NI siku nyingine tena tunakutana katika safu yetu bora ambayo inazungumzia mambo ya mapenzi. Inapanua uelewa na kujenga kujiamini zaidi katika uwanja wa mapenzi. Wengi wamenufaika kupitia hapa.
Ndoa nyingi zilizopoteza muelekeo zimekaa sawa baada ya kusoma ukurasa huu. Kadhalika kuna vijana wengi ambao wamefanya maamuzi sahihi na kuoa/kuolewa na wenzi sahihi baada ya kupata muongozo hapa.
Naam! Ni kisima cha ujuzi wa mambo ya mapenzi. Mada inayoendelea ni kama inavyosomeka hapo juu. Tupo katika juma la pili la kuangalia ni wapi hasa mwanamke bora anapopatikana.
Wiki iliyopita tulianza kwa kuona faida na hasara za mwanamke wa kijijini. Pia tulianza kuona faida za mwanamke wa mjini. Leo tuanze na kuona hasara za mwanamke wa mjini kabla ya kusonga mbele zaidi.
HASARA
Inaelezwa kwamba wanawake wa mijini, hutumia vibaya utandawazi na hujikuta wameharibika na hivyo kuwa na tabia chafu. Mitandano ya simu za mikononi na intaneti zinatajwa kama vyombo vinavyotumiwa na baadhi ya wanawake hao kufanya ufuska.
Ni wanawake wa gharama sana, wanapenda kutolewa ‘out’, disko na kumbi mbalimbali za burudani kila mwisho wa wiki. Kama akizoeshwa ndiyo huwa hatari zaidi, kwani siku asipotolewa, huwa ugomvi mkubwa, maana ameshachukulia kama sehemu ya maisha yao ya kimapenzi.
Wakati mwingine ni wabishi, wanaweka fedha mbele, wakiamini fedha ni kila kitu katika mapenzi. Baadhi yao huwa na wanaume kwa ajili ya kujipatia fedha tu, na siyo ajabu siku fedha ikiisha ikawa ndiyo mwisho wa mapenzi.
Mara nyingi wanawake hawa wamezoea maisha mepesi, siyo rahisi sana kukabiliana na mikikimikiki ya maisha. Kwa maneno mengine, huwa hawawezi kuishi katika mazingira ya shida au mabadiliko ya mazingira.
Tatizo lingine kwa wanawake hawa ni mavazi yao, mara nyingi hayana staha na hata kama ukimweleza juu ya hilo, huwa mgumu sana kubadilika.
Siyo werevu wa kukabiliana na vishawishi (hasa waliopo maofisini). Ni wepesi sana kushawishiwa kwa ahadi ndogo ndogo au mvuto wa kimahaba wa wanaume watanashati. Kama hutakuwa makini na mwanamke huyu, unaweza kuwa kwenye foleni ya mapenzi bila kujua.
Ni mjanja sana wa kutengeneza mambo, anaweza kuwa amefanya kitu, lakini akakudanganya kwamba hajafanya, hata kama ni kwa kutoa machozi! Huyu ni mkali wa kufanya usanii na usishtukie kirahisi.
Kwa uchache tu, hizo ndiyo hasara za kuwa na mwanamke huyu wa mjini. Hata hivyo, usisahau kwamba, siyo kila mwanamke anaweza kuwa na tabia nilizoanisha hapo juu. Wengine wana baadhi, zaidi au pungufu lakini kwa wastani wengi wana tabia hizo.
Sina shaka sasa, umeanza kuelewa japo kidogo sana kuhusu wanawake hawa wanaoishi katika mazingira tofauti. Swali la msingi sasa ni je, nani kati ya hawa anaweza kuwa mke bora zaidi ya mwenzake?
Je, kuna ukweli kwamba wanawake wa kijijini wakiolewa na wanaume wa mjini hubadilika? Je, mwanaume wa kijijini anaweza kuoa mjini na kumchukua mwanamke huyo kwenda kuishi naye kijijini? Tuendelee kuona.
VIPI MAZINGIRA?
Wengi wanaamini wanawake wa vijijini wana mapenzi ya kweli, wazuri, wakarimu na wenye sifa zote nzuri za kuwa wake bora, lakini wakiolewa na kupelekwa mjini hubadilika! Sababu ambazo zinatajwa kusababisha kubadilika huku ni pamoja na kuathiriwa na mazingira.
Inaelezwa kuwa, msichana ambaye amekulia kijijini ambapo hakuna mambo mengi kama mjini, akifika mjini anabadilishwa na mazingira. Hili siyo la kweli. Sikatai kwamba hakuna wanawake ambao wakifika mjini wanabadilika, lakini nataka kukuambia kwamba,
kinachombadilisha siyo mazingira bali tabia yake.
Kama mwanamke ana tabia chafu, hata akiwa kijijini anaweza kuendelea na uchafu wake vizuri sana. Lakini tunapotizama suala la mazingira, siku hizi za Sayansi ya Teknolojia, kuna vitu vingi sana vipo vijijini.
Nishati ya umeme, mawasiliano yameondoa matabaka yaliyokuwepo zamani, angalau kwa kiasi kidogo, hivyo mwanamke wa kijijini hatakuwa na mageni sana atakapoenda mjini.
Kama umeamua kuoa kijijini na kumchukua mkeo huyo kwenda naye mjini, ni vizuri sana kumwangalia kwa karibu, mweleweshe mji ulivyo, mtahadharishe na walaghai, mwambie jinsi unavyompenda na ulivyomuona wa thamani.
Mtake aithamini thamani hiyo kwa kumchagua yeye, mambo haya na mengine yanayofanana na hayo yanaweza kumbabadilisha mwanamke wako na kuwa mwenye heshima na asiyebabaishwa na mabadiliko hayo.
Kubwa zaidi ni vyema kama utapata muda wa kuzungumza naye kabla ya kumpeleka mjini, yaani picha nzima ya maisha ya mjini awe nayo kabla ya kufika mjini, hii nayo inaweza kumsaidia na kumfanya aishi kwa umakini bila kushawishika.
Kumbuka kwamba, makosa mengi yanayofanywa na wanawake ni kwa sababu ya kuhadaiwa, sasa kama utakuwa umeshamfumbua macho mapema, siyo rahisi kudanganyika!
Mada bado inaendelea, wiki ijayo nitakuja kumalizia sehemu ya mwisho, USIKOSE!
No comments:
Post a Comment