MKUTANO Mkuu wa Wanachama Wote wa Simba utafanyika Agosti tano 
mwaka huu katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay kama ilivyopangwa.
Mipango yote kwa ajili ya mkutano huo muhimu kikatiba imekamilika 
na klabu inawaomba wanachama wake wote hai kuhudhuria mkutano huo 
muhimu.
Uongozi umepanga kutoa mabasi kwa ajili ya kuwasafirisha wanachama 
wake kutoka katika maeneo mbalimbali kwenda katika ukumbi wa mikutano.
Kutakuwa na mabasi matatu kwenye eneo la Shibam Magomeni... Mabasi 
matatu Temeke mwisho na mabasi matatu katika makao makuu ya Simba SC 
Mtaa wa Msimbazi.
Pia klabu itapeleka mabasi mawili katika wilaya za Mkuranga na 
Kibaha kwa ajili ya kuwaleta wanachama wake walio katika mkoa wa Pwani 
kuhudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amewahakikishia 
wanachama wa Simba kwamba mkutano huo utaendeshwa kisasa na usalama 
umehakikishwa kwa asilimia 100 kwa vile eneo la mkutano liko chini ya 
Jeshi la Polisi.
"Napenda kuwahakikishia wanachama wote wa Simba kwamba mkutano huo 
utakuwa bora na wote watakaokuja watafurahi na kujisikia fahari kuwa 
washabiki wa klabu ya soka ya Simba. Kwa wale ambao wamepanga kuja 
kufanya vurugu kwenye mkutano huo, klabu itaviachia vyombo vya dola 
vifanye kazi yake," alisema.
NGASSA
MCHEZAJI mpya wa Simba, Mrisho Ngassa, leo amekabidhiwa jezi namba 16 atakayokuwa akiitumia kwenye klabu yake msimu huu.
Ngassa alikabidhiwa jezi yake hiyo katika makao makuu ya Simba Mtaa
 wa Msimbazi jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey
 Nyange Kaburu.
Kaburu alisema Simba inamkaribisha Ngassa kwa moyo mmoja na kwamba 
wapenzi wote wa Wekundu wa Msimbazi wana imani kubwa naye kwani uwezo 
wake mkubwa wa soka unafahamika ndani na nje ya nchi.
"Tunashukuru kwamba tumekidhi vigezo vyote vilivyohitajika kwa 
ajili ya usajili wa mchezaji huyu. Tumeingia naye mkataba wa mwaka mmoja
 baada ya kumaliza muda wa mkopo wake kutoka Azam na ni imani yetu 
kwamba ujio wa Ngasa utaimarisha zaidi timu kwani yeye ni miongoni mwa 
wachezaji ambao Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic, anawapenda," 
alisema. 
Akizungumza katika tukio hilo, Ngassa alisema amefurahi kusajiliwa 
na Simba kwani ni sawa na historia kujirudia, akikumbusha kwamba baba 
yake mzazi, Khalfan Ngassa, aliwahi kuwa mchezaji wa klabu katika miaka 
ya 1990.
Kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, Ngassa alifanya 
mazoezi na wachezaji wenzake wa Simba katika ufukwe wa Coco, jijini Dar 
es Salaam ambako Simba inaendelea na mazoezi yake chini ya makocha 
Amatre Richard na James Kisaka.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment