Leon Bahati
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ameizuia Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kuchunguza sakata la kusimamishwa kwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando.Mhando na watendaji wengine watatu walisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo Julai 14, mwaka huu wakituhumiwa kwa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Tamko hilo lilionekana kuishangaza POAC na kuifanya iitishe kikao cha dharura na Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wajumbe wa kamati hiyo wamekubaliana kuwahoji wajumbe wa Bodi ya Tanesco inayoongozwa na Jenerali Mstaafu Robert Mboma kuhusiana na hatua hiyo.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe aliliambia gazeti hili jana kwamba, mpango wao ulikwama baada ya Makinda kuwashauri wasiingilie uamuzi huo uliotolewa na Serikali ambao ni mhimili mwingine.
“Spika alituelekeza tuache mhimili huo ufanye kazi zake. Maadamu (Mhando) hakufukuzwa, amesimamishwa tu, ameona tuiache Serikali ifanye uchunguzi wake,” alisema Filikunjombe.
Mbunge huyo wa Ludewa alisema wajumbe wa POAC, waliunga mkono wazo la Spika Makinda na kuona kuwa ni hoja ya msingi, hivyo wakaamua kusitisha mchakato huo.
Spika Makinda
Spika Makinda aliliambia gazeti hili jana kuwa, kimsingi POAC haina madaraka ya kuhoji kuhusu Mhando kusimamishwa kazi.
“Hawana madaraka hayo. Kazi ya Kamati ya Bunge ya Kusimamia Hesabu za Mashirika ya Umma ni kupitia Hesabu za Mashirika ya Umma zilizokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),” Makinda alifafanua.
Alieleza kuwa, POAC inapaswa kupitia hesabu za mashiririka yote ya umma kila baada ya mwaka kumalizika na kutoa ushauri wake kabla ya kuingia bajeti nyingine.
Hata hivyo, Makinda alisema POAC haijamwandikia barua yoyote wala kwenda kumwona ili awashauri juu ya mkakati wao wa kwenda kuihoji Bodi ya Taneso.
“Hawajaniomba,” alisema Makinda na akiweka msimamo kwamba, POAC haina madaraka ya kwenda kuhoji juu ya utendaji wa Serikali.
Zitto Kabwe
Hata hivyo, Zitto aliliambia gazeti hili jana kuwa mpango wa kamati yake kukutana na bodi bado uko palepale, lakini akakataa kuliweka wazi suala hilo.
“Lengo ni kufafanua masuala fulani fulani ya kimahesabu,” alisema Zitto akibainisha kuwa kwa sasa wanasubiri kamati ya kisekta ikamilishe kazi yake na bodi hiyo.
Julai 13, mwaka huu Zitto alisema POAC itamwomba Spika Makinda awaruhusu kwenda kuihoji bodi ya Tanesco kuhusu hatua yake ya kumsimamisha kazi Mhando na kwamba, watamwita Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kupata ufafanuzi juu ya suala hilo.
“POAC tunahusika na usimamizi wa hesabu za fedha za shirika, tunataka kujua ubadhirifu na masuala ya kisheria na itahakikisha uwajibikaji unaostahili na tutasimamia hilo kwa nguvu zote kwani hatutaki uonevu.”
Taarifa ya Bodi ya Tanesco ilionyesha kuwa, Mhando alisimamishwa Julai 13 na kuagiza uchunguzi uanze kufanyika mara moja.
Watendaji wengine waliosimamisha kazi na Mhando ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Ununuzi, Harun Mattambo.
Katibu Mkuu Nishati na Madini anena
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesema kuwa Bodi ya Tanesco bado haijawapatia taarifa rasmi ya kusimamishwa kwa Mhando.
“Hatujapata taarifa yoyote ya maandishi… Hata mimi nimezisoma kupitia vyombo vya habari kama ulivyosoma wewe,” alisema Maswi.
Kauli hiyo ya Maswi ni tofauti na ile aliyoitoa kwa gazeti hili wiki iliyopita akisema kwamba anafahamu kwa undani juu ya sakata hilo.
Juhudi za kumpata Jenerali Mboma ili afafanue suala hilo zilishindikana baada ya msaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Omari kusema kuwa alikuwa amebanwa na mikutano mjini Dodoma.
Mhando aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanesco Juni Mosi Mwaka 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Meneja Mkuu wa Usambazaji Umeme na Masoko wa shirika hilo.
Mhando alichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Idris Rashid ambaye alimaliza muda wake.
Aliajiriwa na Tanesco Oktoba, 1987 kama Mhandisi wa Umeme na baadaye alipandishwa na kuwa Mhandisi katika njia za umeme. Mwaka 1990 hadi 1992 alikuwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment