Mambo muhimu ya kijana ya kujikomboa kimaisha sehemu ya 4
Je, tunazitumia kazi tulizopata kwa moyo au tunafanya uzembe, tunaiba na kunyanyasa watu? Tulitafuta gari tukapata, tunalitumiaje gari hilo, je ni kama gesti ya kufanyia uhuni na wake za watu au ni kwa ajili ya kutusaidia katika shida za usafiri? Ni lazima tujifunze na kujua namna ya kutumia vema vitu tunavyopata ili tuweze kupata mafanikio.
Kimsingi kutafuta pekee hakuwezi kubadilisha maisha ya vijana kama vitu vinavyopatikani havitumiwi kwa nidhamu.
TUNAVYOPOTEZA
Watu wengi wanatafuta vitu na kupata, lakini kuna jambo moja kubwa ambalo limekuwa likiwatokea nalo ni kupoteza walivyopata. Wapo waliotafuta kazi, fedha, nyumba, magari, wakapata lakini leo tunaposoma somo hili kupata kwao kumebaki historia.
“Khaa! Huyu usimuone hivi amesoma sana, sema tu alipata matatizo. Jamaa alikuwa na maisha mazuri sana lakini ilitokea bahati mbaya akafilisika. ”Hizi ni baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikitolewa kuwahusu watu waliopata vitu fulani, lakini wakavipoteza.
Kupoteza yaliyopatikana kuna sababu kuu mbili, nazo ni kupoteza kusikotarajiwa na kupoteza kwa matarajio. Ninaposema kusikokuwa na matarajio ninamaanisha majanga ambayo huwakuta watu bila wao wenyewe kuzembea mahali popote. Kwa mfano ukame, kimbunga, wizi, ajali na kadhalika.
Ninapozungumzia kupoteza kwa matarajio ninamaanisha matukio yanayotokana na kuwepo kwa uzembe wa mtu mwenyewe katika kusimamia mambo aliyoyapata. Kwa mfano kupata utajiri na kuanza kufuja fedha kwa anasa, kuhonga, kutozingatia kanuni za kupata kingi na kutumia kichache na mambo kama hayo ni moja kati ya sababu za kizembe ambazo huwafanya vijana kama si watu wengi kupoteza walivyopata.
Lakini pamoja na kuwepo kwa sababu hizo mbili za kupoteza, wataalamu wanasema watu wengi wanaotokewa na tatizo hili wanatoka katika kundi la pili, yaani wanaopoteza kwa makusudi.
Uchunguzi unaonesha kuwa asilimia 91 ya wanaopoteza vitu walivyovipata wanajitakia, lakini ni asilimia 4.5 kati yao ndiyo wanaotambua baadaye kuwa kupoteza kwao kulitokana na wao wenyewe na asilimia zilizobaki huhifadhi makosa yao kwenye sababu ya kwanza yaani kupoteza kusikotarajiwa.
Hii ina maana kuwa, ni watu wachache sana ambao wanatafuta na kupata kisha kupoteza na hatimaye kutafuta tena kwa mara ya pili na kupata pengine zaidi ya walivyopata mwanzo. Lakini wengi wao kama tulivyoona wakipoteza hushindwa kutafuta tena na kujikuta wakizama kwenye hali mbaya mpaka wanakufa au kujikuta wakipata vitu dhaifu sana.
Ni vema wakati tunatafakari hili, tukajiuliza ni watu wangapi ambao tunawafahamu, walifukuzwa kazi, wakahangaika kupitia uzoefu na uwezo wao kupata kazi nyingine nzuri zaidi ya zile walizokuwa nao?
Je, ni watu wangapi ambao biashara zao zikifilisika huanza mwanzo kutafuta mtaji na kufanikiwa kurudisha maduka yao kwa ukubwa ule ule au zaidi?
Ni wangapi ambao, walipoteza wapenzi, wake/waume na hatimaye kupata wengine wazuri kiasi cha kusema wamepata bora kuliko wa kwanza? Bila shaka watakuwepo, lakini haiwezi kuwa idadi ya kuzidi asilimia 4.5 niliyoitaja hapo juu.
Kama hali iko hivi ni wazi kwamba vijana wengi hawafahamu kanuni ya kutafuta baada ya kupoteza. Kwa kuwa hawafahamu hilo wengi wao wamejikuta wakifanya makosa na kuambulia madhara makubwa likiwemo suala la kukata tamaa ya kufanikiwa kimaisha.
No comments:
Post a Comment