Muda mwingi umekuwa
ukipotea bungeni kutokana na baadhi ya mawaziri na wabunge kuanza
kuchangia hoja kwa kuongea mambo ambayo kwa kweli hayana msingi wowote
kwenye hoja husika. Kwa mfano, unakukuta waziri anaanza kujibu hoja za
wabunge waliyochangia makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa kuwataja
majina wabunge wote waliochangia wote. Wakati mwingine inamchukua waziri
karibu nusu saa akitaja na kushukuru wale wote waliochangia kwenye
bajeti yake.
UTANGULIZI
Hotuba nyingine za bajeti zinaanza na utangulizi mrefu ambao hauna uhusiano wowote na bajeti husika. Kwa
mfano soma hapo chini utangulizi wa hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa kwa mwaka 2012/2013. Zaidi ya kupoteza muda utangulizi
huu hauhusiani kabisa na hotuba ya makadirio ya wizara. Ifike wakati tuzingatie muda hasa bungeni na sehemu nyingine za kazi hasa zile za umma.
HOTUBA YA WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA
TAIFA, MHESHIMIWA SHAMSI VUAI NAHODHA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013
1. Mheshimiwa Spika, baada ya
Bunge lako Tukufu kupokea taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa
Mwaka wa Fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, kwanza
napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyenijalia afya
njema na kuniwezesha kuwasilisha hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka
2012/2013. Pili namshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuniteua
kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Nawathibitishia
Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote wa Tanzania kwamba
nitatekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, tatu
napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri
walioteuliwa kushika nyadhifa hizi hivi karibuni. Vile vile nampongeza
Mhe. James Mbatia (Mb.) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge.
Nampongeza pia Mhe. Mussa Azan Zungu (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Bunge. Vile vile napenda kuwapongeza Watanzania
waliochaguliwa na Bunge letu Tukufu kuwa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki.
4. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Mwaka wa Fedha 2011/2012 Wabunge wenzetu watatu waliiaga
dunia. Wabunge hao ni Marehemu Jeremia Sumari, Marehemu Mussa Silima na
Marehemu Regia Mtema. Napenda kutoa pole za dhati kwako Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge, ndugu, marafiki na Watanzania wote kwa
ujumla kwa msiba huo mkubwa uliotupata. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze
roho zao Peponi. Amin.
5. Mheshimiwa Spika, halikadhalika,
napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Edward Lowassa, Mbunge
wa Monduli kwa kutupa ushauri na mapendekezo mazuri sana wakati
wakichambua mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara
yangu. Kamati hii imekuwa ikiishauri vyema Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa kuhusu njia mbalimbali za kuimarisha utendaji wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Kujenga Taifa ili liweze kutekeleza
majukumu yake ya Ulinzi wa nchi yetu.
6. Mheshimiwa Spika, kabla
sijatoa maelezo yangu kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2012/2013 napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge kuwapongeza Mheshimiwa
Mizengo Kayanza Pinda (Mb), Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mhe. Dk.
William Mgimwa (Mb), na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Mheshimiwa Steven Wasira (Mb) kwa hotuba zao ambazo zimetoa
mwelekeo katika masuala ya Mipango, Uchumi, Mapato na matumizi ya
Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Hotuba nzima inapatikana: http://www.modans.go.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=107&Itemid=123
No comments:
Post a Comment