1. UTANGULIZI
Wazo la
kuanzisha Vitambulisho vya Taifa kwa Raia wa Tanzania na Raia wageni
waishio nchini Tanzania lilizaliwa mwaka 1968 katika Kikao cha
“Interstate Intelligence Gathering” kilicho-jumuisha wajumbe kutoka nchi
za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia. Kwa wakati huo nchi za Kenya na
Zambia tayari zilikuwa na Vitambulisho vyao vya Taifa. Iliazimiwa kwamba
ili kuimarisha mahusiano ya kiusalama yanayozingatia Utawala wa Sheria
katika nchi hizo nne ni lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa
Vitambulisho vya Taifa kwa Raia wao.
Kumekuwa na
jitihada mbalimbali za Serikali kuhakikisha Watanzania na wageni wote
wanapatiwa Vitambulisho vya Taifa, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa
matunda yaliyotajariwa kwa kipindi kirefu kutokana na sababu
mbalimbali. Mwaka 1986 Serikali ilitunga Sheria ya Vitambulisho ambayo
haikutumika wala kutungiwa kanuni zake.
Ni ukweli
ulio wazi kwamba kwa wakati huu kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na
Vitambulisho vya Taifa kulingana na mazingira tuliyonayo. Kuanzishwa kwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo nchi tano zimeungana na kukubaliana
kwamba watu wa nchi hizo wanaweza kutembeleana bila bughudha pia
kumeongeza umuhimu wa kuwa na Vitambulisho. Ikumbukwe kuwa Tanzania na
Uganda ndizo nchi pekee katika Jumuiya hiyo ambazo hazina Vitambulisho
vya Taifa.
Upembuzi yakinifu wa Vitambulisho vya
Taifa ulikwishafanyika na matokeo ni kwamba Mradi unatekelezeka. Aidha
taarifa hiyo imeainisha makadirio ya gharama za Mradi na namna mradi
utakavyotekelezwa ambapo teknolojia ya “Smartcard” ndiyo itakayotumika
kama ilivyokubaliwa na Baraza la Mawaziri katika kikao kilichokaa mjini
Dodoma mwezi Februari, 2007.
Mhe. Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania tayari ametia saini Hati ya kuidhinisha
kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia Vitambulisho vya Taifa
kinachojulikana kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa au “National
Identification Authority (NIDA)”. Hati hii imechapishwa katika Gazeti la
Serikali, GN No.122 ya tarehe 01/08/2008.
Aidha
katika Kikao chake cha tarehe 3 Februari, 2007 Baraza la Mawaziri
lilitoa mwongozo kuwa iundwe Kamati ya Usimamizi (Steering Committee) ya
Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara na Vitengo vinavyohusika na mambo muhimu
kuhusu Vitambulisho vya Taifa. Kamati hii pamoja na mambo mengine
itakuwa na jukumu la kutoa mwongozo na mwelekeo wa program za Mradi.
Baraza
pia liliamua kuwa taarifa ya upembuzi yakinifu ya Kampuni ya Gotham
International Limited (GIL) iwe ndio mwongozo wa utekelezaji wa Mradi na
Kampuni hiyo iliteuliwa kuwa Mshauri mwelekezi wa Mradi.
Katika
hatua nyingine, Serikali ilitoa mwongozo kuwa taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa mradi ikiwemo ile ya mshindi wa zabuni ya mkandarasi wa
kutengeneza mfumo wa Vitambulisho vya Taifa ziwasilishwe katika Baraza
la Mawaziri ili kupata ridhaa yake.
2. DHANA YA KITAMBULISHO CHA TAIFA
Swala
la mfumo wa Kitambulisho cha Taifa bado ni dhana ngeni miongoni mwa
watu wengi hususani umuhimu wake kwa mwananchi, Taasisi mbalimbali na
Serikali kwa ujumla. Hata wakati mwingine baadhi ya watu hudhani ya
kwamba ni kitambulisho cha Uraia, au ni Kitambulisho kama vilivyo
vitambulisho vingine vya kazi, au ni kipande cha karatasi chenye picha,
jina la mhusika pamoja na anuani yake.
Dhana
nzima ya mfumo wa Kitambulisho cha Taifa ni pana zaidi ya hapo. Pia ni
vyema ieleweke kwamba kadi za Vitambulisho vya Taifa zitatolewa kwa watu
wazima kuanzia miaka 18 na sio watoto wadogo kama inavyoelezwa.
Vitambulisho
vya Taifa kulingana na Nchi mbalimbali mfano Angola, Afrika Kusini,
Bostwana na Kenya, ambazo zimeweza kutengeneza Vitambulisho vyao vya
Taifa hutengenezwa kutokana na taarifa zilizohifadhiwa kwenye daftari
maalum. Daftari hilo hutunza kumbukumbu za mtu kuanzia alipozaliwa hadi
mwisho wa uhai wake, huboreshwa kwa kupokea au kuongezwa taarifa za mara
kwa mara za mhusika kutokana na matukio mbalimbali yanayomhusu mhusika.
Taarifa hizo huhifadhiwa katika daftari moja, na mhusika hukabidhiwa
kadi ambayo hutumika kama alama ya utambulisho. Aidha Taasisi nyingine
zinaweza kutumia taarifa zilizohifadhiwa kwenye daftari hiyo kwa
makubaliano maalum.
Wakati mwingine watu hutaja
kitambulisho cha Uraia wakiwa na maana ya Kitambulisho cha Taifa. Ukweli
ni kwamba Taasisi hii itahusika na kutengeneza Kitambulisho cha Taifa
ambacho kitatolewa kwa Raia wa Tanzaia na watu wengine ambao sio Raia wa
Tanzania.
3. UMUHIMU WA MFUMO WA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Mfumo wa Kitambulisho cha Taifa unaanzishwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
- Kutambua mtu au mhusika.
- Kusaidia kumtambua mhusika anapohitaji kupatiwa huduma katika Taasisi mbalimbali mfano benki,taasisi za mikopo, huduma za afya n.k.
- Kuunganisha mifumo mingine kwa lengo la kuwasiliana na kubadilishana taarifa muhimu ambazo zitalenga kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
- Kumtambua mtu pale anapofanya uhalifu wa aina Fulani; hii itasaidia sana katika kupambana na uhalifu.
- Kutambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye mabenki hasa pale wakopaji wanapochukua mikopo kutoka katika mabenki mbalimbali.
- Kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari.
- Kutambua walipa kodi, hii itasaidia kupambana na wakwepaji wa kulipa kodi.
- Kumtambua mtu anapofanya biashara mbalimbali kwa kutumia majina tofauti.
- Kuhakikisha kuwa mtu anapata stahili zake za jamii, kwa mfano kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu , haki za kujiunga na shule ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo Raia wa Tanzania anastahili. Hii itasaidia kuondoa watumishi hewa kwenye “payroll “ ya Serikali.
- Kuboresha utendaji kazi Serikalini kwa kuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao; hasa pale wanapostaafu.
- Kupunguza gharama za mwananchi kutokana na huduma mbalimbali anazozipata kutolewa na Taasisi moja.
- Kurahisisha zoezi la kuhesabu watu/sensa.
4. MAENEO YANAYOTAKIWA KUBORESHWA ILI KUFANIKISHA MFUMO WA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Gharama
za kutengeneza Vitambulisho hujumuisha gharama mbalimbali ikiwa ni
pamoja na miundombinu yake, rasilimali watu, mafunzo na kuboresha maeneo
muhimu yatakayokuwa yakishirikishwa katika utekelezaji wake mfano ni
yafuatayo:-
- RITA (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini) – kuboresha mfumo wa Usajili wa vizazi na vifo.
- TRA (Mamlaka ya Kodi) – Uboreshaji wa mfumo wa utoaji wa leseni za uendeshaji wa magari.
- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara hii ndiyo msimamizi wa Serikali za Mitaa na ndio wenye taarifa zote za watu Mijini na Vijijini.
- Polisi, kuboresha mfumo wa taarifa za udhibiti wa uhalifu.
- Mifumo ya mishahara na ki-utumishi kwa kurahisisha namna ya kuwatambua watumishi.
- Kuanzisha Mtandao wa Mawasiliano “Networking and Connectivity”.
- Kujenga vituo vya usajili vya Wilaya (Registration Centres) na kujenga (Data Centre) Makao Makuu.
- Kutoa elimu kwa Umma (Public Awareness) ili kuwawezesha kujua umuhimu wa dhana nzima ya Vitambulisho vya Taifa.
- Kuanza zoezi la usajili wa watu kwa lengo la kupata taarifa muhimu za watu.
- Taasisi za mifumo ya jamii kama NSSF, PPF, GEPF n.k zitaweza kupata taarifa za watu baada ya kuboresha mifumo yao. Kwa hiyo tunapozungumzia gharama za kuendesha shughuli za Vitambulisho vya Taifa hutumaanishi kadi tu bali ni jumla ya gharama zote za uendeshaji katika kutekeleza zoezi zima la mfumo wa Vitambulisho vya Taifa.
5. HATUA ZA UTEKELEZAJI
Utekelezaji
wa Mradi umepangwa kuwa katika awamu mbili ambapo awamu kwanza ni
maandalizi ya Mradi na awamu ya pili ni awamu ya utekelezaji wa Mradi
wenyewe. Ifuatayo ni taarifa ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya
maandalizi ya mradi:-
- Jengo la ofisi limenunuliwa na kufanyiwa ukarabati pamoja na kuwekewa samani za ofisi
- Hati ya kuanzisha Mamlaka (Establishment Instrument) tayari imesaniwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali GN. 122 ya tarehe 01/08/2008. Mamlaka hiyo inajulikana kama “National Identification Authority” (NIDA) au Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
- Zabuni kwa utaratibu wa Pre- Qualification ilitangazwa na Makampuni 104 yalijitokeza kununua vitabu vya zabuni.
- Makampuni 54 yalirudisha zabuni zao
- Kamati ya Uchambuzi ilitumia mwezi mmoja kufanya tathimini na kupendekeza makampuni manane (8) yaingie katika hatua inayofuata.
- Bodi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilikutana na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Uchambuzi
No comments:
Post a Comment