My Web
Emmanuel
CONTACT
Monday, April 9, 2012
Wanaume Simba waifunika Dar
SIMBA ndiyo ina rekodi ya kuwa timu iliyowahi kupata mapokezi makubwa zaidi kuliko nyingine yoyote katika historia ya soka nchini.
Mwaka 2003, wakati Simba inarejea nchini (angalia picha hapo juu), mashabiki zaidi ya 100,000 walijitokeza mitaani kuipokea baada ya kuing’oa na kuivua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek ya Misri.
Ijumaa iliyopita, ikiwa ugenini imefungwa mabao 3-1, lakini imesonga mbele kwa faida ya bao la ugenini baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani.
Leo, wakali hao walitarajiwa kutua nchini saa 12 asubuhi kama mashujaa ikiwa ni baada ya kuwang’oa Waarabu, safari hii wa Algeria, ES Setif.
Mapokezi ya Simba, huenda yakawa gumzo na timu hiyo ikaongeza rekodi nyingine ya kupokewa na watu wengi ingawa inaonekana ile ya mwaka 2003 huenda isifikiwe, kwa kuwa Tanzania ipo kwenye msiba wa msanii maarufu wa filamu nchini, Steve Kanumba, anayezikwa kesho jijini Dar es Salaam.
Jana asubuhi, Simba walipanda ndege ya Egypt Air, wangepumzika Cairo, Misri kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, akizungumzia mapokezi hayo amesema, baada ya timu hiyo kutua majira ya saa 12:05, itaelekea kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Maestro alisema klabuni hapo wameandaa hafla fupi ya kuwapongeza wachezaji baada ya kutinga katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf).
“Baada ya kuwasili nchini, msafara mzima wa Simba utaelekea klabuni ambako tumeandaa hafla fupi ya kuwapongeza wachezaji wetu,” alisema Maestro.
Mashabiki wengi waliotuma ujumbe kwenye gazeti hili, walionyesha wamepania kwenda kuwapokea wachezaji wao huku zaidi wakitaka kumuona Emmanuel Okwi aliyefunga bao ‘noma’ lililoisongesha mbele timu hiyo.
Tayari, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ yupo nchini kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mapokezi hayo ya Simba ‘mla’ Setif.
Wakati huohuo, wachezaji Juma Kaseja na beki, Victor Costa, wameweka rekodi ya kuwa wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye kikosi kilichoing’oa Zamalek na leo wanatua jijini Dar wakiwa kwenye kikosi ‘kilichoimega’ ES Setif.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment