Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Mwaimu.
KWANZA tumshukuru Mungu kwa kutuweka hai leo na kubwa zaidi kwa
kutuwezesha kukutana katika safu hii kwa mara nyingine tena, hakika
Mungu anastahili kuabudiwa.Baada ya kusema hayo leo nitazungumzia zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa.
Kusema kweli zipo dalili lukuki hivi sasa zinazoonyesha kwamba zoezi hilo la kuandikisha wananchi ili wapewe vitambulisho vya uraia, halitafanikiwa, labda itokee miujiza.
Kwa kusema kweli zoezi limeanza vibaya, na inaonesha waandaaji, Mamlaka ya Vitambulisho (Nida) hawakujiandaa vya kutosha na pia hawakuwaandaa raia kuitikia wito wa kujitokeza kujiandikisha.
Babu zetu walisema ‘Siku njema huonekana asubuhi,’ lakini kwa Nida, sivyo maana shughuli yao ‘asubuhi’ yaani siku za kwanza za zoezi hilo mambo ni shaghalabaghala na wamesababisha wananchi kushindwa kujiandikisha na badala yake kusumbuka.
Nikiwa raia ninayeipenda nchi hii nafikiri nina wajibu wa kuonyesha upungufu na kufichua uozo unaoweza kukwamisha zoezi hilo muhimu lenye manufaa kwa taifa na ustawi wa watu wake.
Yapo matatizo makubwa yanayokwamisha zoezi hilo na tatizo kubwa lipo serikali kuu, haionyeshi dalili zozote za kufahamu nini kinaendelea katika mchakato mzima wa mpango huo.
Zoezi hilo nyeti linaonekana kuachwa katika mikono na mamlaka za chini za serikali za mitaa ambazo kwa kweli hazina uwezo wala nyenzo za kulifanikisha.
Kutokana na hilo wananchi wamekuwa wakiteseka na kupoteza muda mwingi kwenye foleni na wengine kushindwa kujiandikisha licha ya kutumia muda mwingi wakiwa kwenye foleni.
Katika baadhi ya sehemu taratibu zenye mkanganyiko zinatawala wakati wa kujiandikisha.
Kama hiyo haitoshi, Mamlaka ya Vitambulisho (Nida) imeonyesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kufahamu kuwa, ilipaswa kwanza kuendesha programu kubwa ya uhamasishaji kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Lakini pia waandikishaji wote walipaswa kupewa mafunzo stahiki ili kuepusha makosa na ubabaishaji ambao wananchi wanaushuhudia sehemu mbalimbali za nchi.
Uwezo wa waandikishaji wengi umeonekana kuwa chini ya kiwango na imegundulika kwamba wengi wao hawana elimu ya kutosha, matokeo yake ni kukosea majina ya wananchi wanaokwenda kujiandikisha.
Kutokana na hilo ni wazi kwamba siku ya kutolewa vitambulisho hivyo ikifika vinaweza kuwa na majina yaliyokosewa, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa na lawama kwa serikali.
Lakini pia kuna taarifa kuwa katika baadhi ya sehemu kuna idadi kubwa ya wananchi ambao wamegundulika kutojua kusoma wala kuandika na kufanya zoezi hilo kuwa gumu.
Kutokana na usimamizi usioridhisha wa Nido, wananchi wameonekana kutokuwa na uelewa wa taarifa gani wanazotakiwa kuwa nazo katika ujazaji wa fomu, kwani baadhi ya waandikishaji wamekuwa wakiwataka walete rundo la vitambulisho.
Mchanganyiko huo wa masharti ya utambulisho uko wazi kwani katika sehemu nyingine wametakiwa kuonyesha kitambulisho kimoja tu.
Wananchi pia wamekuwa wakilalamikia kasi ndogo ya uandikishaji ambayo imesababisha misururu mirefu katika vituo vya uandikishaji kiasi cha watu kushindwa kujiandikisha.
Mbaya zaidi hakuna utaratibu wowote wa kuwahudumia watu wenye ulemavu, wajawazito au wenye watoto wadogo na wazee au vikongwe. Nimeshuhudia mateso makubwa kwa watu hao kutokana na idadi ndogo ya waandikishaji katika vituo vya kujiandikisha.
Nido imewaruhusu wajumbe wa mashina ya chama tawala kuwajazia fomu za utambulisho wananchi wanaoishi katika maeneo yao ili waweze kuorodheshwa na serikali za mitaa na hatimaye kupewa vitambulisho vya uraia.
Utaratibu huo tayari umelalamikiwa na raia wa vyama vingine vya siasa kwani wanadai kuwa wajumbe hao wametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wanachama wa chama chao kujiandikisha kwa wingi ili washinde katika chaguzi zijazo.
Ni vigumu kuelewa kwa nini serikali kuu na Nido hazikuona umuhimu wa kuhakikisha kwamba vifaa kama karatasi, kalamu, huduma za kupiga picha na kurudufu zinapatikana bila malipo kama ilivyokuwa wakati wa kujiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Matokeo yake kuna baadhi ya wananchi wanaofika kujiandikisha wanalalamika kwamba sehemu fulani hapa nchini wanadaiwa rushwa kwa kisingizio cha serikali kutoweka vifaa hivyo na huduma nyingine.
Kutokana na mlolongo wa changamoto hizo nasema kuwa zoezi hilo limekwenda ndivyosivyo na naamini siyo wananchi wote wataweza kulipa fedha hizo, hawa wakulima na watoto wao na wengine wanaweza kuacha kwenda kujiandikisha.
Ipo haja basi Nida kuongeza muda na elimu kwa waandikishaji ili kusudio la serikali kuandikisha raia wote ili wapatiwe vitambulisho vya taifa linafanikiwa, vinginevyo tutakuwa tunapoteza muda na fedha bure.
Namuomba Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na timu yake kuyaangalia haya na kuyasafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment