Mji wenye moja ya maajabu saba mapya ya dunia
NI nyumba zilizochongwa kwenye miamba ya mawe. Au kwa msemo mwingine, ni mawe yaliyochongwa nyumba.
Ni moja ya maajabu mapya saba ya dunia yaliyopitishwa hivi karibuni.
Maajabu hayo yako katika Mji wa Petra huko Jordan.
Gazeti hili liliwahi kuandika kuhusu ‘miujiza’ hiyo, sasa linatoa simulizi pana zaidi kuhusu maajabu hayo yaliyofanywa na mikono na akili ya binadamu yakiwa moja ya maajabu saba mapya duniani.
Petra ulianzishwa karne ya sita Kabla ya Kristo (KK) katika miteremko ya Mlima Hor.
Petra ni neno la Kigiriki likimaanisha ‘mwamba’ (jiwe). Huo ulikuwa mji mkuu wa watu wa kabila la Kiarabu la Nabataea. Uko eneo la milima ya rangi nyekundu ukiwa na majumba na makaburi yaliyochongwa kwa nakshi, urembo na utaalam wa hali ya juu.
Taifa la Nabatea lililofanya maajabu hayo ‘yasiyoaminika’, lilitoweka zamani ambapo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita waliufanya mji huo kuwa kiungo muhimu cha biashara ya hariri na viungo (vya chakula) katika njia za kwenda China, India, Arabia ya Kusini, Syria, Ugiriki na Roma.
Mji huo ulikuwa haufahamiki kwa walimwengu wa nje hadi mwaka 1812 alipofika huko mvumbuzi wa Uswiss, Johann Ludwig Burkhardt, hatimaye kutangazwa ulimwenguni kuwa ni moja ya sehemu 40 ambazo mtu ‘analazimika kuziona kabla ya kufa’.
Eneo hilo liko jangwani na anayelitembelea inambidi kuvaa viatu, kofia na kubeba maji mengi ya kunywa ili kupambana na joto kali.
Utaalam huo wa kuchonga miamba ulitokana na utamaduni wa watu wa eneo hilo kuwazika watu katika mapango ya mawe. Huo ukawa mwanzo wa kupata utaalam wa kuchoga miamba.
Mbali na majengo na makaburi kuna pia mahekalu, viwanja vya michezo na minara, vyote vikiwa vilichongwa kwenye miamba. Mojawapo ni uwanja wenye uwezo wa kuingiza watu 3,000 uliochongwa kwenye miamba na ‘viti’ vya watu kukaa.
Hiyo ndiyo Petra ambayo kwa simulizi za Kiarabu, ni sehemu ya Nabii Moses (Musa) wa kwenye Maandiko Matakatifu, alipiga mwamba kwa fimbo yake na maji yakatoka, ndipo ambapo Aaron (Harun) kaka wa Musa alipozikwa katika Mlima Hor ambao leo unajulikana kama Jabal Haroun au Mlima Aaron.
Ni sehemu hiyohiyo pia ambapo Miriam (Mariam) dada wa Moses anaaminika alizikwa, bila kusahau kwamba bonde jembamba la kuingilia Petra linajulikana kama ‘Wadi Musa’ yaani ‘Bonde la Musa’.
Jengo lililochongwa kwenye mwamba.
Watalii wakiishangaa sanaa hiyo ya zamani.
No comments:
Post a Comment