Na Walusanga Ndaki
JE, ulikuwa na umri wa miaka mingapi wakati mfalme wa muziki wa Pop wa Marekani, hayati Michael Jackson alipoitembelea Tanzania mwaka 1992 na kufika shule maalum ya watoto yatima na wenye mtindio wa ubongo iliyopo Sinza?
Mwanamuziki huyo aliyekuwa maarufu zaidi duniani hadi anakufa 2009, alifika nchini akiwa balozi wa ziara ya Umoja wa Mataifa na akapokelewa kiserikali na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, hayati Hassan Diria.
Michael Jackson alitua jioni moja uwanja wa ndege wa Dar akiwa amevalia shati la kijani lenye mikono mirefu, suruali nyeusi na kofia nyeusi, akapandishwa kwenye Mercedes iliyompeleka hadi Kilimanjaro Hotel (wakati huo) ambayo baadaye ikawa Kilimanjaro Hotel Kempinsk, sasa ikiitwa Hyatt Regency Dar es Salaam.
Mashabiki waliokuwa na habari walijazana uwanja wa ndege Dar “kumkodolea mimacho” mwanamuziki huyo wakati huo akiwa na umri wa miaka 34 tu, mbali na wale waliomfuata hadi kwenye hoteli hiyo. Wakaungana na wale waliokuwa wakimsubiri hapo kumshangilia kwa mbinja na mayowe ya furaha.
Pia, mashabiki waliokuwa na habari za ujio na ratiba yake, walijitokeza kwa wingi na kumshangaa vilivyo, The Wacko Jacko alipotembelea shule hiyo ya Sinza, kesho yake.
Katika ziara yake hiyo ya siku mbili nchini, alikutana na mkuu wa nchi ambaye wakati huo alikuwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Ndivyo Michael Joseph Jackson alivyofika Tanzania na kushikana mikono na watoto wa Sinza miaka karibu 20 iliyopita!
No comments:
Post a Comment