My Web

Emmanuel

CONTACT

Friday, June 29, 2012

Dk Ulimboka akiendelea kupata matibabu

Dkt. Ulimboka akiwa katika hali mbaya mara baada ya kuokotwa akiwa hajitambui. Inadaiwa Ulimboka alitekwa jana mida ya saa 6 usiku baada ya kupigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Abeid na alitekwa na watu wawili waliokuwa na silaha. Kufuatia hali hii wafanyakazi wa chumba cha maiti Muhimbili nao wamegoma na mgomo huenda ukawa mkubwa zaidi!












HAPA AKIWA HOSPITALINI 






Dk Ulimboka akiendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa 
Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).




Na Waandishi Wetu
NYUMA ya kipigo alichopewa kiongozi wa madaktari ambao wako kwenye mgomo nchi nzima, Dk. Steven Ulimboka kuna siri nzito, Ijumaa lina ripoti kamili.
Gazeti hili lilinyetishiwa mkanda mzima na mtu aliyekuwa na Dk. Ulimboka (jina tunalo ambaye naye ni daktari) usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

MUVI LA MATESO LAANZA
Jamaa huyo alidai kuwa, wakiwa viwanjani hapo wakipooza koo, walifika watu watano waliojitambulisha kuwa ni askari wakiwa na silaha ambapo walidai kuwa walimfuata Dk. Ulimboka na kumwambia anatakiwa Kituo cha Polisi Kati (Central).
Ilidaiwa kuwa Dk. Ulimboka alishurutishwa kupanda kwenye gari leusi ambalo halikuwa na namba za usajili na kuondoka eneo hilo huku akiacha gumzo kuwa Central anapelekwa kwa ishu gani.
Ikadaiwa kuwa baada ya Dk. Ulimboka kuchukuliwa, marafiki zake walitoka spidi kuelekea Central kujua kulikoni na pia kumwekea dhamana.
Jamaa huyo alidai kuwa marafiki zake walipofika Central hawakumkuta na wala hakukuwa na dalili za Dk. Ulimboka kufikishwa mahali hapo.
Aliendelea kudai kuwa walianza kufanya mawasiliano usiku huo ili kujua rafiki yao alipelekwa wapi lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.



SIMU HAIPATIKANI
Alidai wakiwa Central, askari mmoja aliwataka kutulia hadi asubuhi wangepata taarifa kamili kwani kwa wakati huo hata simu yake ilikuwa haipatikani.
Jamaa huyo alidai kuwa saa 12:00 asubuhi alipokea simu kutoka kwa msamaria mwema aliyekuwa maeneo ya Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar akamwambia kuna mtu amemkuta akiwa taabani ambaye alimtajia namba kwa shida ili aipige na kutoa taarifa ya hali yake.
“Alisema alimtajia namba tu na hakumsesha tena,” alisema rafiki huyo wa Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa baada ya kujulishwa habari hiyo alitaka aende mwenyewe lakini alipoomba ushauri watu walimsihi asiende peke yake.
Jamaa huyo alisema alitafuta watu akaenda nao na walipofika huko walimkuta Dk. Ulimboka aliyechukuliwa akiwa mzima hajitambui na hakuwa na uwezo wa kuzungumza.
Alisema kuwa baada ya kumuona mwenzao alivyochakazwa, wakamchukua na kumpeleka kwenye Kituo cha Polisi cha Bunju ambapo yule msamaria mwema alitoa maelezo jinsi alivyomkuta.
Rafiki huyo wa Dk. Ulimboka alidai kuwa, katika maelezo ya yule msamaria mwema alisema kuwa alishtuka alipomkuta akiwa porini na hali mbaya huku akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni na kutapakaa madonda mabichi mwili mzima.
Baada ya kuchukuliwa maelezo walipatiwa PF-3 ambapo walifanya jitihada za kumkimbiza katika Hospitali ya Muhimbili kwa kutumia ambulance ya AAR, alipofikishwa tu madaktari wenzake walianza kumpa matibabu ya hali ya juu ili kunusuru uhai wake huku mgomo wao ukiendelea.

MTU ALA KIPIGO
Wakati anafikishwa Muhimbili tayari wanaharakati mbalimbali walishajitokeza ili kumpokea lakini mara baada ya kufikisha mtu mmoja aliyesadikiwa kuwa ‘njagu’ aliingia chooni na akasikika akizungumza na simu.
Ilidaiwa kuwa katika mazungumzo yake alisikika akisema kumbe jamaa hajafa, jambo lililoibua hisia kwamba alijua kilichoendelea.
Ilisemekana kuwa watu waliomsikia wakamchomoa na kumpa kipigo cha mbwa mwizi hadi Radio Call inayotumiwa na polisi ikamchomoka kwenye suruali kabla ya askari waliokuwa doria kumwokoa na kuondoka naye.

KOVA ATHIBITISHA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo linalodaiwa kuwa la utekaji na kuongeza kuwa uchunguzi unafanyika na sheria itachukua mkondo wake dhidi ya wahusika.
Wananchi waishauri serikali
Wakiongea na Ijumaa mara baada ya tukio hilo kutokea, baadhi ya wananchi wameitaka serikali kuhakikisha uchunguzi wa kina na wa haraka unafanyika na ripoti yake kuwekwa hadharani ili kuondoa utata uliotawala.

ASEMA ATAANIKA KILA KITU BAADAYE, ASEMA ACHWE APUMZIKE, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI WANAOMTIBU ASEMA ALING'OLEWA KUCHA, MENO MAWILI NA KUPATA MTIKISIKO WA UBONGO
Geofrey Nyang'oro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya  usiku wa kumkia juzi, kisha kutupwa  Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema atazungumza kwa kina yote yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe auguze maumivu makali yanayomkabili.

Dk Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.

Jana, Dk Ulimboka ambaye amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa haijatengemaa vyema, alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali anaendelea vizuri ikilinganishwa na siku ya kwanza.

Dk Ulimboka alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na kutupwa msituni.



Hata hivyo, hadi sasa wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi huyo wa madaktari, bado limetanda.

Siri nzito
Akisimulia mkasa huo kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema, akiwa katika klabu hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa atokee Tandika na baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia vibaya tofauti na siku nyingine na kuongeza;  "Yaani  sikuwa na amani."

Alisema, "Mara, katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk Ulimboka)," alieleza na kuongeza:

"Sijakaa sawa, nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."

Hata hivyo, jana Dk Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala yake alirekodiwa, na Mwananchi kupata sauti yake  akijibu swali kuhusu hali yake na tukio hilo,  baada ya uongozi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.

Daktari huyo wa magonjwa ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

"Kidogo najisikia nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina maumivu makali. Kwa hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu yeyote anayetaka kuniona pengine hilo jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti hiyo ya Dk Ulimboka.

Lakini, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka, kuna ulinzi mkali wa madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo tu kwa sababu za kutaka aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu ovyo.

Madaktari wanaolinda eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo tutahakikisha sisi wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.

Kiongozi jopo la madaktari

Katika hatua nyingine, kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka, Profesa Joseph Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka ana majeraha mwili mzima.

“Ingawa kwa sasa anaendelea vizuri, Dk Ulimboka  ameumia sana, kwani mwili wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji hao,”alisema Profesa Kahamba na kuongeza:

“Aliumia mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha za vidole na kichwani  na kinywani, ambako aling’olewa meno mawili,”alisema.

Alifafanua kwamba, kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la mtikisiko wa ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na harakati za kuokoa maisha yake.

Uongozi wa Moi watoa neno

Uongozi wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa bado amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.

Msemaji wa Moi, Almas Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali yake kuendelea vizuri, lakini  haingewezekana kwa waandishi wa habari kuingia ndani ya chumba alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.

“Mgonjwa anaendelea vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua watu wanaokwenda kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi imeshindikana kwa sababu yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu wake,”alisema Jumaa.

Jumaa aliongeza kwamba ili mtu aweze kuingia wodini   analazimika kuvaa vazi maalumu na mavazi yaliyopo, yasingetosha, lakini pia wapo watu wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.

Tamko la Jumuiya ya Madaktari

Wakati hali ya Dk Ulimboka ikiwa hivyo, madaktari wameipinga tume ya uchunguzi iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza suala hilo, wakidai mazingira ya tukio hayaliondoi jeshi hilo kuhusika.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage aliwaambia waandishi wa habari kuwa wangependa kuundwa kwa tume huru itakayofanya kazi ya kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma.

“Madaktari kwa ujumla wetu tunalaani tukio la kutekwa nyara,kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande, lakini pia hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kwa sababu mazingira ya tukio hayaondoi kuhusika ama kutohusika kwa jeshi hilo,”alisema Dk Chitage.

Chitage alitoa msimamo wa madaktari kuwa ni kuendelea na mgomo, huku akionya Serikali kuacha vitendo vya kuwatisha, kwa madai kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa suluhu ya mgogoro kati ya pande hizo mbili.

“Kumekuwa na vitisho kwa madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza. Tunaionya Serikali kuacha mara moja na itambue kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kwa namna nyingine yoyote bali ni kwa Serikali kutekeleza madai ya madaktari,”alisema Chitega na kuongeza:

“Sisi madaktari kwa umoja wetu, tumechoka kushuhudia Watanzania wakipoteza maisha kwa magonjwa tunayoweza kuyatibu, kufanya kazi katika mazingira magumu huku kukiwa hakuna mipango ya kuboresha mazingira ya kazi, kukosekana kwa dawa na vifaa tiba.”

Mgomo huo wa madaktari leo unaingia siku ya saba tangu ulipotangazwa na mwenyekiti huyo kuwa, ungeanza rasmi Jumamosi iliyopita.




Katibu wa Jumuiya ya Madaktari,Dk Edwin Chitage akitoa tamko la Jumuia hiyo kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam la kutokuwa na imani na Tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la kupigwa kwa Mwenyekiti wao Dk Stephen Ulimboka.Picha na Fidelis Felix




Waandishi Wetu
TUKIO la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa vibaya, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, limechochea kasi ya mgomo baada ya madaktari bingwa kutangaza kujitosa rasmi kwenye mgogoro huo.Awali madaktari hao hawakushiriki mgomo huo, lakini jana walieleza kwa nyakati tofauti kuwa, wameamua kuungana na 
wenzao kutokana na unyama aliofanyiwa kiongozi wao akiwa katika harakati za kutetea na kupigania haki zao.

Madaktari hao wa hospitali za Muhimbili, Moi, KCMC, Mbeya, Bugando na Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuwa wameingia kwenye mgomo huo kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali kutoa tamko kuhusu utata wa tukio hilo.

Tukio hilo la aina yake kutokea nchini, limeathiri upatikanaji wa huduma zote za matibabu katika hospitali hizo, huku madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Moi, wakielekeza nguvu zao kunusuru maisha ya mwenzao aliyeumizwa.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgomo huo utaendelea hadi hapo Serikali itakapotekeleza madai yao.

"Tunaitaka Serikali kuacha vitisho kwa madaktari nchini, tunaitaka itambue kwamba mgogoro huu hauwezi kumalizwa kwa njia yoyote vikiwemo vitisho bali ni kwa kukaa meza ya majadiliano na kukubaliana na madaktari," alisema Dk Chitega na kuongeza:

"Ninawashukuru madaktari wote nchi nzima, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla wao kwa kusitisha huduma baada ya kupigwa mwenzetu. Tunaomba mshikamano huu uendelee," alisema Dk Chitega.

Gazeti hili lilishuhudia wagonjwa wakiwa wamekaa katika makundi bila kujua la kufanya, huku wengine wakiamua kuondoka na kwenda hospitali binafsi.

Waliliambia Mwananchi kwamba kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kuungana na madaktari hao kuitaka Serikali kutatua mgogoro huo haraka.

Wagonjwa waliofika katika eneo hili pia walielezwa bayana na maofisa wa Moi kwamba huduma zimesitishwa  kutokana na madaktari kugoma.

Ocean Road

Madaktari bingwa katika Taasisi ya Ocean Road nao waligoma kutoa huduma hatua iliyozua taharuki kwa wagonjwa waliofika kwa ajili ya matibabu.

Gazeti hili lilishuhudia ofisi za madaktari hao zikiwa zimefungwa na hata zile ambazo zilikuwa wazi, madaktari hawakuwapo.

Mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Dachi, alisema kuwa, wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikishwa mapokezi, lakini wanachukua muda mrefu kumuona daktari.


Mgomo huo pia umeendelea katika Hospitali ya Amana wilayani Ilala huku uongozi wa hospitali hiyo ambao uligoma kuzungumza na vyombo vya habari, ukihaha kunusuru hali hiyo.

Katika Hospitali za Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.

Mbeya

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,madaktari bingwa ambao awali hawakugoma jana waliingia kwenye mgomo na kusababisha wagonjwa katika hospitali hiyo hususan kitengo cha wazazi, kusota bila matibabu.

Habari kutoka katika hospitali hiyo zilieleza kuwa hivi sasa madaktari bingwa wanatoa huduma kwa kujuana.

Mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya yao kimewakatisha tamaa.

Alisema kuwa, hali hiyo sasa imehamia hadi katika Kituo cha Wazazi cha Meta na kufafanua kuwa hali ni mbaya, tayari wajawazito wametakiwa kuhamia katika Hospitali ya Mkoa ambayo imefurika wagonjwa.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa, Dk Eliuter Samky hakuweza kuzungumzia tukio hilo jana kutokana na kile kilichoelezwa na katibu wake muhtasi kwamba ana kazi nyingi.

Mwanza
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mkoani Mwanza nao wamegoma, huku kiongozi wa Kamati Ndogo ya hospitali hiyo inayoshughulikia migomo, akikataa kuzungumzia hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baada ya kutoonekana katika maeneo ya hospitali, mmoja wa viongozi wa Kamati hiyo, Dk Geogre Adrian, alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi suala hilo na kwamba kufanya hivyo, ni kwenda kinyume na maagizo aliyopewa na Kamati Kuu.


Akizungumzia huduma katika hospitali hiyo alisema kuwa hajui lolote kwa kuwa hawajagusa maeneo ya kazi kwani  wapo kwenye mgomo.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia huduma katika hospitali yake, hakupatikana.

Watimuliwa
Jana Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alitoa tangazo la kuwataka madaktari waliopo mafunzoni ‘Interns’ katika hospitali hiyo kurejea kazini na kama watakiuka agizo hilo, watakuwa wamejifukuzisha wenyewe.


Manyara
Mkoani Manyara, madaktari kumi katika Hospitali ya Haydom Wilaya ya Mbulu wamegoma tangu juzi.Idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), inaongezeka siku hadi siku.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina yao, madaktari hao ambao wanafanya mafunzo ya vitendo katika hospitali hiyo, wamesema kuwa hawatatibu wagonjwa mpaka madai yao yatekelezwe.


Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo na kufafanua kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi.

Choya alisema kuwa madaktari wanaoendelea na kazi, wameelemewa  kutokana na wagonjwa kuwa wengi.

Alisema kati ya madaktari 11 wanaosoma kwa vitendo hospitalini hapo, mmoja tu anayesomeshwa na hospitali hiyo, ndiye hajagoma.

KCMC
 Hali katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro imezidi kuwa tete na kuwafanya ndugu kuwahamishia wagonjwa wao katika hospitali binafsi.

Mwananchi lilitembelea wodi za hospitali hiyo na kukuta vitanda vikiwa wazi.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye mgomo kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hawako tayari kurudi kazini kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Dodoma
 Wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana walijikuta wakipata taabu baada ya madaktari wa hospitali hiyo kusitisha huduma kwa takriban saa sita kuanzia asubuhi.

Muda wa mchana utoaji huduma katika hospitali hiyo uliendelea ingawa kwa  kusuasua.

Tofauti na siku zote, jana chumba cha daktari kilichokuwa wazi ni kimoja tu hali iliyosababisha msongamano mkubwa.


Arusha

Mjini Arusha, madaktari wameendelea na mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kusababisha kudorora huduma huku wagonjwa kadhaa wakiondolewa hospitalini hapo.

Mgomo huo, ulianza saa 1 asubuhi hadi saa 6:00 mchana, ambapo madaktari na wauguzi,waligoma kutoa huduma wakitaka kujua hatima ya Dk Ulimboka. Walitaka pia kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo na waandishi wa habari, kuhusu mgogoro wao.

Askari anyimwa huduma

Askari wa Usalama Barabarani ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye alipata ajali jana, alijikuta akishindwa kuhudumiwa katika hospitali ya Mount Meru na kuondolewa kutokana na mgomo huo.

Askari huyo, aliyevaa sare, alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 asubuhi akiwa kwenye teksi, lakini wauguzi waliokuwa zamu walishauri apelekwe sehemu nyingine.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali ya mkoa, ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Omar Chande, jana ulifanya kazi ya ziada ya kuwabembeleza madaktari hao, kurejea kazini, kusubiri uamuzi wa Serikali.



Mgomo, Dk Ulimboka
vyateka Bunge

Mgomo wa madaktari na kutekwa kisha kupigwa Dk Ulimboka jana vilitawala mjadala wa Bunge hadi pale Spika Anne Makinda alipotoa mwongozo kwamba suala hilo lisijadiliwe kwani liko mahakamani.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa juzi pale alipokuwa akizungumzia mgomo wa madaktari na kuhitimisha kwamba Serikali ilikuwa inajiandaa kutoa kauli na msimamo wake hivyo “liwalo na liwe’.

Pinda alilazimika kutoa maelezo kutokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kufahamu maana ya kauli ya Waziri Mkuu ambayo aliita kuwa ni nzito na iliyozua mjadala mkali nchini.

Kadhalika, Mbowe alitaka kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma za tiba kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba madaktari katika hospitali kadhaa walikuwa wakiendelea na mgomo.


Kadhalika Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alimuuliza Pinda kwamba haoni kwamba ni busara kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ahadi yake kwamba mgomo wa madaktari usingetokea, lakini ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka.

Akimjibu Mbowe, Pinda alikiri kutoa kauli hiyo ndani ya Bunge juzi na kusema alifanya hivyo akiamini kuwa jambo hilo lilikuwa mahakamani na akasema asingeweza kusema jambo lolote kwa kuwa hana tabia ya kuwa na utovu wa nidhamu wa kuingilia mambo ya mahakamani.

Hata hivyo, alijitetea kuwa kabla ya kutoa kauli hiyo bungeni juzi, hakuwa na taarifa kuhusu tukio la kupigwa kwa Ulimboka na akasema kuwa, kauli yake haihusiani kabisa na Serikali kuhusika katika jambo hilo kwa namna yoyote ile.

Waziri Mkuu alisema tayari amekwishaagiza vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya haraka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki mara moja.

“Kwanza namtakia afya njema ndugu Ulimboka, na mimi nataka Watanzania waamini kuwa tulikuwa katika mazungumzo mazuri na madaktari chini yake Ulimboka hivyo tukio hilo ambalo limetokea katika mazingira magumu limetushtua kweli, kama ni Serikali basi ingekuwa ni Serikali ya ajabu kweli,’’alisema Pinda.

Kuhusu namna ya kusaidia Watanzania wasiathirike na mgomo huo, alisema tayari Serikali imeshaagiza madaktari kutoka wizarani kutumika na kuwaomba waliostaafu kutoa huduma katika kipindi hicho kigumu.

Mkakati mwingine ni pamoja na kutumia hospitali za Jeshi ikiwamo Lugalo waanze kutoa huduma hizo wakati Serikali inaendelea kuzungumza kwa utaratibu na madaktari.

Lissu aliuliza swali la nyongeza kumtaka Pinda kuachia ngazi hali iliyosababisha mvutano kwani Waziri Mkuu alikosoa uulizaji wa swali hilo kuwa halikustahili.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la madaktari akitaka taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilifanyia kazi suala la mgomo wa madaktari ijadiliwe bungeni.

Hata hivyo, Spika Makinda alisema ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa kwani tayari Serikali ilishakabidhiwa kwa ajili ya kuifanyia kazi na kwamba mapendekezo ya Bunge kupitia ripoti hiyo yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.


Habari hii imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Godfrey Kahango,Mbeya, Joseph Lyimo,Mbulu, Sheilla Sezzy,Mwanza, Rehema Matowo, Moshi, Masoud Masasi,Dodoma, Fidelis Butahe, Geofrey Nyang'oro Dar, Mussa Juma, Arusha, Bakari Kiango na Victoria Mhagama

No comments:

Post a Comment

New