Umekata tamaa? tiba hii hapa.
KUPANDA na kushuka ni hali ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Siku zote dira ya kuishi inapatikana katika kanuni hii inayoacha giza la maisha ya kesho.
Pamoja na kuwepo kwa mambo hayo mawili katika maisha yetu, imebainika kuwa kukosa limekuwa ni jambo baya linalokatisha tamaa watu wengi. Ingawa kukosa ndiyo njia sahihi ya mwandamu kujifunza, lakini si wote wanaopenda kujielemisha kupitia kwayo.
Kukosa, limekuwa ni suala la aibu na lenye kukatisha tamaa ya kuendelea kuishi. Si wasomi wengi wanaofurahia kushindwa mitihani yao na wachache kati ya watafuta kazi wanaoridhika na majibu ya HAPA HAKUNA KAZI, pindi wanaposaka ajira.
Bila shaka hii ni changamoto kubwa katika maisha ya wengi, machozi ya wanadamu yanadondoka chini pale suala la kushindwa kufanikiwa katika jambo fulani linapotokea. Wasiopata usingizi na wanyonge wa kauli wanatoka katika makundi ya waliojaribu mara nyingi kupata wachumba, kutafuta kazi, kufanya biashara, kutafuta utajiri, kulima na kujikuta wakipata jibu la kukosa.
Mpaka sasa tafiti zinaonyesha kuwa, dunia imepoteza watu wengi kwa sababu ya ukataji tamaa, hii ina maana kwamba, wengi hatufahamu mantiki ya kukosa katika harakati za maisha yetu. Lakini ukweli unabaki kuwa mafanikio hayana maana kama kutofanikiwa hakutakuwepo.
Mara nyingi mafanikio makubwa ya kimaisha hutokana na kushindwa. Watoto wanapoanza kutambaa au kutembea huanguka na kuumia, lakini kwao si apizo la kutorudia tena kupiga hatua, bali ni zingatio la umakini zaidi juu ya nguvu na mbinu za kutembea bila kudondoka wakati ujao. Hivi ndivyo inavyompasa mwanadamu anayetafuta na kukosa, yaani ajaribu mara nyingi na asikate tamaa.
Lakini kwa kuwa ukataji tamaa mara nyingine si kitu cha kupenda na hasa linapokuja suala la kuzama kwa matumaini yaliyokusudiwa na mhusika, ndiyo maana nimeona ni muhimu kuandika mbinu kadhaa za kumsaidia mtu aliyejaribu na kujikuta katika hali ya kukata tamaa.
KWANZA: Jifunze kuwa mtu mwenye kutegemea mafanikio bila kujali kama una kitu au huna. Ukilala na kuamka itazame kesho kuwa ndiyo siku ya kufanikiwa kwako. Usikubali kuwa na mtazamo wa kutofanikiwa, kwani mawazo ya aina hiyo yatakuondolea ujasiri wa kujaribu na kujikuta unazidi kudidimia katika matatizo. Kumbuka waliofanikiwa si miungu ni watu kama wewe!
PILI: Ukikabiliwa na mawazo ya kukosa jipe muda wa kupumzika, kwa kusikiliza muziki na nyimbo uzipendazo. Fanya mazoezi ya viungo na utembelee sehemu zinazokuvutia, ukifanya hivyo utaiongezea akili yako nguvu ya kufikiri vema na kupunguza uwezekano wa mawazo ya kukata tamaa kukua na kukunyonya nguvu za kujaribu tena.
TATU: Zungumza na rafiki zako mara kwa mara juu ya yale ambayo unaona hayaendi sawa. Usiwe mtu mwenye kukaa peke yako chumbani, kwani utaipa uhuru mkubwa akiri kupembua na kuzalisha mawazo hasi mengi ambayo yatazidi kulikuza tatizo lako. Waswahili husema; akili isiyo na mawazo toka nje ni nyumba ya shetani.
NNE: Kaa chini na ufikiri zaidi kwa nini hukufanikiwa ulipojaribu.
lengo la kufanya hivyo lisiwe katika kujihukumu, bali kukusanya nguvu zaidi za kujaribu kwa mara nyingine. Ikiwa ulifeli mtihani, jiulize ni kwa kiwango gani ulisoma, ili kama kuna mahali hukujituma, wakati mwingine uongeze bidii.
TANO: Jiamini mwenyewe na usifikie hatua ya kujihukumu na kujiona hufai miongoni mwa jamii. Usijilinganishe sana na waliokuzidi kimaisha na kutamani kuwa kama wao kwa tukio la mvumo kama kulala masikini kuamka tajiri. Usipojiamini na kujipenda mwenyewe huwezi kufanikiwa kabisa. Fahamu wewe ni bora kuliko yule unayemuona mbele yako.
SITA: Kumbuka kuwa tunajifunza kutokana na makosa, kwa maana hiyo ukiona umeshindwa kufikia malengo, tambua kuwa umejifunza siyo kwamba umekwama. Katika kushindwa zidi kupata ujuzi na kujisahihisha. Ukizingatia hayo utajikuta kesho ya furaha inakuja mbele yako.
No comments:
Post a Comment