Wizara
ya Maliasili na Utalii itashiriki katika maeonyesho ya Nanenane ambayo
yatafanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma tangu
tarehe 1 Agosti 2012. Kama kawaida Wizara imeandaa banda moja kubwa
ambalo italitumia pamoja na Mashirika, Wakala, Taasisi zake na wadau wa
Wanyamapori, Misitu, Nyuki Malikale na Utalii.
Maandalizi ya banda la Wizara ya Maasili na Utalii ambalo lina sehemu kuu tano yamekamilika. Sehemu hizo tano ni:
(i) banda kuu ambapo maelezo yatatolewa na machapisho kugawiwa kwa wageni,
(ii) Bustani ya miti;
(iii) Shamba la Nyuki;
(iv) Wanyamapori hai;
(v) Mashindano ya ufugaji Bora wa nyuki bora.
Katika
sehemu ya Wanyamapori hai kutakuwa na aina 20 za wanyama. Leo jioni
tarehe 29/7/2012 Wanyama watakaowekwa kwenye mabanda maalum
yaliyoandaliwa tayari kwa maonyesho ni Simba, Chui, Tumbili, Kobe, Kanu,
Fisi madoa, Fisi Mraba, Sokwe Mtu na Chatu. Wanyama wengine na ndege
watawasili leo usiku tayari kuwekwa kwenye mabanda yao kesho.
Aidha
katika banda la Maliasili kutakuwa na maonyesho ya asali kitaifa ambayo
yameandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwa njia ya ushindani.
Katika mashindano hayo wafugaji wa nyuki walitembelewa na wataalam
katika sehemu wanakofugia na kushindanishwa kwa kuzingatia ufanisi
katika ufugaji na utunzaji bora wa mazao ya nyuki hususan asali.
Washindi watapewa zawadi na Mgeni Rasmi siku ya kilele cha maonyesho
haya ya Nanenane tarehe 8/8/2012.
Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu ni: “Kilimo Kwanza: Zalisha kisayansi na kitekenolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la mahitaji ya watu”.
Kutokana
na kauli mbiu hiyo Wizara itawelimisha wananchi kuhusu uhusiano wa
shughuli za Maliasili na Utalii na “Kilimo Kwanza”. Kwa mfano wananchi
wataombwa kuhifadhi misitu na kupanda miti kwa kuwa misitu inachangia
katika kuleta mvua inayofanikisha kilimo. Vilevile vyanzo vya mito
inayofanikisha kilimo cha umwagiliaji ni katika misitu.
Aidha
wanyamapori hufanikisha utalii ambao huchangia asilimia 26 ya pato la
fedha za kigeni nchini. Fedha hizo za kigeni zinatumika katika kununulia
zana za kilimo, kama vile matrekta. Pia biashara ya mazao ya Maliasili
huleta maduhuli ambayo yanapelekwa Hazina na hatimaye kutumika katika
kufanikisha kilimo, kama vile kununua pembejeo.
Wananchi
wanaoishi katika mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani wanakaribishwa
kutembelea banda la Maliasili katika maonyesho ya Nanenane Dodoma ili
wapate utaalam wa kushiriki katika shughuli za kuhifadhi na kuendeleza
Maliasili kwa manufa yao.
[MWISHO]George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Tarehe 29 Julai 2012
No comments:
Post a Comment