My Web

Emmanuel

CONTACT

Wednesday, April 11, 2012

KWA STEVEN KANUMBA HAITATOKEA TENA

Na Waandishi Wetu
JANA ilikuwa ni simanzi na majonzi kwa Watanzania wakati wa kutoa heshima zao za mwisho kwa mcheza sinema, marehemu Steven Kanumba ambaye alifariki dunia Aprili 7.
Kanumba aliagwa jana kwenye Viwanja vya Leaders Kinondoni jijini Dar es Salaam majira ya saa nne asubuhi na kushuhudiwa na waombolezaji akiwemo mgeni rasmi Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete.
Ni rahisi kusema kuwa haitatokea tena Tanzania kwa mtu kuagwa na watu wengi namna hii mbali na wale waliojitokeza katika kumuaga aliyekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hii, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia mwaka 1999.

Watu wengi
Watu walianza kujazana kwenye viwanja hivyo kuanzia saa moja kamili asubuhi na ilipofika majira ya saa mbili kulikuwa hakuna sehemu yoyote ya mtu kupita au kuegesha gari.

Mwili waingizwa viwanjani
Majira ya saa nne asubuhi mwili wa marehemu Kanumba uliingizwa uwanjani hapo na maelfu ya watu waliokuwa uwanjani hapo walianza kulia, huku wengine wakizimia na kukimbizwa katika sehemu za watu wa huduma ya kwanza.
Pamoja na kuwa kulikuwa na askari wengi lakini walizidiwa na kuanza kutumia nguvu ili kuwatawanya watu waliokuwa wamezuia njia. Hata hivyo, sehemu iliyokuwa imeandaliwa maalum kwa ajili ya wageni wa heshima nayo ilivamiwa na umati wa watu ikiwemo sehemu aliyokuwa amekaa mama mzazi wa Kanumba ambapo ilibidi ahamishwe.

Mama yake ashindwa kuaga
Baada ya wageni rasmi kumaliza kuaga, ilikuwa zamu ya mama yake Kanumba na wanafamilia lakini kabla hawajaanza kufanya hivyo, umati wa watu ulivamia lilipokuwa jeneza la mwili huo na hivyo ikawabidi walinzi wawazuie watu wasiendelee kumuaga marehemu, akiwemo mama yake.

Watu waambiwa wakasimame barabarani
Baada ya maelfu kushindwa kuaga walitakiwa waondoke kwenye viwanja hivyo na kwenda kujipanga barabarani ambapo wangeliona gari lenye mwili likipita, hivyo na watu wakaanza kukimbilia eneo la nje ya makaburi.

Makaburini watu wazimia kwa joto, uzio wavunjwa
Waombolezaji walizidi kuwa wengi kwenye makaburi na walipojaa ndani walizuiwa kuingia lakini wengine waliamua kuvunja uzio na kuingia ndani huku wake kwa waume wakiruka ukuta na kukanyaga makaburi. Baada ya hali hiyo askari waliongezwa na kuwa wengi zaidi lakini pia walizidiwa nguvu kwani watu walikuwa wengi sana.

Wasanii wasema ilitakiwa kuwa siku ya kuaga tu
Wasanii wengi waliokuwa hapo walisema leo ilitakiwa kuwa siku ya kuaga tu na iandaliwe siku nyingine ya mazishi kwa kuwa watu walikuwa ni wengi mno, lakini mwenyekiti wa kamati ya mazishi, Gabriel Mtitu, alisema hawakutegemea kuwa kutakuwa na idadi kubwa namna hiyo.

Mabasi yatoka Morogoro na Dodoma
Mabasi mengi yalionekana yakiwa na watu waliotoka Dodoma na wengine Morogoro ingawa wengi wao hawakupata nafasi ya kuuaga mwili huo.

Mwanamke anywa sumu, mwingine agoma kupika
Mwanamke mmoja kutoka Zanzibar ameripotiwa kuwa alikunywa sumu baada ya kusikia taarifa za kifo cha mcheza filamu huyo, wakati huko mkoani Mwanza mwingine aligoma kupika kwa siku tatu na kupewa talaka na mumewe kutokana na sababu hiyohiyo

No comments:

Post a Comment

New