Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akiwatangazia waandishi wa habari,
jijini Dar es Salaam jana, juu ya kuwasimamisha kwa muda Mkurungenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Watendaji wengine wa Mamlaka hiyo
ili kupisha uchungunzi wa tuhuma mbalimbali katika bandari. Picha na
Fidelis Felix
AMSIMAMISHA MKURUGENZI MKUU, WENGINE WATANO,AANIKA UFISADI, RUSHWA, WIZI WA MAFUTAFidelis Butahe
WAZIRI
wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe, wasaidizi wake
wawili na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo kupisha
uchunguzi wa wizi wa vitu mbalimbali yakiwamo makontena 40 ya vitenge,
katika Bandari ya Dar es Salaam.
Dk Mwakyembe alitangaza uamuzi
wake huo jana jijini Dar es Salaam, akiendeleza kile alichokifanya Juni 5
mwaka huu alipomtimua kazi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi.
Hata hivyo, waziri
huyo hakutaja majina ya vigogo waliosimamishwa na badala yake alitaja
nafasi walizokuwa wakizishikilia ambazo ni pamoja na Meneja wa Kituo cha
Mafuta ya Ndege Kurasini (Kurasini Oil Jet - KOJ), Meneja wa Kituo cha
Mafuta JET na mhandisi wa mafuta wa kituo hicho, baada ya kubainika
kuwapo kwa wizi wa mafuta.
Kutokana na uamuzi huo, Dk Mwakyembe
amemteua Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi,
Injinia Madeni Kipande kukaimu nafasi ya Mgawe.
Gazeti hili
lilimtafuta Mgawe kwa simu kuzungumzia uamuzi huo, lakini simu yake ya
mkononi ilikuwa ikiita muda wote bila majibu na wakati mwingine kukatwa.
Uamuzi
huo umekuja baada ya kuwapo kwa taarifa za kupotea kwa makontena
takriban 40 ya vitenge na vitu mbalimbali, yaliyokuwa yakipelekwa nchi
jirani.
Dk Mwakyembe alisema ameunda kamati ya watu saba ambao
hakuwataja majina ili kuchunguza wizi huo na kwamba amewapa wiki mbili
tu, wawe wamekamilisha kazi hiyo.
“Nimeunda kamati ya kuchunguza
suala hili, nimewapa hadidu za rejea zenye maswali 50..., majina ya
waliopo katika kamati hii siyatangazi kwa sasa kwa sababu zangu
binafsi,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema amechukua uamuzi huo
baada ya kukutana na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA juzi na kwamba hawezi
kuvumilia kuona nchi inakosa mapato kwa sababu ya wizi uliokithiri.
Alisema
kwa muda mrefu katika bandari hiyo ya Dar es Salaam, kumekuwa na
malalamiko ya wizi wa vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ule wa vifaa
vya magari, mafuta na kukithiri rushwa.
Alifafanua kwamba wizi
huo umesababisha Bandari ya Dar es Salaam kukimbiwa na wateja ambao hivi
sasa wanatumia bandari za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.
“Makontena
yanaibwa kama njugu, hivi sasa watu wa Rwanda, Uganda DRC hawaitumii
tena Bandari ya Dar es Salaam, wanaona bora waingie hasara na wameanza
kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Mombasa Kenya, Beira nchini
Msumbiji na Durban Afrika Kusini,” alisema Dk Mwakyembe.
Dk
Mwakyembe alisema kuwa hivi karibuni mfanyabiashara mmoja mwanamke
alitishia kuhamia nyumbani kwake, baada ya kuibiwa kontena zima la
vitenge vilivyokuwa na thamani ya dola 180,000 za Marekani.
“Ni
mambo ya ajabu sana hatuwezi kuwa na maendeleo kwa masuala ya ‘kisanii’
kama haya, nimeamua hivi kutokana na mamlaka niliyonayo na uamuzi
nitakaouchukua najua wenzangu watanielewa,” alisema.
Wakati
akieleza majukumu ya Mamlaka hiyo alisema, “Nimewataka TPA watambue
majukumu yao jinsi yalivyo nyeti, nimewaeleza wazi kuwa imani ya
wananchi imepungua sana kwa mamlaka hiyo.
“Kama waziri mwenye
dhamana sitakuwa tayari kuona jambo hili linaendelea, hili suala
haliwezi kuachwa likaendelea ni lazima uchunguzi ufanyike.”
Dk
Mwakyembe alisema kuwa ameiagiza bodi ya wakurugenzi, kitengo cha sheria
TPA kiuchambue upya mkataba wa Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena
katika Bandari ya Dar es Salaam (Ticts) na kumpatia taarifa Jumatano
ijayo.
“Kontena likiwa na vitenge hata ukiweka askari 40
linaondoka, tumepoteza wateja wengi na watu wanaona bora kukimbilia
bandari nyingine, nimewaagiza wauchambue upya mkataba huu,” alisema Dk
Mwakyembe.
Agizo
Alisema ili kukomesha rushwa ameitaka
Bodi ya Wakurugenzi TPA, kuanzia Septemba mosi mwaka huu kuacha kutumia
utaratibu wa kulipa fedha dirishani, badala yake fedha zote zilipwe
kupitia benki.
“Mtindo wa malipo ya fedha dirishani ndiyo
unachochea wizi unaofanywa na mtandao wa kisanii pale TPA. Nimeagiza
malipo yote yafanyike kupitia benki au kwa njia zozote za teknohama
kuanzia Septemba mosi,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Kama
malipo haya yakiendelea mwezi ujao watakaolipa waandike tu wenyewe barua
za kuacha kazi, kampuni ndogondogo nchini zinalipa fedha kupitia benki,
kwa nini TPA washindwe?”
Aliongeza kuwa ameiagiza bodi hiyo
kuangalia upya mfumo mzima wa uongozi wa TPA na bandari kwa kuwa kuna
viongozi wana mamlaka makubwa wakati vyeo vyao ni vidogo.
“Meneja
wa bandari ana mamlaka makubwa kiasi kwamba utendaji kazi ndani ya
bandari unasuasua wakati wapo viongozi wa juu yake,” alisema Dk
Mwakyembe.
Wizi wa mafuta
Akizungumzia wizi wa mafuta, Dk
Mwakyembe alisema katika kituo cha KOJ kuna wizi mkubwa wa mafuta ambapo
wahusika wakibanwa hutoa kisingizio kuwa mafuta yanayochukuliwa ni
machafu.
“Mafuta yale siyo machafu, hiyo imekuwa ndiyo biashara
yao kila mwaka, ndiyo maana tenda ya mafuta machafu inagombewa sana,
tumefuatilia na kugundua kuwa yanapelekwa katika vituo mbalimbali vya
mafuta nchini” alisema Mwakyembe na kuongeza:
“Niliwahi kwenda
katika eneo lile saa 12 asubuhi na kukuta malori yanajaza mafuta.
Niliuliza lori lina uwezo wa kupakia lita ngapi, kuanzia meneja mpaka
watu wa chini kabisa walishindwa kunijibu.”
Alisema kutokana na
kitendo hicho, amechukua sampuli ya mafuta hayo na kuyapeleka Mombasa,
Kenya kuyapima ili kugundua yana kiwango cha mafuta masafi kwa asilimia
ngapi.
Alisema kuwa malori hayo yana uwezo wa kupakia lita 26,000
za mafuta lakini wahusika wanadai kuwa yanaweza kupakia lita 9,000 tu.
“Mafuta
haya huibwa wakati yakitolewa katika meli na kupelekwa katika magari,
karibu asilimia mbili nzima ya mafuta huibwa, kiwango ambacho ni kikubwa
sana,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ameagiza
kurejeshwa kwa kifaa cha kupimia wingi wa mafuta katika malori ya
mafuta, ndani ya mwezi mmoja kuanzia jana.
Aanika ufisadi
Alisema
kampuni ya Singirimo iliyopewa zabuni ya kusafirisha mafuta machafu,
mkataba wake ulishaisha siku nyingi, lakini bado inaendelea na kazi hiyo
na kwamba mwaka 2008, Ikulu iliwahi kueleza kuwa kampuni hiyo ni kinara
kwa kusafirisha mafuta masafi na kudai machafu.
“Kampuni hii
kila mwaka inashinda tenda ya kusafirisha mafuta tu, hivi sasa
inachunguzwa na Ewura na Takukuru, nimeagiza mamlaka husika kwamba
kampuni hii isijihusishe tena na usafirishaji wa mafuta ili kupisha
uchunguzi,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Kampuni iliyokuwa
namba mbili katika utoaji wa tenda ndiyo ipewe jukumu hilo na kama
isipopewa ndiyo nitajua kuna kitu kinaendelea.”
Alisema kuwa
mwaka 2008 Ikulu ilisema kuwa kampuni ya Singirimo ni ya wafanyakazi na
vigogo wa TPA na inasafirisha mafuta masafi na kudai kuwa ni machafu.