Na Saleh Ally
SIKU chache baada ya kiungo wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila, kumshauri kocha wa timu hiyo, Kosta Papic (pichani), kuwa anatakiwa kumtumia Hamis Kiiza kama mshambuliaji wa kati na siyo wa pembeni, ushauri huo umetekelezwa na umezaa matunda.
Lunyamila alitoa ushauri huo kupitia kolamu yake maalum ya uchambuzi ndani ya Gazeti la Championi Jumatatu, ambapo alisema Yanga inakabiliwa na tatizo la kutokuwa na mfungaji wa kutumainiwa na akasema ni vema Papic afanye maamuzi magumu kwa kumtumia Mganda huyo na mmoja kati ya washambuliaji wa kati, Kenneth Asamoah au Davies Mwape.
Papic aliamua kumtumia Kiiza kama mshambuliaji wa kati akimpanga na Mwape huku Asamoah akiwekwa benchi. Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani Kiiza aliifungia timu yake bao pekee la ushindi katika mechi ya juzi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, wengi walitegemea ingeisha kwa suluhu kwa kuwa wenyeji waliwabana Yanga muda mwingi, lakini Kiiza alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kipa wa Coastal, Godson Mmasa, kufanya makosa ya kuutema mpira.
Katika siku za hivi karibuni, Kiiza amekuwa akifunga mabao muhimu katika kikosi hicho cha Jangwani wakati Mwape na Asamoah wakionekana kuwa butu kwenye safu ya ufungaji licha ya kupewa nafasi mara nyingi.
No comments:
Post a Comment