU katika jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ni moja ya matatizo makubwa na ambayo ni dhahiri uongozi wa jiji hili unaelekea kuwa umeshindwa kulipatia ufumbuzi. Ni mengi yamesemwa kuhusu aibu hii kubwa ua uchafu kwa jiji hili ambalo linapaswa kuwa kioo kwa taifa letu (Tanzania) kwa usafi kutokana na kupokea wageni wa kimataifa ambao huja nchini kwa shughuli mbalimbali.

Lakini, kukithiri kwa uchafu katika maeneo mengi ya jiji hili pamoja na kushindikana kuzolewa kwa taka laini na ngumu ni changamoto ambayo inalikabili jiji hili na wakazi wake. Nionavyo mimi ni uchafu huo ni kana kwamba umefunika nyuso viongozi wetu wakiwamo wa jiji na manispaa zake tatu kiasi kwamba hawahangaiki nao tena.

Tatizo hili, sielewi kwani limekuwa mzigo kwani naamini watendaji wengi wa jiji na manispaa zake wamepata nafasi ya kutembelea nchi nyingi duniani ambazo naamini wamepata fursa ya kujifunza.

Kama bado naamini hao wangeweza kujifunza kutoka miji michache nchini ambayo inaongoza kwa usafi na mazingira yao yanaridhisha. Suala hili la usafi ambalo ni hulka linatakiwa kupewa mtazamo mwingine na jamii, tukiongozwa na wakuu wetu ambao hawana budi kueleza wenzao wamefanya nini hata miji yao ikawa katika viwango vya usafi vya hali ya juu.

Iwapo wameshindwa kujifunza huko, basi wakuu hao wa Dar es Salaam na manispaa zake kama hawaoni tena aibu ya uchafu kiasi cha kuliacha jiji likigeuka ‘jalala’, nawashauri waende wakajifunze kule Moshi, mkoani Kilimanjaro au katika Manispaa ya Iringa.

Ni wazi kwamba miji hii imepiga hatua kubwa inayofaa kupigiwa mfano kwa usafi. Pengine, swali la kujiuliza ni kwa nini Moshi au Iringa waweze, halafu Dar es Salaam ambako ni makao makuu ya shughuli karibu zote za nchi, washindwe? Hapa kuna tatizo tena tatizo kubwa ambalo tiba yake nadhani bado hijapatikana.

Ni wazi kuwa katika Jiji la Dar es Salaam kuna upungufu mkubwa wa vifaa vya kuwekea takataka hasa katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama vile vituo vya mabasi ya abiria (daladala), viwanja vya mpira na maeneo ya kazi.
Hali hii inachangia sana kukithiri kwa uchafu katika maeneo mengi ya jiji kwani utamshawishi je mtu kuzunguka akiwa amebeba takataka mkononi kutwa nzima akitafuta sehemu ya kuihifadhi? Takataka ni mzigo, iwe ni chupa ya maji ya kunywa au mfuko wa plastiki.

Iwapo mtu anatoka katikati ya jiji akiwa na chupa ya maji mkononi, pale anapomaliza kunywa maji yake hawezi kuzunguka na chupa hiyo kutwa nzima eti anatafuta sehemu ya kutupa, ni dhahiri kwamba kuna wakati uvumilivu utamshinda na kuitupa popote bila kujali kama utupaji huo una athari katika mazingira husika.

Ni wazi kuwa uchafu husababisha magonjwa ya milipuko hususan kuhara na kipindupindu. Ajabu ni kwamba viongozi wa jiji la Dar es Salaam utawaona wakihaha kujaribu kuokoa maisha ya wagonjwa wa kipindupindu.
Ninadhani viongozi wa jiji wamesahau kwamba kuzuia ni bora kuliko kuponya. Kama viongozi wa jiji la Dar es Salaam wangekuwa wakilipa umuhimu suala la usafi kama ambavyo huangakika kuanzisha kambi za wagonjwa wa kipindupindu, basi jiji hilo lingekuwa katika hali tofauti na sasa.

Tatizo ni kwamba viongozi hawa kama walivyo viongozi wetu wengi, wamejenga utamaduni wa kutekeleza majukumu yao katika hali ya dharura. Kila kitu ni dharura, hakuna kazi wanayoweza kuifanya katika utaratibu wa kawaida wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Dharura hizi ni mbaya tena ni mzigo kwa umma wa Watanzania.

Kwanza, dharura haitatui matatizo ya wananchi kwa asilimia 100, kwani kipindupindu kikilipuka wapo wengine hupoteza maisha. Hawa roho zao haziwezi kurudi, hata tungefanya nini. Mzigo mwingine ni gharama. Gharama za kufanya mambo kwa dharura ni kubwa, tena wakati mwingine huathiri utekelezaji wa majukumu mengine ambayo pia ni muhimu kwa umma.
Lazima viongozi wetu wajifunze na wakubali kubadilika. Wakati wa mvua za masika jijini Dar es Salaam huwa ndio wakati wa kipindupindu. Tunahitaji viongozi makini ambao watatuwezesha kuondokana na aibu hii ya kila mwaka.

Wakati wa masika usiwe wakati wa kipindupindu bali uwe wakati mwema na wa kufurahia maisha kwa wakazi wa Dar es Salaam. Nasema hivi kwani mvua hizo zinaongeza changamoto na hatari ya magonjwa ya mlipuko. Wapo wanaozitumia vibaya kwa kufungulia mifereji ya maji machachu na kinyesi.

Tabia hii pia inatoa funzo lingine kwetu. Kwamba pamoja na kuwepo kwa sheria ndogo za kudhibiti watu wanaochafua mazingira kwa makusudi, lakini kuna jambo la ziada linapaswa kufanywa. Hili si jingine bali ni elimu kwa umma. Wahenga walisema “Hiari yashinda utumwa”.

Lazima ufike wakati ambao sehemu kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam wanabadilika na killa mmoja anajiona kuwa msimamizi wa usafi katika eneo alilopo, iwe nyumbani, kazini au kwingineko.Elimu kwa umma ni muhimu, watu wahamasishwe na watiwe shime ili wawe washiriki wa kampeini ya usafi wa jiji kila siku na kila wakati.

Katika manispaa ya Moshi hii ndiyo siri ya mafanikio ya mji waokuwa safi wakati wote. Wasimamizi wa usafina ni wananchi wenyewe kwa wenyewe. Mjini Moshi ukitupa hata vocha ya simu iliyotumika unakamatwa na kutozwa faini tena bila ajili. Hawana mzaha na sauala la usafi na hapo wamefanikiwa.

Inawezekana sheria zetu katika jiji la Dar es Salaam zimetungwa kulenga kukusanya fedha zinazotokana na faini. Sawa, faini kama adhabu nyingine mimi sipingani nayo. Lakini kujikusanyia mamilioni ya faini sidhani kama una tija kama hakuna mabadiliko ya hali ya usafi.

Tuamke sasa, tulifanye suala la uchafu na kipindupindu katika jiji la Dar es Salaam kuwa historia.
Haika Kimaro ni mwanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Time (TSJ).

No comments:

Post a Comment

New