My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, March 7, 2012

ZOEZI LA TBS KUKAGUA MAGARI UINGEREZA NI MCHEZO WA KUIGIZA

Ukaguzi wa magari yaingiayo nchini kutoka Uingereza unalalamikiwa kwamba unafanyika ndivyo-sivyo.

TENDA iliyotolewa na serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kufanya ukaguzi wa magari nchini Uingereza kabla ya kuletwa nchini, inasemekana imezaa zoezi la kuigiza kwani kazi iliyodhamiriwa si hiyo inayofanywa hivi sasa. Msomaji wetu wa mtandao ambaye yuko nchini Uingereza (jina lake tunalo) na anayefuatilia zoezi hilo ameeleza yafuatayo kwa kifupi:

….”Tenda ya ukaguzi wa magari iligawiwa kiholela kwa watoto wa wakubwa mwaka 2007 na huko Uingereza ilipewa kampuni ya WTM UTILITY ambayo ni kampuni ya fundi bomba na mmiliki wake ni mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa TBS aliyejulikana kama Mama Mtabazi ambaye sasa ni marehemu.

Toka kampuni hiyo imepewa tenda hiyo haijawahi kununua hata spana kwa ajili ya ukaguzi wa magari bali imekuwa ikiuza vyeti vya ukaguzi kuonyesha kwamba magari hayo hayana matatizo.

Kwanza kijana huyo husika alikuwa hana hata ofisi lakini watu walipopiga kelele ndipo akafungua kajiofisi kwenye chumba kimoja cha jumba moja kuukuu jijini London. Kuna kipindi wakaguzi wa TBS walipokwenda Uingereza kijana huyo akawapeleka kwenye gereji moja jirani na ilipo ofisi yake na kuwaambia kwamba wafanyakazi wa gereji hiyo ndiyo waliokuwa wakaguzi wa magari husika.

Pia inasemekana fedha nyingi za biashara hii ya vyeti vinavyodaiwa kuwa vya ukaguzi hazifikishwi serikalini bali huishia midomoni mwa wajanja wachache wenye dili hilo.

Hii tenda ilitangazwa tena mwaka jana tarehe 28/07/2011 chini ya kumbukumbu No (PVoC) TENDER NO PA/044/2010/2011/NC/02 ambapo makampuni manane yaliomba tenda hiyo na kijana huyohuyo wa WTM akaingiza kampuni mbili kwenye mchakato huo zote zikiwa zake -- WTM UTILITY SERVICES LTD na AWS.

Alifanya hivyo akijua kati ya kampuni hizo mbili moja lazima ingenasa tenda hiyo licha ya kufahamu kwamba wafanyakazi wengi wa TBS walikwishang’amua mtu huyo alivyokuwa anaharibu jina la shirika lao. Katika hilo alitamba kuwa alikuwa na kigogo mmoja wa TBS aliyekuwa anamlinda.

Mchakato wa tenda uliendelea na zikabakia kampuni tatu kwenye mchakato huo kutoka Uingereza ambazo ni: WTM UTILITY SERVICES, INTERTEK INTERNATIONAL LTD na SERENGETI FREIGHT FORWARDERS LTD.

Tenda zilifunguliwa rasmi mwezi wa tisa mwaka jana na matokeo mpaka sasa hayajatangazwa lakini kijana huyo wa WTC anaendelea na kuuza “vyeti vya ukaguzi”.

Ikumbukwe kwamba tenda ilipotangazwa makampuni mengine yalitumia fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya ukaguzi wa magari pamoja na kuwatuma wajumbe wake Tanzania kwenye mikutano ya tenda.

Ni ajabu kwamba hali hii inaendelea licha ya malalamiko juu ya jambo hilo kufikishwa kwa kamati husika ya bunge inayowajumuisha Waheshimiwa Wabunge, Zitto, Cheyo na Filikunjombe.

Ukweli ni kwamba hakuna ukaguzi wa kweli wa magari unaofanyika Uingereza na Watanzania wanaoishi nchini humo wanafahamu hilo wazi.

Kinachofanyika ni wizi wa fedha za Watanzania na uongo ambao utaliletea hasara taifa letu.

Hatua lazima zichukuliwe sasa kabla hali haijaharibika bila hivyo watu tunaloifahamu suala hili tutajitokeza bila woga na kuweka mambo bayana”… alisema msomaji huyo na kuongeza kuwa yuko tayari kutoa ushahidi wa anachokisema kwa mamlaka itakayohitaji. kwa wanaohitaji mawasiliano wawasiliane na web master wa mtandao huu.

No comments:

Post a Comment

New