Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
NI kama msemo wa kutesa kwa zamu, kwani baada ya utawala wa watumishi kadhaa wa kiroho, sasa upepo umegeuka kwa Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Maombezi, Nabii Flora Peter.
Nabii Flora ambaye kanisa lake lipo Mbezi Beach, Dar es Salaam, anatajwa kuwa malkia wa miujiza kutokana na neno lake pamoja na mafuta anayotumia kuponya watu wenye maradhi na matatizo mbalimbali.
Uwazi limeelezwa kuwa watu wengi wanamiminika kwa Nabii Flora kupata tiba kwa sababu hutumia mafuta aliyoyaombea ambayo akimrushia muumini wake, hupona maradhi, mikosi na matatizo yote yenye mkono wa Shetani.
Waandishi wa gazeti hili wamefuatilia maombezi yanayofanywa na nabii huyo kwa wiki mbili sasa, waligundua kuwa mafuta yanayotumika ni ya mzaituni kutoka Israel na Nabii Flora huyaweka kwenye kisahani kabla ya kuanza kuwapaka au kuwamwagia watu wenye matatizo.
HUPONYA UKIMWI, UTASA, KISUKARI
Baadhi ya watu waliodai kuwa na maambukizi ya ukimwi walipanda juu ya madhabahu kanisani hapo na kusema kuwa wamepona, hali iliyofanya waumini wengine kushangilia.
Mmoja wa watu hao ni Mosi Suleiman, Mkazi wa Ukonga Majumbasita, alitoa ushuhuda kuwa alikuwa na ugonjwa huo tangu 2006 lakini Mei 5, mwaka huu alijiunga katika kanisa hilo na kushuhudia mbele ya umati wiki iliyopita kuwa amepona.
Aidha, mwanamke mmoja, Ruth Ezekiel ambaye alidai alikuwa na matatizo ya kizazi kwa muda mrefu na kuondolewa katika Hospitali ya Dar Group alisema baada ya kuombewa na nabii huyo, sasa ni mjamzito na anashangazwa na hilo.
Mwingine ambaye alitoa ushuhuda ni mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Tatu Mohamed, mkazi wa Magomeni Mapipa, Dar aliyedai kuwa alikuwa na ujauzito kwa miaka mitatu lakini baada ya maombezi ya mama huyo na kupakwa mafuta, alijifungua salama.
Naye Suleiman Mohammed aliyedai kuwa alikuwa na uvimbe kwenye mgongo kwa miaka 26, lakini baada ya kuombewa umetoweka na kuanzia siku hiyo ameamua kusali hapo.
“Siyo uvimbe tu bali pia nilikuwa na kipanda uso, baada ya maombezi nimepona kabisa,” alisema Mohammed.
Aidha, Frida John alidai mbele ya waumini kanisani hapo kuwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kisukari lakini baada ya maombezi tatizo hilo halipo tena, hivyo anamshukuru Mungu.
MTOTO AKUTWA MAKABURINI USIKU
Tukio lililowatia majonzi wasikilizaji ni la mtoto Scola Mashaka, mkazi wa Mbezi Beach, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam ambaye alitoweka nyumbani kwao kimiujiza, lakini siku moja alipatikana makaburini usiku baada ya maombezi.
Mama wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Scola Kangale (51) aliyezungumza na gazeti hili kanisani hapo alisema kwamba mwanaye huyo alitoweka alfajiri ya Septemba 8, mwaka huu na akapatikana Septemba 21 usiku katika makabari ya Tegeta baada ya maombi ya Nabii Flora.
Akisimulia mkasa huo mama huyo alisema: “Mtoto wangu alitoweka katika chumba alichokuwa amelala na watoto wenzake na haikujulikana alipoelekea.
“Ilibidi tumfuate bibi yake aitwaye Kisa Kajeba ambaye anaishi maeneo hayo lakini hakupatikana hali iliyosababisha tupatwe na hofu, tulilazimika kwenda Kituo cha Polisi cha Mbezi juu kutoa taarifa ambapo tulifunguliwa jalada namba MBJ/RB/4057/2011,” alisema.
Alifafanua kuwa walimtafuta mtoto huyo katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam na kuamua kumtangaza magazetini na kwenye vituo vya runinga lakini hakuonekana.
Alisema walielekezwa na wasomaji wa magazeti kuwa waende kwa Nabii Flora na walipofika na kufanyiwa maombi alituambia hakufa isipokuwa alikuwa makaburini, Tegeta.
“Tulikwenda na saa tano usiku, tulimkuta akiwa amechoka, tulipomuuliza alikuwa wapi hakutujibu, tukampeleka kwa mjumbe wa nyumba kumi,” alisema.
Kwa upande wake mtoto Scola alisema haelewi alitowekaje nyumbani kwao kwani anachokumbuka ni kuona kivuli cha mtu na fahamu zikapotea.
MAELEZO YA NABII FLORA
Nabii Flora alipohojiwa na waandishi wetu waliotaka kujuwa mbinu alizotumia hadi mtoto huyo kupatikana alisema: “Kazi yangu ni kushusha huduma ya maombezi baadaye Mungu ananifunulia na kunionyesha.”
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walidai kuwa waliwahi kwenda kwa Babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Masapile, hawakupokea uponyaji lakini kwa nabii huyo wameupokea
No comments:
Post a Comment