WENZI kuishi mbalimbali ni mtihani mkubwa kwa wengi. Jambo hilo linapotokea, fikra huhamia kwenye kuwapoteza wapenzi wao, kusalitiwa au kugombana. Kwa namna fulani, mawazo hayo huwa sahihi, lakini leo nitakupa mbinu.
Kama mtakumbuka vyema, wiki chache zilizopita niliwahi kuandika mada inayozungumzia faida za wapenzi kuishi mbalimbali, leo nitasogea mbele zaidi, nikilenga namna ya kuboresha uhusiano huo na kumfanya mwenzi asipate wazo la usaliti.
Tatizo hapa ni kukosa mbinu za kuboresha penzi, hapo ndiyo mwanzo wa kuchochea kuachana. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba wapenzi ambao wanaishi mbali mbali, kama wasipokuwa makini ni rahisi sana kuachana au kuwa na ugomvi ambao mwisho wake ni kutengana kuliko wale ambao wanaishi pamoja au eneo moja.
Waswahili wanasema, fimbo ya mbali haiui nyoka, hivyo ukitokea ugomvi mdogo, hasa ukizingatia kwamba wanaishi mbali inakuwa rahisi kwa mmoja wao kuamua kulipiza kisasi kwa kutoka na patna mwingine.
Katika mada hii, nitakupa njia mbadala za kuufanya uhusiano wako uendelee kuwa hai, pamoja na kwamba mnaishi mbali na mpenzi wako. Hebu twende pamoja.
MAWASILIANO
Kuwasiliana na mpenzi wako mara kwa mara kunatajwa kama njia mojawapo kati ya nyingi zinazoweza kukusogeza karibu zaidi na mwandani wako, hivyo kumfanya azidi kukupenda na kushindwa kukusahau.
Hata hivyo, wengi hushindwa kujua aina ya mawasiliano na jinsi ya kutumia ili kuteka akili za wapenzi wao na kuwafanya waendelee nao siku zote za maisha yao, pamoja na kwamba wapo mbali nao.
Hapa chini ni vijisehemu vichache ambavyo vinaainisha mambo ambayo ukiyazingatia, utaendelea kuulinda uhusiano wako hata kama mwenzi wako yupo mbali.
(i) Barua pepe
Njia hii ya mawasiliano kwa wapenzi walio mbali ni nzuri sana. Hata hivyo inategemea mpenzi wako yupo wapi, maana kuna maeneo mengine yanakuwa hayana huduma za Mtandao wa Intaneti.
Kutokana na kukua kwa Teknolojia, wengi humiliki kompyuta za mikononi (lap top) ambazo huwarahisishia mawasiliano ya moja kwa moja na watu wengi. Kama mpenzi wako ni mmoja wao, hii ni nafasi nzuri sana kwako.
Mtumie kadi nzuri zenye ujumbe mwanana wa mapenzi kwa ajili ya kuhamasisha penzi. Mwandikie tungo za mapenzi ukionesha ubunifu wako. Pia waweza kumtumia vichekesho kwa ajili ya kumburudisha na kumfanya mwenye furaha.
Haya unaweza kufanya kwa wingi kadri uwezavyo na kwa nafasi yako, huku ukizingatia upatikanaji wa huduma hiyo na uwezo wa kumudu gharama. Kadhalika unapaswa kuzingatia uwiano wa kumfikia mpenzi wako.
Hapa namaanisha kwamba kama anamiliki lap top yake ni rahisi zaidi maana unaweza kumtumia nyingi kadiri uwezavyo, lakini kama ni wa kwenda Internet Cafe mara moja kwa wiki, basi unapaswa kumtumia mara moja kwa wiki. Umenipata?
(ii) Simu
Kuwasiliana kwa njia ya simu za mkononi ni moja kati ya njia bora za mawasiliano na kuboresha uhusiano wa wapenzi. Mwenzi wako anapokuwa mbali na wewe, kwa kutumia njia hii, unaweza kumsogeza karibu yako na kufurahia sana uwepo wako, ingawa upo naye mbali.
Epuka neno ‘habari yako?’ baada ya kumpigia simu. Lazima kauli yako iwe laini, uzungumze naye kwa unyenyekevu na kumtia hamasa ya kuzidi kuzungumza na wewe. Kadhalika unapomwandikia meseji, kaa chini na utunge, siyo unamwandikia ‘sema mwenzangu, uko poa? Umeshakula?’ Hii ni meseji mbaya kwani haina hamasa yoyote ya kimahaba.
Unapaswa kumtumia sms za mapenzi, tungo za mahaba, maneno ya utani, vichekesho na kejeli. Hivi ni kati ya vitu vya kufurahisha ambavyo kwa hakika vikifanywa, humfanya mwenzi wako kuwa na hofu ya kukusaliti.
Unaweza kumtumia meseji nyingi kadiri uwezavyo kulingana na uwezo wako wa kifedha, ingawa mitandao mingi ya simu za mikononi siku hizi huwa na ofa maalumu ya kutuma sms nyingi kwa gharama ya chini. Unaweza kujisajili kila siku kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na mpenzi wako.
Pamoja na kwamba uwezo wako kifedha, muda na majukumu vinaweza kukufanya uamue idadi ya meseji utakazomtumia mpenzi wako, lakini ni lazima umtumie angalau meseji tano kwa siku.
Meseji hizo hutumwa kwa muda maalum, mathalani baada ya kuamka asubuhi unapaswa kumtumia ujumbe mzuri, uliojaa mashairi na tungo za mapenzi, ukimtakia asubuhi njema na mafanikio katika kazi zake za kutwa hiyo.
Mchana, mtakie mlo mwema na kazi njema, alasiri mtumie ujumbe wa kichekesho. Usiku, mtumie ujumbe wa kumpa pole kwa kazi, kisha malizia kwa kumtumia ujumbe mwanana wakati wa kulala.
Kama nilivyoeleza awali, unaweza kutuma meseji nyingi zaidi kulingana na uwezo wako na muda huku ukizingatia majukumu yako ya kazi.
Inawezekana mwenzi wako huko alipo, ana kazi nyingi na ratiba zake zinambana sana, kama ndivyo unapaswa kuhakikisha humtumii meseji nyingi sana, kwani unaweza kumkera kwa milio ya simu kila wakati, muda ambao yeye hutumia kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuboresha maisha yenu ya baadaye.
Ni vyema kuangalia sana ratiba yake ya mchana, kwa suala la kumpigia simu na kumwandikia meseji. Unaweza kumpigia simu angalau mara mbili kwa siku, kisha baada ya hapo ukamwachia muda wa kufanya kazi, kwani si busara kumsumbua sana anapokuwa ana majukumu kazini.
Usiku ni muda mzuri kwako ‘kumlinda’ mpenzi wako. Zungumza naye kwa sauti laini ambayo inaweza kuamsha hisia zenu na kujikuta kila mmoja akiwa anaridhika kwa kusikia tu sauti ya mwenzi wake.
Haya ni mambo yanayowezekana na kwa hakika kama ukijaribu utaona mafanikio yake makubwa. Inawezekana, jaribu utaona.