My Web

Emmanuel

CONTACT

Tuesday, October 18, 2011

mambo muhimu ya kufanya ili kijana ajikomboe kimaisha sehemu ya 3

SINA shaka kuna watu wametafuta sana elimu, kazi, biashara, wachumba, watoto, uongozi na mambo mengine mengi waliyoyahitaji katika maisha yao na kwa kiwango chao wamepata. Lakini tathmini inaonesha kuwa, asilimia 87 ya watu waliopata walivyokuwa wanatafuta hawanufaiki navyo au kwa lugha nyingine kupata kwao hakukuwasaidia.

Mamia kwa mamia ya vijana wametumia au wanatumia mpaka sasa karibu nusu ya maisha yao kutafuta elimu, lakini wanapoipata haiwasaidii wao kama watafutaji, haiwanufaishi wazazi na walezi na haina tija pia hata kwa taifa lao.

Huo ni mfano mmoja, lakini wapo watu wanaotumia muda mwingi kutafuta wasichana wazuri wa kuoa, wanatumia muda mwingi kutafuta fedha, wanajituma kupita katika maofisi na vyeti vyao asubuhi na jioni kutafuta kazi, wakiamini kuwa wakipata wanavyotafuta watanufaika.

Lakini kupata kunapotokea ni wachache wanaoonesha mabadiliko waliyotarajia wao wenyewe au jamii walizotoka na wanazoishi!

Ni mara ngapi tumeshuhudia wasomi wakifanya mambo ya ovyo pamoja na elimu zao? Au hatuwaoni watu wanachezea ajira kwa kutojali sheria za kazi, kuwa wazembe, wezi na hata mafisadi?

Hii ina maana kwamba, vijana wengi walipozaliwa walifundishwa na wazazi wao kutafuta, ndiyo maana hakuna asiyejua njia za kutafuta na uthibitisho wa hili upo kwenye shughuli wanazojishughulisha nazo.

Watoto wa wakulima wanajua kutafuta maisha kupitia kilimo, kwao ili kupata maisha ni kuwa hodari wa kushika jembe, kwa nini? Walifundishwa na wazazi wao tangu utotoni kutafuta kwa njia ya kilimo. Vivyo hivyo kwa wazazi wafanyabiashara, wasomi na hata viongozi.

Kumbe tatizo la vijana wa leo si la kujua njia za kutafuta na kupata mahitaji yao tu bali ni pamoja na kuelewa namna ya kutumia vizuri vitu wanavyopata. Ni lazima vijana wajue namna ya kutumia fedha wanazopata bila kujali ni nyingi kiasi gani. Inawezekana nikisema kutumia fedha anazopata kuna wanaoweza kudhani nazungumzia mamilioni na hivyo wao wenye kipato cha shilingi 10,000 somo hili haliwahusu.

Kimsingi kanuni sahihi ya matumizi ya fedha yoyote duniani, ili iweze kuleta mafanikio kwa mtumiaji bila kujali kiwango, ni INGIZA PESA NYINGI TUMIA CHACHE. Kwa bahati mbaya elimu hii vijana wengi hawapewi na wazazi wao, kwa maana hiyo hawajui namna ya kutumia vizuri fedha wanazopata na hapo ndipo wanapokutana na tatizo la mshahara hautoshi.

Mbali na suala la fedha, vijana wengi kama nilivyosema hawafahamu namna ya kutumia vitu wanavyovitafuta na kuvipata. Leo tuna vijana wengi wanaoa, lakini hawajui kuwatumia wake zao, matokeo yake wanajikuta wakivutwa na tamaa za kwenda kwa wanawake wengine na kuangukia magonjwa, fumanizi au vishawishi vya kufanya mabadiliko ya wapenzi waliowachagua mwanzo.

Yote hayo yanatokana na kutojua namna ya kutumia vitu, maana haijapata kutokea mtu akatosheka na anachopata, isipokuwa awe na elimu inayomuwezesha kutambua matumizi sahihi ya vitu anavyojikusanyia maishani mwake.

Kwa msingi huo naamini kila anayesoma mada hii, ana vitu anavyomiliki, inaweza kuwa elimu, kazi, ujuzi, biashara, mali, nyumba, watoto, mke, mume na hata dini, lakini shaka yangu inabaki kwenye matumizi sahihi.

Hebu tujiulize, tunazitumia vema dini zetu, tunawatumia vizuri waume zetu baada ya kuoana nao, tunawalea sawa sawa watoto tuliowatafuta kwa miaka mingi?

No comments:

Post a Comment

New