My Web

Emmanuel

CONTACT

Thursday, April 12, 2012

Tume Ya Katiba: Mtihani Wa Pili Kitaifa Kwa Jaji Warioba

Na Maggid Mjengwa,
JAJI Mstaafu, Joseph Sinde Warioba, kwa mara ya pili katika historia ya nchi hii, amepewa na Rais aliye madarakani, Jakaya Mrisho Kikwete, heshima ya kutwishwa jukumu kubwa linaloweza, ama kubadili sura na mwelekeo wa taifa la Tanzania, au kuliacha taifa likiwa limenasa kwenye tope zito.
Ndio, Jaji Joseph Warioba amepewa jukumu zito la kuongoza Tume ya Kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Itakumbukwa, baada ya nchi kuzama katika vitendo vya rushwa huku viongozi wakiongoza katika kutenda dhambi hiyo,
Mwalimu Nyerere alimnadi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kama ’ Mr Clean’- Bwana Msafi. Na katika moja ya kauli zake, Mkapa alipata kutamka kuwa hatokuwa na suluhu na rushwa.
Na umma ukaingiwa na matumaini makubwa pale Mkapa alipomteua Jaji Joseph Sinde Warioba kuongoza Tume ya Kuchunguza mianya ya rushwa na kupendekeza njia ya kuiziba mianya hiyo. Jaji Warioba aliifanya kazi yake. Hata hivyo, ripoti ile ya Jaji Warioba ikaishia kukusanya vumbi kwenye makabati ya watendaji Serikalini.
Mapendekezo ya Ripoti ya Warioba hayakupata kufanyiwa kazi. Na ajabu ya kauli ya Mkapa ya kwamba hatokuwa na suluhu na rushwa, ni ukweli kuwa, leo yeye ni mmoja wa wanaotuhumiwa kutumia vibaya Ikulu ikiwamo kuanzisha kampuni binafsi akiwa kwenye uongozi wa nchi na kwa anuani ya Ikulu.

Hivyo, Jaji Warioba ana mtihani mgumu. Kwamba Tume yake ya Katiba itakuja na rasimu. Kuna wanayoyataka wananchi wengi yawemo kwenye Katiba mpya. Lakini, kuna kuna tofauti ya wanayoyataka wananchi na ambayo Serikali haiyataki hata kama haisemi kwa sauti kuwa haiyataki. Mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya utakuja kuthibitisha ninayoyaandika hapa. Ndipo hapo, Jaji Warioba na wajumbe wenzake wa Tume watakapokabiliwa na mtihani mgumu. Kuchagua ni upande gani wa kusimama, na kwa maslahi ya nani.

Na hakika, tulipofikia sasa, kikubwa kinachokosekana miongoni mwetu Watanzania ni IMANI. Mchakato mzima wa kudai Katiba Mpya, tangu ulivyoanza miaka ya 1990, ulitawaliwa na hali ya kutoaminiana. Hali ya kukosekana kwa imani ingalipo. Na kukosekana kwa imani kunachangiwa na hofu. Ni hofu ya walio kwenye mamlaka kupoteza mamlaka yao.

Hivyo basi, changamoto ya kwanza kabisa kwa Tume iliyoundwa ni kufanya kazi ya kuandaa rasimu ya Katiba itakayowarudishia imani Watanzania juu ya dhamira ya Serikali ya kutaka kuwepo kwa Katiba itakayoifanya Tanzania iwe nchi ya kisasa. Kwamba Katiba ichangie kwenye kuwarudishia imani Watanzania juu ya namna watakavyoendesha nchi yao.

Hakika, tatizo letu kubwa kwa sasa ni kukosekana kwa imani miongoni mwetu . Hatuaminiani. Ndio maana, Serikali nyingi Afrika hazipendi kuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi kwa vile hutoa nafasi kwa walio kwenye upinzani kuingia madarakani. Na kwa vile hawana imani nao , kwa maana ya wapinzani mara nao watakapoingia madarakani, basi, Serikali hizo huona ni vema kutokuwepo kwa Tume Huru za Uchaguzi. Hilo la mwisho linawabakishia matumaini ya kuendelea kubaki madarakani. Maana, anayeamua hatma ya uchaguzi si mpiga kura, bali muhesabu kura.

Kama Tume hii iliyoundwa itapendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi , basi, huo utakuwa ni mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi. Nahofia, Tume Huru ya Uchaguzi itasubiri mpaka tuchinjane kwanza kwa kutuhumiana kuibiana kura kwenye chaguzi. Tatizo ambalo lingeweza kumalizwa kwa kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoaminika na pande zote zinazoshiriki chaguzi. Itakayoaminika na wananchi.

Tukumbuke, kuwa imani ikikosekana hususan kwa vyama na wananchi dhidi ya Serikali katika kuandika Katiba hii, basi, kutaufanya mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya uwe ni wa gharama kubwa bila matunda tarajiwa kwa umma.

Kuna wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon alitamka; kuwa tatizo kubwa la Serikali nyingi si nakisi ya bajeti bali nakisi ya imani ya Wananchi kwa Serikali hizo. Ndio, kupungua kwa imani. Ndio, inahusu imani na ni wajibu wa Serikali na Chama cha Mapinduzi kuirudisha imani ya wananchi kwa Serikali na chama hicho.

Nimepata kuandika, kuwa nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi.

Watanzania wengi kwa sasa wana kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo.

Tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Kikwete itusaidie kutupitisha kwenye njia ya pili; Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa.

Na siku zote, nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi bila kuwa na utulivu wa kisiasa. Kuna dalili, huko twendako, hakutakuwa na utulivu wa kisiasa kama tutaicha hali hii ya sasa iendelee kama ilivyo. Hali ya kutoaminiana na kukosekana kwa muafaka wa kitaifa wa kisiasa.

Itakumbukwa mwaka jana kwenye hotuba ya Rais Kikwete ya kuzindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano- 2011 hadi 2016 Rais alitamka haya;
” Bila Utawala Bora , bila kuwa na demokrasia, bila kuheshimu Haki za Kibinadamu, mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana.”

Rais hakupigiwa makofi ya nguvu. Ndio, wengi wa viongozi waliokuwa wakimsikiliza Rais kwenye ukumbi ule wa Saint Gasper pale Dodoma ni Wana-CCM. Bila shaka kuna waliokuwa wakifikiria Ukuu wa Wilaya wao na Ukuu wao wa Mkoa. Walifikiria nyadhifa zao. Mambo ya kupanua demokrasia ikiwamo uwepo wa vyama vingi kwao ina tafsiri ya kutishia vibarua vyao!

Lakini, katika hicho alichotamka Rais ndipo palipokuwa na hoja ya msingi kabisa. Ni ukweli, kuwa wenzake na Kikwete walio wengi ndani ya CCM hawaamini kwa dhati katika demokrasia, hususan demokrasia ya vyama vingi.

Nimepata kuandika, kuwa kwa hili la rushwa na ufisadi, kuna wachache ndani ya CCM ambao Chama wamekigeuza kuwa ’ Shimo la Panya’- watoke wakatafune mali ya wananchi, kisha wakimbilie shimoni kwa maana ya kwenye chama. Na shimoni ndiko kwenye ’ kulindana’. Na hii ndio sababu ya msingi ya kupungua umaarufu kwa chama hicho tawala miongoni mwa Watanzania na hususan kundi kubwa la vijana.

Maana, ni ukweli, wengi wanaotuhumiwa kushiriki ufisadi wamo ndani ya Chama tawala . Ni wenye mahusiano mazuri au kama inavyosemwa siku hizi, ni ’ marafiki’ wa CCM. Naam , hivi ni vijipanya tu ni vyenye ’vijishimo vyao’ ndani ya CCM. Si tumepata kusikia ikitamkwa; ” Ukitaka biashara yako ikunyokee, njoo CCM!”

Na hapa ndipo inapokuja dhana yangu ya uwepo wa ubaguzi wa kisiasa katika nchi yetu. Ubaguzi huu wa mathalan, ’ Hawa ni wenzetu’ na ’ Wale ni maadui zetu’ umejengeka katika misingi ya kulindana katika maovu. Wenye kuendekeza ubaguzi huu ndio wenye kugombania fito wakati tunajenga nyumba moja.
Na Profesa wa Uchumi, Jeffrey Sachs ana mfano hai wa Poland. Katika kuwashauri kuinuka kiuchumi WaPoland wale , Profesa Sachs aliwaambia; ” Political power must be shared”. Kwamba kuna umuhimu wa vyama kuwa na utayari wa kugawana madaraka ya uongozi wa kisiasa.

Ndio, Fundi Umeme yule Lech Walensa wa chama cha wafanyakazi na aliyeanzisha vuguvugu la mapinduzi ya kujikomboa kutoka Ukomunisti aliambiwa na Profesa Jeffrey Sachs; ” Chama chako cha Solidarity kiwe radhi kuunda Serikali ya Mseto na Chama Cha Kikomunisti”. Na ikawa hivyo, kimoja kikatoa Waziri Mkuu na kingine Rais. Kukawepo utulivu wa kisiasa. Poland ikaanza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi. Ndio, hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa kisiasa. Katiba Mpya itakayohakikisha, mbali ya mambo ya mengine, inatupa Tume Huru Ya Uchaguzi. Nahitimisha

No comments:

Post a Comment

New