Polisi yatakiwa kutenga fungu kuhudumia watuhumiwa wagonjwa
Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuweka utaratibu au kutenga fungu ambalo litatumiwa na jeshi hilo kwa ajili ya kuwahudumia watuhumiwa ambao wanaumizwa, kuugua au kupata matatizo ya kiafya wakiwa mikononi mwa Polisi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na na jeshi la polisi jana wito huo umetolewa na maafisa wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja walipozungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Shamsi Vuai
Kwa mujibu wa taarifa hiyo askari hao “wamesema kuwa mara nyingi hulazimika kuwalipia watuhumiwa matibabu kutoka mifukoni mwao ama kurudi nao vituoni patipo matibabu kama aliyempeleka hakuwa na fedha mfukoni jambo ambalo wamesema ni hatari kwao na kashfa kwa Jeshi zima pale mtuhumiwa anapofariki akiwa katika kituo cha Polisi” imesema taarifa hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Mh. Nahodha amesema atalifuatilia suala hilo ili kupata ufumbuzi lakini anachojua ni kwamba jukumu la kuwatibu watuhumiwa ni la wizara ya Afya kwa vile Jeshi la Polisi halina mafungu kwa ajili ya matibabu kwa watuhumiwa. Mh. Nahodha pia ametoa onyo kwa viongozi wa mamlaka za Viwanja vya Ndege na Bandari kutowazuia Askari Polisi kufanya kazi zao ipasavyo kwa visingizio vyovyote kwani pamoja na kuwa maeneo hayo yapo chini ya mamlaka husika, lakini Polisi ndiyo wenye wajubu mkubwa wa kuhakikisha Ulinzi na usalama katika maeneo hayo.
Amewataka viongozi wa maeneo hayo kutowa ushirikiano kwa Askari Polisi na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama katika maeneo hayo ili kutekeleza majukumu yao kwa taifa pasipo kuwawekea mipaka lakini amesema ushirikiano huo ulenge katika kazi tu na sio katika njia za kujinufaisha binafsi.
Awali akitoa taarifa kwa Mh. Nahodha, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa pamoja na Polisi kudhibiti vitendo vya uhalifu kwa kiasi kikubwa, lakini mkoa huo unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo la ufinyu wa bajeti usiokithi mahitaji yaliyopo kiusalama.
Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amesema mpango wa Polisi Jamii ukishamiri utapunguza mlundikano wa kesi na watuhumiwa katika vituo vya Polisi na kwenye Magereza yetu kwani amesema uhalifu utadhibitiwa mapema mitaani kabla ya kufikishwa Polisi.
Kamishna Mussa amesema anaamini kuwa mpango wa Polisi Jamii ni ufumbuzi wa kukomesha uhalifu nchini na kwamba kama utapata msukumo ikiwa ni pamoja na wananchi kupewa elimu ya kutosha juu ya mpango huo, utaleta ufanisi katika mradi mpya wa Jeshi la Polisi wa utekelezaji wa Utii wa Sheria pasipo shuruti.
No comments:
Post a Comment