Mpango wa kadi za vitambulisho vipya vya taifa umeanza mwezi uliopita jijini Dar es Salaam katika jitihada za kuimarisha usalama na kuongeza mapato ya serikali, kwa mujibu wa Naibu Kamishna Mkuu wa Polisi, Issaya Mangulu. Mpango huo unawataka raia wa Tanzania na wa kigeni wanaokaa nchini humo kwa angalau miezi sita kujisajili na walio na umri wa kuanzia miaka 18 kujisajili na kutembea na kitambulisho.
"Kimsingi, vitambulisho hivi vitasaidia
mfumo wetu wa kuwafuatilia wahalifu," Mungulu aliiambia Sabahi. "Taarifa
kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zitatumika (wakati wa
uchunguzi) kujua historia ya mshukiwa, ambayo inajumuisha anapoishi au
kufanya kazi na mengine kama hayo."
Alama za vidole na picha za wenye
vitambulisho hivyo zitachukuliwa kurahisisha utaratibu wa kuwatambua
watu hapo baadaye. Kuwatambua watu wanaoishi na kufanya kazi nchini
Tanzania ni jambo la msingi katika kuhakikisha usalama, hasa kutokana na
idadi isiyojulikana ya wakimbizi ambao wameingia kutoka nchi jirani
zenye vita na migogoro, alisema. Kwa zaidi ya miaka 40, Tanzania
imepokea wakimbizi kutoka Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo, na baadhi ya wahalifu wanaweza kuja kupitia njia hiyo hiyo,
alisema Mungulu.
Kutokana na wimbi hilo la wakimbizi
wanaoingia nchini, kuwa na mfumo wa kutambua utaifa wa mtu, hadhi ya
kisheria na taarifa nyingine kunakuwa muhimu kwa juhudi za jumla za
usalama, alisema. Taarifa za vitambulisho vya taifa zitaunganishwa na
mifumo mingine ya kitaifa, kama vile mfumo wa namba za posta, Mamlaka ya
Mapato ya Tanzania, taarifa za polis,i na mashirika ya usalama ya
kimataifa kama vile Interpol. Mafungamano ya mashirika kadhaa, ya ndani
na ya nje, yatasaidia kufikia lengo la muda mrefu la usalama na uchumi,
alisema Mungulu.
Hadi sasa, waajiriwa wa serikali na
wataalamu wanaofanya kazi kwenye mabenki wamepewa kipaumbele na
kusajiliwa, alisema Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu, katika
mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Mpango huo ulioanza
Septemba, utasambaa sehemu zote za nchi. Usajili unatarajiwa kukamilika
mwaka 2014, lakini utaendelea hata baada ya hapo kuwasajili raia ambao
wanafikia umri wa kulazimika kuwa na kitambulisho. "Usajili utakuwa
utaratibu wa kuendelea," alisema Maimu.
Kwa ajili ya kujiandaa vyema na hatua
hii, Maimu alisema NIDA ilifanya programu ya majaribio mwanzoni mwa
mwezi Juni katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Zoezi hilo
liliisaidia mamlaka hiyo kuyagundua na kuyapatia ufumbuzi mapungufu
yaliyoonekana kwenye mchakato huo, alisema. "Kama unavyojua, Dar es
Salaam ndio mji mkubwa kabisa nchini. Tukifanikiwa kutoa vitambulisho
Dar es Salaam, mradi huu utafanikiwa nchi nzima," Maimu aliwaambia
waandishi wa habari. Vitambulisho vitatolewa bure kwa Watanzania wote,
ambapo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)
litalipia gharama za vitambulisho vya wakimbizi.
Vitambulisho vinaunganishwa na huduma za kijamii, mikopo ya benki
Chini ya mpango huo mpya, itakuwa ni
lazima kwa raia wa Tanzania kujisajili na kutembea na kitambulisho cha
uraia. Kuvunja sheria hiyo kunaweza kupelekea kifungo cha hadi miezi
sita, alisema Meneja Mahusiano wa NIDA, Thomas William. "Baada ya yote,
kitambulisho hicho kitakuwa kinaunganishwa na mifumo ya huduma za
kijamii. Ukikataa kujisajili au kutoa taarifa za uongo, hilo litakuwa na
athari kwako mwenyewe. Utakuwa hustahiki kupata huduma nyingine za
kijamii hadi utakapokuwa na kitambulisho hicho. Kwa hivyo, watu lazima
wawe navyo," William aliiambia Sabahi.
Vitambulisho hivyo vitatolewa na kampuni
ya Malaysia iitwayo Iris Corporation Berhad, ambayo imeshinda zabuni ya
kutoa vitambulisho milioni 25. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni
200 (dola milioni 124) na unafadhiliwa na serikali ya Tanzania. Joseph
Bwakyayo, 55, mfanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara jijini Dar es
Salaam, aliiambia Sabahi kwamba kuwatambua wakopaji kutawasaidia
wakopeshaji kutathmini hatari na gharama za mtu binafsi na kuamua juu ya
uwezo wa kukopesheka wa kila mkopaji, ambako kutaifanya mikopo iwe
rahisi zaidi kufikiwa na raia. "Watanzania hawakusajiliwa na ni gharama
kubwa kuwatambua waombaji wote wa mikopo kuhakikisha kuwa benki
zinawakopesha watu wanaostahiki. Ni kama kucheza kamari," alisema
Bwakyayo.
Bwakyayo alisema mara kwa mara
wakopeshaji hulazimika kuthibitisha mambo mepesi kama eneo la makaazi
kwa kutembelea nyumbani au kwenye biashara ya mkopeshwaji, na ambako pia
huweza kukutana na utapeli wa wale wanaojifanya kuwa ni wamiliki wa
biashara fulani. "Kufidia hatari kama hizo, tunaweka kiwango kikubwa cha
riba," alisema. Pamoja na kuziweka gharama za kuthibitisha juu ya
wakopaji, baadhi benki hulipisha hadi asilimia 40 kuepuka hatari ya
kufilisika, alisema.
No comments:
Post a Comment