Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco Bw. William Mhando, amesimamishwa kazi leo kupisha
uchunguzi juu ya tuhuma dhidi yake za ubadhirifu na matumizi mabaya ya
madaraka.
Bodi
ya wakurugenzi ya Shirika la Umeme Nchini -TANESCO- imemsimamisha kazi
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi WILLIAM MHANDO ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa dhidi ya Menejimenti ya
TANESCO.
Taarifa
hiyo imetolewa na mwenyekiti wa bodi hiyo Jenerali Mstaafu ROBERT
MBOMA ambapo katika taarifa yake amesema maamuzi hayo yamefikiwa katika
kikao cha dharura kilichofanyika jana kujadili masuala mbalimbali
ikiwemo tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Taarifa
zinasema katika kikao hicho, Bodi iliona tuhuma hizo ni nzito hivyo ni
vyema zikafanyiwa uchunguzi huru na wa kina mara moja.
Jenerali MBOMA katika taarifa hiyo amesema uchunguzi huo utaanza mara moja kwa kutumia mchunguzi huru.
Aidha
Bodi hiyo, leo imefanya kikao kingine cha dharura ambapo imeamua
kuwasimamisha kazi mara moja wafanyakazi wengine wakiwemo naibu
mkurugenzi mtendaji, huduma za Shirika Ndugu ROBERT SHEMHILU, afisa
mkuu wa fedha Ndugu LUSEKELO KASSANGA na meneja mwandamizi, manunuzi
Ndugu HARUN MATTAMBO.
Jenerali
MBOMA amesema kufuatia hatua hizo zilizochukuliwa, Bodi imechukua hatua
stahiki ili kuhakikisha shughuli za kiutendaji na uendeshaj wa TANESCO
zinaendelea kama kawaida.
No comments:
Post a Comment