mwisho wa GADDAFI
Mwandishi Wetu na intaneti
Wanajeshi wa Serikali ya Baraza la Mpito la Libya (NTC), walitamba wakishangilia, wakati asilimia kubwa ya raia walizizima kwa vilio juzi (Alhamisi) baada ya kupokea taarifa kwamba Muammar Gaddafi amefariki dunia.
Gaddafi aliyeiongoza Libya kwa zaidi ya miongo minne, enzi yake ilifika mwisho baada ya kuuawa na wapiganaji wa NTC kwenye jiji alilozaliwa la Sirte, Libya.
Habari zinasema kuwa wapiganaji wa NTC walimshambulia Gaddafi miguuni, hivyo kumfanya ashindwe kukimbia kabla ya ‘kumshuti’ na kummaliza kabisa.
Waziri wa Habari wa NTC, Mahmoud Shammam alithibitisha kuuawa kwa Gaddafi aliyeanza kuitawala Libya kuanzia mwaka 1969 kabla ya utawala wake kuangushwa mwaka huu.
Hata hivyo, picha za awali zilizotolewa zikimuonesha kiongozi huyo akiwa amefariki dunia, zilikosolewa kwa maelezo kwamba zilitengenezwa kwa lengo la kuuzuga ulimwengu.
Ubishi uliisha baada ya kutolewa kwa video inayowaonesha wapiganaji wa NTC wakiuburuza barabarani mwili wa Gaddafi uliokuwa umejaa damu huku wakimpiga na kumdhihaki.
Kutokana na hilo, wanaharakati wa haki za binadamu wamevishutumu vikosi vya NTC kwa kitendo cha kuuzungusha mwili wa Gaddafi barabarani na kumpiga.
Kwa mujibu wa NTC, yalitokea mapigano makali kati ya wapiganaji waliokuwa wanamlinda Gaddafi dhidi ya wanajeshi wa baraza hilo la mpito.
NI ZAIDI YA MATESO
Video zinazomuonesha Gaddafi baada ya kuuawa, zinaonesha jinsi kiongozi huyo wa zamani wa Libya alivyokumbwa na mateso makali katika saa za mwisho za uhai wake.
Katika moja ya video, wapiganaji wa NTC walionekana wakiuchanachana mwili wa Gaddafi, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na wanaharakati wa haki za binadamu.
Baadhi ya wananchi wa Libya hasa Waislamu, baada ya hali kuchafuka juzi kutokana na kifo cha mtawala wao wa zamani, walijumuika misikitini na kusali kumuombea apumzike kwa amani.
Walisema kuwa kwa mateso ambayo wapiganaji wa NTC walimpa Gaddafi, ni afadhali sasa apumzike na Mungu atamkadiria yale aliyotenda duniani kama yanafaa kumpeleka peponi au motoni.
YALIYOMSIBU SAA 24 KABLA YA KIFO
Baada ya Gaddafi kuuawa, NTC walifanikiwa kumtia nguvuni mmoja wa watoto wake wa kiume ambaye hata hivyo hawakumtaja jina.
Imeelezwa kuwa mtoto huyo aliwaambia wapiganaji wa NTC kwamba 24 kabla ya kifo cha Gaddafi, alikuwa akisumbuliwa na mawazo ya kutenganishwa na familia yake ingawa hakujua kama na kifo kimemkariba.
Habari zinaeleza kuwa Gaddafi alishachoka kupambana lakini alikuwa haelewi hatima yake ni nini ndiyo maana alibakiza wafuasi wachache wa kumlinda.
Ilielezwa pia kuwa katika kipindi cha saa hizo, alikuwa akionesha dalili za kufika mwisho wa maisha yake ya hapa duniani.
Ilifika wakati alikuwa akishindwa kula kama zamani, muda mwingi akionesha kukata tamaa, kumbe wapiganaji wa NTC walishamkaribia.
No comments:
Post a Comment