Waheshimiwa Wananchi wenzangu,
Amani iwe kwenu,
Kwa kipindi cha wiki nzima kumekuwepo
na mjadala mkali bungeni, kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii
na katika taifa kwa ujumla juu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2012/13 sanjari na yaliyojiri kutokana na kauli niliyotoa bungeni juu ya
udhaifu wa Rais katika usimamizi wa maandalizi na utekelezaji wa bajeti
pamoja na mipango muhimu ya maendeleo. Ukweli ni uhuru!.
Aidha, kupitishwa kwa Mpango wa
Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 na Bajeti ya Mapato na
Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/2013 bila marekebisho
yoyote ya msingi pamoja na michango mingi ya wabunge ya kukosoa
kumedhihirisha kile nilicho tahadharisha tangu awali kwamba; kwa kuwa
udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa Rais juu ya bajeti na
uendeshaji wa nchi, udhaifu wa Rais una athiri maisha ya wananchi.
Ukweli ni Uhuru!.
Katika mazingira haya, udhaifu wa rais
na uzembe wa bunge unapandikiza migogoro kati ya wananchi na serikali
kutokana ufisadi na masuala ya maendeleo kutopewa kipaumbele cha kutosha
zaidi ya matumizi ya kawaida lakini pia inachochea pia migomo baridi ya
watumishi wa umma hususun madaktari, walimu na askari kutokana pia na
madai yao ya muda mrefu kutokuzingatiwa kwenye bajeti. Ukweli ni Uhuru!
Kadhalika udhaifu wa kanuni za Kudumu
za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka kwa mujibu wa kanuni 97 (2) ya
kuchangia mjadala kuhusu hotuba ya bajeti kwa kuchangia tu mambo ya
ujumla yanayohusiana na hali ya uchumi wa nchi na kwamba mbunge yoyote
haruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi
ya serikali. Ukweli ni Uhuru!
Pia, katiba imempa mamlaka makubwa
Rais juu ya Bunge kwa kuwa Bunge likikataa bajeti ya serikali kwa mujibu
wa Ibara ya 90 (2) (b) moja kwa moja Rais analivunja bunge suala ambalo
huwapa hofu wabunge wengi hususani wa chama kinachotawala na kuwafanya
wapige kura ya NDIO hata kama waliikosoa bajeti husika. Hivyo, udhaifu
wa bunge unachangiwa na ukweli kwamba katiba imeweka nguvu kubwa kwa
Rais katika kuvunja bunge linapokataa bajeti wakati huo huo kanuni
zimekataza wabunge kupendekeza mabadiliko katika bajeti; kwa hivyo
wabunge hawana uwezo wa kubadilisha na wakati huo huo wakikataa bunge
linavunjwa, katika mazingira haya udhaifu wa Rais wa kushindwa kutumia
nguvu hizo za kikatiba una madhara makubwa sana kwa nchi na maisha ya
wananchi. Ukweli ni Uhuru!
Kwa mantiki hiyo, katika mchakato wa
katiba mpya ni muhimu kwa wananchi kutoa maoni ya kuwezesha ukuu na
uhuru wa bunge katika kuisimamia serikali kwenye mchakato wa bajeti kwa
ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. Wakati
katiba mpya ikisubiriwa, ni muhimu kwa marekebisho ya haraka kufanyika
katika kanuni za kudumu za bunge hususani sehemu ya tisa inayohusu
utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kuanzia kanuni ya 94
mpaka kanuni ya 107 ili kuongeza nguvu za bunge katika kuishauri na
kuisimamia serikali kwa mujibu wa madaraka ya bunge ya ibara ya 63 (2)
na (3) ya katiba ya sasa. Katika muktadha huo, nimeanza kufanya
uchambuzi ili kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni.
Ukweli ni Uhuru!
Hata hivyo, hata kwa kanuni zilizopo
sasa udhaifu wa bunge unaongezeka kutokana na maamuzi ya kizembe
mathalani ya kutozingatia matakwa ya kanuni za bunge, mfano Kanuni ya 94
inalitaka bunge ili kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika ibara ya
63 (3) (c) ya Katiba kwa kukaa kama kamati ya mipango katika mkutano
wake wa mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendezo ya
mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali kwa mwaka wa fedha
unaofuata, kanuni ambayo toka niingie bungeni haijawahi kutekelezwa kwa
wakati hata mara moja pamoja na kuwakumbusha wanaohusika kusimamia
kanuni. Ukweli ni Uhuru!
Mwaka huu udhaifu umekuwa mkubwa zaidi
kwa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 sanjari
na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha
2012/2013 tarehe 18 Juni 2012 na kupitishwa siku moja tarehe 22 Juni
2012 hali ambayo imechangia katika kufanya bajeti ya nchi isizingatie
kwa ukamilfu mpango wa taifa wa miaka mitano. Ukweli ni Uhuru!
Nashukuru kwamba Spika wa Bunge Anna
Makinda amekiri bungeni tarehe 20 Juni 2012 kwamba kulikuwa na udhaifu
wa miaka mingi wa kutozingatia kanuni ya 106 ambayo inalitaka bunge
kujadili muswada wa sheria ya fedha mwishoni baada ya bunge kukamilisha
kazi ya kupitisha muswada wa fedha za matumizi ili kuiwezesha serikali
kuongeza vyanzo vya mapato kama wabunge tulivyopendekeza mwaka 2011 na
pendekezo hilo kurudiwa tena na kamati ya fedha na uchumi tarehe 18 Juni
2012. Ukweli ni Uhuru!
Izingatiwe kuwa iwapo sheria ya fedha
ingepitishwa tarehe 22 Juni 2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali athari
zake zingekuwa kubwa kwa kuwa udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa
Rais juu ya utaratibu wa kutunga sheria kuhusu mambo ya fedha kwa
mujibu wa ibara ya 99 (1) kwa kuweka masharti kwamba bunge
halitashughulikia sehemu kubwa ya masuala ya fedha isipokuwa kama Rais
amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na bunge na pendekezo hilo
la Rais liwe limewasilishwa kwenye bunge na waziri. Hivyo, michango na
mapendekezo ya wabunge bila Rais mwenyewe kupendekeza isingeliwezesha
bunge kufanya mabadiliko ya kupanua wigo wa mapato kwa kuwa kwa kuwa
mujibu wa ibara 99 (2) (a) (i) udhaifu wa bunge ni pamoja na kukatazwa
kutoza kodi au kuongeza kodi. Ukweli ni Uhuru!
Hivyo, Kamati ya Fedha na Uchumi
itumie vizuri mwanya wa ibara ya 99 (3) kurejea maoni yake, ya kambi
rasmi ya upinzani bungeni na michango ya wabunge ya mkutano wanne wa
Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 na kufanya
marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha kwa kumshauri Waziri. Ukweli
ni Uhuru!
Aidha, ili kuondoa udhaifu uliopo Rais
Kikwete mwenyewe asome kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard) za tarehe 18
Juni mpaka 22 Juni 2012 na kuliongoza baraza la mawaziri kumwezesha
Waziri wa Fedha ya 86 (10) kuwasilisha muswada wa sheria uliochapishwa
upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayopaswa kufanyika yenye
kulenga kupunguza kodi katika bidhaa zenye kuchangia mfumuko wa bei na
kupanua wigo wa mapato kwa kuongeza kodi kwenye vyanzo mbadala
tulivyovieleza bungeni. Ukweli ni Uhuru!
Izingatiwe kuwa nilipotolewa bungeni
tarehe 19 Juni 2012 nilieleza kwa ufupi nilichosema bungeni na
nilichotarajia kusema na kuahidi kwamba nitatoa tamko kamili baadaye;
baada ya kujipa muda wa kutafakari nimefikia uamuzi wa kutoa tamko
husika wakati bunge litakapoelekea kujadili utekelezaji wa bajeti ya
mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya
Rais kwa mwaka wa fedha 2012/2013; ambapo pamoja na masuala mengine
nitaeleza hatua ambazo Rais anapaswa kuchukua kuwezesha ahadi alizotoa
kwa watanzania kuweza kutekelezwa na serikali. Ukweli ni Uhuru!
Kwa sasa niwashukuru wananchi wa
Ubungo, wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na watanzania kwa ujumla
walionielewa na kuniunga mkono kupitia maoni yao kwenye mitandao ya
kijamii, simu za mkononi na katika vyombo vya habari. Nawashukuru pia
viongozi wa dini, chama na asasi mbalimbali nje na ndani ya serikali
walionipa moyo wa kuendelea kusimamia ukweli na kuacha unafiki ili
kusimamia uwajibikaji wa viongozi kwa maendeleo ya taifa. Ukweli ni
Uhuru!
Nashukuru pia kwa mchango wa
walinipinga na kunikosoa kutokana na kauli niliyotoa juu ya udhaifu wa
Rais Kikwete, wapo walioeleza kuwa ilitokana na jazba na wengine
wameeleza kuwa ningetumia lugha ya diplomasia kufikisha ujumbe ili
kutodhalilisha taasisi ya urais na kwa kuzingatia utamaduni wetu wa
heshima kwa wakubwa na wapo wachache waliosema kwamba ni matusi kutamka
‘udhaifu wa Rais’. Ukweli ni Uhuru!
Wakati mjadala huu ukiendelea ni rai
yangu kwamba rejea ifanyike katika mchango wangu wa tarehe 5 Julai 2011
wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais
kwa mwaka 2011/2012 na rejea kamili pia ifanyike kwenye mchango wangu wa
tarehe 19 Juni 201; na ieleweke kwamba naheshimu taasisi ya urais na
umri, naamini katika matumizi ya lugha ya kidiplomasia, hata hivyo
nilitafakari na kuamua kuusema ukweli kwa lugha ya moja kwa moja ili
ujumbe ufike kwa mamlaka zote zinazohusika na wauchukulie kwa uzito
tofauti ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita. Ukweli ni uhuru!
Niliamini, naamini na nitaendelea
kuamini kwamba kutamka neno ‘udhaifu wa Rais’ sio kumtukana Rais na wala
sio kulitumia jina la Rais kwa dhihaka; hata hivyo kwa kuwa pamekuwepo
na mwelekeo wa propaganda za kudai kuwa kauli hiyo ni matusi na kwa kuwa
chanzo cha propaganda hizo ni udhaifu uliofanywa na Naibu Spika Job
Ndugai bungeni wa kunihukumu kwa kutumia kanuni tofauti na tuhuma
iliyotolewa; nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake ili kuwe na
mjadala mpana wa kibunge utakaowezesha kumbukumbu sahihi kuwekwa. Ukweli
ni uhuru!
Katiba ya Nchi ambayo niliapishwa
kuilinda pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba
“Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya
Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia
na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote
katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”. Toka
nichaguliwe kuwa mbunge mwaka 2010 kwa nyakati na maeneo mbalimbali
viongozi wa vyama, dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi
wa kawaida wakilalamika kuhusu udhaifu wa Rais na kutaka atumie nguvu na
mamlaka yake ya kikatiba kuiongoza kwa uthabiti serikali kushughulikia
masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yanayolikabili taifa; niliamua
kuendelea kusema bungeni kwa mara nyingine ikiwa ni sehemu ya kutimiza
wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Ukweli
ni Uhuru!
Tarehe 19 Juni 2012 nilieleza bungeni
kabla ya kutolewa sababu za kuikataa bajeti na tarehe 22 Juni 2012
nilipiga kura ya hapana ya kuikataa bajeti kwa kutokuweka misingi
thabiti ya kutimiza ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya maisha bora kwa kila
mtanzania na badala yake kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kushindwa
kukabiliana na matatizo ya mfumuko wa bei. Aidha, kiwango cha fedha kwa
ajili ya miradi ya barabara na maji kwa upande wa jiji la Dar es salaam
ikiwemo jimbo la Ubungo ni kidogo tofauti na kile kilichotajwa na Rais
Kikwete na kuingizwa kwenye jedwali la Mpango wa Taifa wa miaka mitano
kwa upande wa miradi ya maendeleo iliyopaswa kutengewa fedha katika
bajeti ya 2012/2013. Ukweli ni Uhuru!
Pamoja na utetezi uliotolewa na
Serikali juu ya mgongano kati ya tafsiri kati ya kiingereza na
Kiswahili, ukweli utaendelea kubaki kuwa tuliamua kuikataa bajeti kwa
kuwa ilishindwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ambao uliwasilishwa na Rais Kikwete na ukapitishwa kwa azimio la bunge
ambao ulipaswa kuiongoza serikali kuweka mkazo katika kuendeleza nchi
kwa kutumia fedha za ndani kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwenye
miradi ya maendeleo kama zilivyokokotolewa katika mpango husika. Ukweli
ni Uhuru!
Naamini Rais Kikwete anayofursa ya
kurekebisha udhaifu huo kwa kuongeza nguvu zake katika muswada wa sheria
ya fedha kupanua wigo wa mapato na hatimaye kumwezesha Waziri wa Fedha
kuwasilisha bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 107 mapendekezo ya matumizi
ya nyongeza ya fedha za serikali yenye kulenga kuongeza kiwango cha
fedha za maendeleo. Kwa upande wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es
salaam, serikali kwenye bajeti ya nyongeza inayopaswa kuwasilishwa
iongeze fedha za miradi ya Maji kwa upande wa Ruvu Juu ikiwemo kutenga
fedha za kutosha za ujenzi wa Bwawa la Kidunda, kwa upande wa Barabara
iongeze fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara za pembezoni
za mchujo na za mzunguko za kupunguza msongamano wa magari, na fidia ya
ardhi kwa wananchi wa Kata ya Kwembe wanaopaswa kuhama kupisha ujenzi wa
Chuo Kikuu Muhimbili (MUHAS) Eneo la Mloganzila. Ukweli ni Uhuru!
Kwa Wasemaji wa CCM waliodai kwamba
nimetoa lugha ya matusi dhidi ya Rais na mwenyekiti wa chama chao wasome
Kitabu cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania cha mmoja wa waasisi wa
TANU na CCM Mwalimu Julius Nyerere ambapo wakati huo taifa likiwa
katika mtanziko alimueleza Rais wa wakati huo kuwa ni ‘kiongozi dhaifu’
katika ukurasa wa 50 na kuendelea kusema katika Ukurasa wa 51 na
namnukuu “Kwa sababu ya minong’ono-nong’ono ya watu wasiiona mbali
kuhusu Rais, na kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu,
nililazimika kuiambia wazi wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha
Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu wa kumsaidia Rais amalize
kipindi chake salama”. Ukweli ni Uhuru!
Naamini Mwalimu Nyerere hakumtukana
Rais Mwinyi, kwa hiyo kunituhumu nimetukana ni kumtuhumu pia Marehemu
Baba wa Taifa; narudia tena kusisitiza kuwa udhaifu uliojitokeza ni
kutokana na Rais kutokutumia kwa uthabiti nguvu na mamlaka yake kwa
mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36, 37, 38 na 99 juu ya utendaji
wa serikali na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo. Ukweli ni
Uhuru!
Nimalize kwa kunukuu kitabu kingine
cha Mwalimu Nyerere cha miaka ya mwanzoni mwa 1960 cha TUJISAHIHISHE, “
Makosa yetu mengine hutokana na woga; woga unaotuzuia kumlaumu mkubwa
japo tunajua kuwa kakosa, au kumtetea mdogo anayelaumiwa na wakubwa japo
tunajua kuwa hana makosa. Na msingi wa woga ni ubinafsi. Pengine huwa
tunaogopa sisi wenyewe kulaumiwa au kupata hasara fulani. Pengine
twaweza kuwa hatuna cheo chochote ambacho tunaogopa kupoteza; pengine
huwa hatuna wala tamaa yoyote ya kupata cheo fulani. Lakini woga unaweza
kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi
wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza
ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio
wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa
kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha,
wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana.", mwisho wa
kunukuu: Ukweli ni uhuru.
Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika
22 Juni 2012
Bungeni-Dodoma
No comments:
Post a Comment