Marehemu Steven Kanumba.
Khatimu Naheka na Wilbert MolandiMAREHEMU, Steven Kanumba, alikuwa shabiki wa klabu ya Simba na aliwahi kutengana na swahiba wake, Vincent Kigosi ‘Ray’ wakati wawili hao walipokwenda kuangalia mechi ya Yanga na Simba, imefahamika.
Ray ameliambia gazeti hili kuwa Kanumba hakuwa mpenzi sana wa soka lakini alikuwa akiipenda Simba. “Kuna siku nilienda naye Uwanja wa Taifa, akagoma kukaa kwenye jukwaa la Yanga nilipokuwa naenda kukaa, akaenda upande wa Simba.
Aidha, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema marehemu Kanumba kabla ya kufariki alikuwa na ndoto za kuwa mbunge.
Kanumba ambaye alifariki usiku wa kuamkia juzi kutoka na kile kinachoelezwa kutokea mkwaruzano wa kimapenzi kati yake na mwigizaji mwenzake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ nyumbani kwake Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, aliwahi kumueleza mbunge huyo juu ya mipango yake ya kuingia katika siasa.
Zitto ambaye alikuwa mmoja wa waombolezaji, alisema Kanumba aliwahi kumfuata na kumwomba ushauri juu ya kiu yake ya kutaka kugombea ubunge kupitia Jimbo la Shinyanga Mjini.
“Nakumbuka miezi michache iliyopita alinifuata na kuniambia anataka kuwa mbunge kupitia chama chetu cha Chadema, nilipanga wiki mbili zijazo ningemtafuta na kumpa kazi ya kufanya yale ya muhimu ili aweze kupata nafasi hiyo,” alisema Zitto.
Wakati huohuo, Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, jana alikuwa miongoni mwa waombolezaji wa msiba wa msanii huyo aliyezaliwa Januari 8, 1984, ambapo mbali na kuwapa pole wafiwa wote aliwataka wasanii kutoingilia uamuzi wa familia juu ya mazishi.
Mara baada ya kupata maelezo mafupi kutoka kamati ya mazishi inayoongozwa na Gabriel Mtitu, Rais Kikwete aliwaagiza wanakamati hao kutoingilia ndugu wa familia katika maamuzi ya mazishi na kuwataka wamjulishe mipango itakavyokuwa kupitia kwa mwanaye, Ridhiwani Kikwete aliyekuwepo eneo la tukio.
“Mara ya mwisho nilikutana naye (Kanumba) Dodoma, mwaka jana, ulipanga mikakati mingi ya kusaidia sanaa ya Tanzania na wasanii wenzake ili kuhakikisha wananeemeka na jasho lao.
“Kinachotakiwa kwa sasa ni kuifariji familia lakini yale niliyowaahidi kuyafanya nitayakamilisha, nasubiri majibu ya kazi niliyowatuma kina JB (Jacob Steven) ili nianze kazi ya utekelezaji haraka,” alisema Kikwete.
Msanii huyu ambaye ameshatoka filamu nyingi anatarajia kuzikwa kesho kwenye makaburi ya Kinondoni, Ataanza kuagwa kuanzia saa tatu asubuhi kwenye Viwanja vya Leaders Kinondoni.
Wakati huohuo, Klabu ya Yanga jana ilitoa Sh milioni moja kama rambirambi yao wakati baadhi ya wachezaji na viongozi walipokwenda nyumbani kwa msanii huyo.
No comments:
Post a Comment